Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gaza: Imegubikwa na joto kali, mapigano na dalili dhahiri za udumavu kwa watoto

Watoto wawili katika makazi ya shule ya UNRWA huko Khan Younis, kusini mwa Gaza, wakielekea kuchota maji.
UNRWA/Fadi
Watoto wawili katika makazi ya shule ya UNRWA huko Khan Younis, kusini mwa Gaza, wakielekea kuchota maji.

Gaza: Imegubikwa na joto kali, mapigano na dalili dhahiri za udumavu kwa watoto

Amani na Usalama

Uhaba mkubwa wa huduma muhimu kwenye eneo lililozingirwa huko Ukanda wa Gaza umeacha watu wengi walio hatarini wakiendelea kuhaha kuishi huku joto kali, mapigano makali nayo yakiendelea na magonjwa yakisambaa, na ukosefu wa utawala wa sheria nao ukishamiri, yamesema mashirika ya Umoja wa Mataifa ya kutoa misaada ya kiutu hii leo.

Mathalani shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula, WFP limesisitiza tena hofu yake kubwa ya kwamba watu waliofurushwa makwao kutoka kusini mwa Gaza wanaendelea kukumbwa na kiwewe kwani sasa wamalundikana kwenye eneo jembamba la ufukwe joto likiwa kali kupindukia.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa WFP, Carl Skau awali alisema kuwa “vita inayoendelea na ukosefu wa sheria” vimefanya hali kuwa ngumu zaidi kwa WFP na wadau wake kukidhi mahitaji ya wakazi wa Gaza hivi sasa.

Dalili dhahiri za udumavu

Watoto wachanga hivi sasa ni miongoni mwa watu wanaokosa huduma muhimu kwani maziwa yao ya kopo hakuna sambamba na virutubisho vya lishe kwa watoto, wajawazito na akina mama wanaonyonyesha watoto, imesema Ofisi ya Umoja wa  Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA.

“Licha ya dalili dhahiri za udumavu miongoni mwa watoto, hakuna taratibu zozote zilizofanyika za kuchunguza kiwango cha utapiamlo na kutibu wale wanaobainika kuwa na utapiamlo, na hii ni kutokana na uwezo mdogo ulioko,” imesema OCHA kupitia ripoti  yake iliyochapishwa Jumatano.

Huduma kwa wajawazito na akina mama waliojifungua hakuna na katika maeneo mengine ya wakimbizi vituo vya afya vinafanya kazi kwa saa chache,  bila dawa za kutosha na kuna ripoti za wajawazito kujifungua katika mazingira ya dharura nyakati za usiku wa manane huko kwenye mahema ya wakimbizi bila msaada wowote wa wahudumu wa afya, imesema OCHA.

Watu wanazidi kuondoka Rafah

Wakati huo huo, jimbo la Rafah lililoko kusini kabisa kwa Gaza, linaendelea kusalia tupu kwani watu wanakimbia mashambulizi ya makombora. OCHA imenukuu makadirio ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA ambayo yanaonsha kwamba ni watu wapatao 65,000 tu ndio wamesalia Rafah. Wiki sita zilizopita kabla Israeli haijatoa amri ya watu kuondoka Rafah, kulikuweko na watu milioni 1.4.

“Katika maeneo ya wakimbizi, watu wamerundikana kwenye makazi ya mud ana mahema, ambayo kwa sasa yanahitaji ukarabati kwa kuwa yameraruka na hayatoi hifadhi ya kutosha wakati huu wa joto kali,” imesema OCHA ikiangazia tathmini yake ya hivi karibuni kwenye maeneo ya wakimbizi ya Deir al Balah, Khan Younis na Al Mawasi – yenye jumla ya watu zaidi ya 130,000.

Katika hatua nyingine, OCHA imeripoti pia kwa mara ya kwanza tangu mapema mwezi huu wa Juni, malori matano yenye nishati ya mafuta yameingia Gaza. Ingawa hivyo bado kuna uhaba “kwa kuwa hakuna nishati yoyote ya mafuta imeingia Gaza katika wiki mbili zilizopita.”