Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Natamani watoto wangu waliomaliza kidato cha 6 waingie Chuo Kikuu – Mkimbizi kutoka DRC

Mnenenwa Mkangwa, mkimbizi kutoka DRC anayeishi kambini Nyarugusu, mkoani Kigoma nchini Tanzania. Ameishi kambini kwa miaka 28 na anatamani watoto wake wapate elimu ya Chuo Kikuu.
UNHCR/Maimuna Mtengela
Mnenenwa Mkangwa, mkimbizi kutoka DRC anayeishi kambini Nyarugusu, mkoani Kigoma nchini Tanzania. Ameishi kambini kwa miaka 28 na anatamani watoto wake wapate elimu ya Chuo Kikuu.

Natamani watoto wangu waliomaliza kidato cha 6 waingie Chuo Kikuu – Mkimbizi kutoka DRC

Wahamiaji na Wakimbizi

Hii leo tuko kambi ya wakimbizi ya Nyarugu mkoani Kigoma, kaskazini-magharibi mwa Tanzania, taifa lililoko Afrika Mashariki likihifadhi wakimbizi wakiwemo wale wanaotoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Na ikiwa leo ni siku ya wakimbizi duniani tunakutana na Mmenenwa Mkangwa, baba wa familia mwenye umri wa miaka 64. Yeye ana watoto 7 na anatoka DRC.

Akizungumza na Maimuna Mtengela, Afisa kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR nchini Tanzania, Bwana Mkangwa anasema alikimbilia Tanzania akitokea DRC mwaka 1996 akiwa na umri wa miaka 36, wakati huo alikuwa na mke, watoto wawili pamoja na mama yake mzazi ambaye alikuwa ni mgonjwa wa kupooza asiyeweza kujihudumia.

Ilikuwaje siku alipoamua kukimbia DRC?

Anakumbuka siku alipoamua kuacha makazi yao, nyumba, mifugo na bustani nzuri ya mboga mboga. “Ulikuwa ni uamuzi wa ghafla, lakini ambao tulitarajia ungeweza kutokea. Wiki mbili kabla tulisikia kuna machafuko na ingewezekana yangefika kijijini kwetu. Tulijawa na hofu, kwa wiki hizo zote tulilala tukiwa tumevaa nguo na viatu na fedha kidogo ambazo zilikuwa ni akiba ya familia nililala nazo kila siku. Majirani wengine walilala nje ya nyumba zao kuhofia kuvamiwa usiku.”

Haikuwa rahisi kuacha makazi tuliyoyazoea, makazi niliyozaliwa na kukulia hapo. Lakini usiku mmoja tulisikia kelele kutoka banda la mifugo, kijana wangu alitoka nje kwenda kuangalia. Ghafla milio kadhaa ya risasi ikasikika. Nilimpoteza kijana wangu, alipigwa risasi na kufariki pale pale. Mimi na wanafamilia wengine tulikimbia.

Kitu cha thamani nilichobeba kutoka nyumbani ni baiskeli, haikuwa mpya lakini ilinisaidia sana hasa kumbeba mama yangu mgonjwa ambaye alikuwa hajiweza pamoja na watoto. Mke wangu alibeba vyombo vichache ambavyo vingine tulivipoteza tukiwa njiani.

Njaa, jua kali, upepo na baridi ilikuwa ni kawaida njiani

Tulikutana na watu wengi njiani, wengine ni majirani zetu na wengine hatukuweza kufahamiana lakini vita ilitufanya kuwa wamoja. Tulitumia siku nne kutembea porini, mchana tulijificha na usiku tulitumia kutembea ili tusionekane, tuliposikia milio ya risasi ilitulazimu kubadili muelekeo na kujificha. Njaa, jua kali, upepo na baridi hivyo vyote havikunipa wasiwasi, wasiwasi wangu ilikuwa kufika mpakani salama na kupokelewa.

Bwana Mkangwa na familia yake walifanikiwa kuingia katika mpaka wa Tanzania kupitia mkoa wa Kigoma kwa usafiri wa boti kutoka upande wa DRC. Walitumia boti kuvuka ziwa Tanganyika, ziwa la pili dunia kwa kuwa na kina kirefu zaidi. Huko walipokelewa na serikali ya Tanzania, shirika la kuhudumia wakimbizi duniani UNHCR pamoja na wadau wake.

Anaendelea kusimulia, “baada ya kukaa kwenye jumba la pamoja kwa siku kadhaa tulihamishiwa kambini kwenye nyumba za familia, kila familia ilipewa hema la kuishi kama familia, tulipewa mikeka ya kulalia, chakula, huduma ya afya, maji, vyombo vya jikoni, blanketi na sabuni. Huduma za afya tunapata pamoja na watanzania, huwa wanakuja kutoka vijiji jirani na hapa kambini. Hivyo tunakutana nao mara kwa mara.

Maisha kambini Nyarugusu kwa miaka 28

Bado nipo kambini Nyarugusu, kwa miaka 28 sasa, mama yangu mzazi alifariki mwaka 1998 tukiwa hapa kambini. Watoto wangu wanasoma hapa kambini kupitia UNHCR na washirika wake. Watoto wanne wamemaliza kidato cha sita, lakini hakuna elimu ya Chuo Kikuu hapa kambini, hivyo wameshindwa kuendelea na elimu ya juu. Ninatamani sana kama watoto wangu wangeweza kusoma zaidi, kupata kazi nzuri na kuishi maisha ya kujitegemea.

Umri wangu umeenda sasa na afya yangu sio nzuri, siwezi kufanya kazi kuhudumia familia yangu. Ninawategemea watoto wangu ili kunihudumia. Ninatamani sana wasome zaidi waweze kuwa madaktari wa kutegemewa, waweze kusaidia jamii na watu wenye uhitaji. Lakini wengine ninatamani wawe wajenzi, waweze kujenga nyumba na kuhamishia ujuzi wao kwa vizazi vyao hata kama hawatakuwa na elimu kubwa sana.

Ukimbizi si hali nzuri, tulinde amani

Ujumbe wangu katika maaadhimisho ya siku ya wakimbizi ni kuwa, amani ni kitu cha Thamani sana, ukimbizi sio hali nzuri ni hali ambayo inaweza kumpata mtu yeyote wakati wowote. Tumtegemee Mungu na tuilinde amani tuliyo nayo”. Anasema Mmenenwa.

UNHCR Tanzania, inahudumia wakimbizi kutoka DRC na Burundi waliopo katika kambi mbili za wakimbizi ambazo ni Nduta na Nyarugusu zote ziko Kigoma na zinahifadhi zaidi ya wakimbizi 230,000.

Wakimbizi hawa wanahitaji huduma za chakula, elimu, afya, maji, uboreshwaji makazi, utunzanji wa mazingira, huduma kwa wenye mahitaji maalumu na huduma nyingine kadhaa ambazo kwa miaka ya hivi karibuni kutokana na majanga mbalimbali duniani, UNHCR imepungukiwa uwezo wa kuweza kuwahudumia wakimbizi hao kwa kiwango kinachostahili. Rasilimali na misaada zaidi inahitajika ili kuweza kutoa huduma kikamilifu.