Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mamlaka nchini Eritrea yatakiwa kuchukua hatua kuboresha hali ya haki za binadamu

Wanawake wawili wanatembea kando ya barabara nje ya Keren, jiji lililoko katika eneo la Anseba nchini Eritrea.
© UNICEF/Giacomo Pirozzi
Wanawake wawili wanatembea kando ya barabara nje ya Keren, jiji lililoko katika eneo la Anseba nchini Eritrea.

Mamlaka nchini Eritrea yatakiwa kuchukua hatua kuboresha hali ya haki za binadamu

Haki za binadamu

Mamlaka nchini Eritrea imetakiwa kuchukua hatua za haraka kuimarisha rekodi zake za masuala ya haki za binadamu kwa kuhakikisha kuna mageuzi ya maana na kufungua njia kwa jamii ambayo haki za binadamu zinaheshimwa na kila mtu anaweza kustawi. 

Wito huo umetolewa hii leo jijini Geneva Uswisi na Mtaalamu huru wa haki za binadamu kwa nchi ya Eritrea  Mohamed Babiker wakati akiwasilisha ripoti yake ya nne kuhusu hali ya haki za binadamu nchini humo ambayo inaonesha kuna kuendelea kwa matumizi yakuwaweka watu vizuizini kiholela na bila mawasiliano, watu kuendelea kupotea  na matumizi ya wanajeshi na maafisa usalama wanaowalazimisha wananchi kufanya kazi, mateso, na ukandamizaji wa kimfumo wa uhuru wa kimsingi nchini Eritrea.

Kupitia taarifa yake iliyotolewa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu OHCHR Babiker ameeleza kuwa na wasiwasi mkubwa kwani mamlaka za Eritrea zimeonesha nia ndogo ya kushughulikia uvunjwaji wa haki za binadamu.

“Ikiwa ukiukwaji huu unaoendelea hautashughulikiwa, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa waathiriwa wanapata haki, mzunguko wa mateso na ukandamizaji utaendelea, na kudumaza uwezekano wa Eritrea yenye amani na maendeleo.” Ameeleza Babiker

Taarifa hiyo imebainisha kuwa wananchi wengi wamekuwa wakikamatwa na kushikiliwa kiholela bila kufunguliwa mashtaka wala kupata nafasi ya kusikilizwa kikamilifu na mahakama nchini Eritrea humo mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi yamekuwa yakikabiliwa na vikwazo vingi, hivyo kuathiri ustawi wa wananchi wengi jambo ambalo limefanya serikali ya Eritrea kupewa changamoto kubwa ya kuhakikikisha haki za binadamu zinalindwa na kuheshimiwa kikamilifu.

Babiker ameripoti kwamba vikosi vya Eritrea vinaendelea kuwepo na kuendelea kuhusika katika uvunjwaji wa haki za binadamu katika sehemu za mkoa wa Tigray nchini Ethiopia huku akiitaka Jumuiya ya kimataifa kufuatilia kwa karibu nchi hiyo.

Jumuiya ya kimataifa isiwatelekeze waathiriwa wa uvunjwaji wa haki za binadamu wa Eritrea. Mustakabali mwema wa Eritrea unategemea kuhakikisha haki kwa waathiriwa, hili linahitaji shinikizo la kimataifa la kudumu ili kuwawajibisha watekelezaji”

Bwana Mohamed Babiker ambaye ni raia wa Sudan aliteuliwa kuwa Mtaalamu huru kuhusu hali ya Haki za Kibinadamu nchini Eritrea na Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Kibinadamu mwaka 2020.