Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sitamani kurudi nyumbani DRC- Mkimbizi

Bahati Bagarwa, mkimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC akiwa kambini Nyarugusu , mkoani Kigoma, kaskazini magharibi mwa Tanzania.
UNHCR/Maimuna Mtengela
Bahati Bagarwa, mkimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC akiwa kambini Nyarugusu , mkoani Kigoma, kaskazini magharibi mwa Tanzania.

Sitamani kurudi nyumbani DRC- Mkimbizi

Wahamiaji na Wakimbizi

Bahati Bagarwa ana umri wa miaka 58, ni mkimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC anayeishi kambini Nyarugusu mkoani Kigoma, kaskazini-magharibi mwa  Tanzania.

Ni mama wa watoto watatu na ni bibi mwenye wajukuu sita sasa. Bahati alikimbia machafuko ya vita nchini DRC mwaka 1999 baada ya kupoteza watoto watatu.

Akihojiwa na Maimuna Mtengela, afisa wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR nchini Tanzania, Bahati anakumbuka maisha yake kabla ya kuwa mkimbizi.

“Ilikuwa mchana, nilienda shambani kuchimba mihogo kwa ajili ya chakula, nyumbani niliwaacha watoto wangu watatu. Mume wangu alikuwa akijishughulisha na shughuli za uvuvi hivyo alikuwa ziwani. Ghafla niliona watu wengi wanakimbia kutoka kijijini kwetu na kunipita hapo shamba. Baada ya kuwauliza waliniambia vita imeingia kijijini, watoto wangu wameshindwa kukimbia, wameuawa pamoja na watu wengine waliokuwa maeneo ya Jirani.”

Taswira ya kilichotokea imesalia kichwani mwangu

“Hizo zilikuwa habari mbaya sana kuwahi kusikia maishani mwangu, sikuweza tena kurudi nyumbani, sikuwaona tena watoto wangu, hii picha inatembea kila siku kichwani mwangu. Niliondoka vile nilivyokuwa, sikufanikiwa kubeba kitu chochote wala kujiandaa. Sikuwa na wazo lingine zaidi ya kupigania uhai wangu,” anasimulia Bahait huku machozi yakimlengalenga.

Kama lilivyo jina lake, kwa bahati nzuri aliweza kukutana na mume wake pembezoni mwa ziwa Tanganyika ambaye alikuwa ameshapata taarifa ya vita na hakuweza kurudi nyumbani. Kwa pamoja wakaungana ili kuvuka ng’ambo ya pili kuingia Tanzania kunusuru maisha yao na kuomba hifadhi.

Bahati Bagarwa, mkimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, (kushoto) akiwa na mume wake kwenye kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu, mkoani Kigoma, kaskazini magharibi mwa Tanzania.
UNHCR/Maimuna Mtengela
Bahati Bagarwa, mkimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, (kushoto) akiwa na mume wake kwenye kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu, mkoani Kigoma, kaskazini magharibi mwa Tanzania.

Sikuweza kumweleza mume wangu kuhusu vifo vya watoto wetu

“Mume wangu aliniuliza kuhusu watoto, sikuwa na jibu zaidi ya machozi tu. Ningemueleza vipi kuwa watoto wote watatu wameuawa na tumebaki sisi wawili pekee kati ya familia ya watu watano? Ndugu wengi pia waliuawa kwenye vita. Tulibaki sisi tu, wawili,” alisema Bahati huku akiuliza swali hilo lisilo na jibu.

Kuvuka ziwa Tanganyika hadi Tanzania na kupata watoto 3

Bahati na mume wake pamoja na jamaa wengine walifanikiwa kuingia Tanzania wakiwa salama. Walipokelewa na serikali ya Tanzania pamoja na UNHCR na mashirika mengine yaliyokuwa yakitoa misaada ya kibinadamu. Kama ilivyo taratibu baada ya kupokelewa walipelekwa katika kambi ya wakimbizi ya Rugufu kabla ya kuhamishiwa kambini Nyarugusu.

Msaada kutoka UNHCR na biashara ndogo ndogo

Kwa sasa Bahati ni mama wa watoto watatu ambao aliwapata baada ya kukimbia kutoka DRC. Anajishughulisha na uuzaji wa karanga, mihogo na miwa. Bidhaa hizi huzipata kutoka kwa watanzania ambao huwauzia bidhaa mbalimbali kambini kwa kibali maalum.

Bahati anakiri kwamba faida ya biashara yake ni ndogo sana, lakini hawezi kuacha sababu sio sawa na kukaa bure. Kupitia biashara hii, yeye na familia yake wana uwezo wa kubadilisha mboga na kununua mahitaji madogo madogo ya nyumbani.

“Kila mkimbizi anapokea kipande kimoja cha sabuni gramu 250 kwa mwezi, kipande hiki tunatakiwa kutumia kwa matumizi yote kufua, kuoga, kuosha vyombo na matumizi yote yanayohitaji sabuni. Biashara hii ndogo inanisaidia sana, ninaweza kununua sabuni ya ziada, kununua mahitaji ya watoto na hata chakula kikiisha kabla ya muda.

Ndoto yangu ni kuondokana na ukimbizi

Ndoto yangu kubwa ni kuondoka katika hali ya ukimbizi, kuwa na maisha mengine tofauti na haya. Watoto wapate elimu wajenge maisha yao, kwa sababu kwa sasa wanaishi maisha ambayo ninaona kabisa sio yao, ni maisha yangu ambayo sio mazuri.

Sitamani maisha haya kwa mtu yoyote. Sitamani kurudi DRC maana huko itakuwa kurudisha kumbukumbu mbaya za maisha yangu, ni bora nife hapa lakini sio DRC.”

Bahati anamalizia kwa kuomba huduma na misaada ya kibinadamu iweze kuboreshwa zaidi kambini Nyarugusu, hasa huduma za afya kwa wazee, wajawazito na watoto.