Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fahamu kuhusu siku ya wakimbizi duniani: UNHCR

Kampeni ya Umoja wa Mataifa  ya sio tu kuwakumbuka wakimbizi bali pia kuwajumuisha kwa michezo kama vile ya kandanda.
Yasmine Eldemerdash
Kampeni ya Umoja wa Mataifa ya sio tu kuwakumbuka wakimbizi bali pia kuwajumuisha kwa michezo kama vile ya kandanda.

Fahamu kuhusu siku ya wakimbizi duniani: UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Fahamu kuhusu siku ya wakimbizi duniani, ilipoanza, umuhimu wake, na kwa nini inaadhimishwa kila mwaka na Umoja wa Mataifa na duniani kote.

Siku ya Wakimbizi Duniani ni nini?

Siku ya Wakimbizi Duniani ni siku ya kimataifa iliyoteuliwa na Umoja wa Mataifa kuwaenzi wakimbizi kote duniani. 

Huangukia kila mwaka tarehe 20 Juni na huadhimisha nguvu na ujasiri wa watu ambao wamelazimika kukimbia nchi zao ili kuepuka migogoro au mateso.

Mkimbizi wa Sudan ameketi na mapacha wake wa miezi mitatu katika kituo cha b kinachoungwa mkono na UNICEF
© UNICEF/Donaig Le Du
Mkimbizi wa Sudan ameketi na mapacha wake wa miezi mitatu katika kituo cha b kinachoungwa mkono na UNICEF

Kwa nini Siku ya Wakimbizi Duniani ni muhimu?

Siku ya Wakimbizi Duniani inaangazia haki, mahitaji na ndoto za wakimbizi, kusaidia kuhamasisha utashi wa kisiasa na rasilimali ili wakimbizi wasiweze kuishi tu bali kustawi. 

Ingawa ni muhimu kulinda na kuboresha maisha ya wakimbizi kila siku, siku za kimataifa kama vile Siku ya Wakimbizi Duniani husaidia Ulimwengu kuangazia juu ya masaibu ya wale wanaokimbia migogoro au mateso. 

Shughuli nyingi zinazofanyika Siku ya Wakimbizi Duniani hutengeneza fursa za kusaidia wakimbizi.

Kuna wakimbizi wangapi duniani? 

Ripoti ya kimataifa ya miendendo ya uhamaji ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR 2024 iliyochapishwa mwezi huu wa Juni mjini Geneva Uswisi imebaini kuwa watu waliolazimika kuyahama makazi yao waliongezeka hadi watu milioni 120 katika mwezi Mei 2024 na mchangiaji Mkubwa wa watu kufurushwa makwao ni vita.

Nchi tano zimekuwa na idadi kubwa ya wakimbizi ambazo ni Sudan, Syria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Myanmar na Gaza.

Na katika miaka mitano iliyopita UNHCR inasema kumekuwa na ongezeko la watu milioni 68.3 waliokimbia makwao sawa na ongezeko la asilimia 50.

Wakimbizi wa Burundi katika makazi ya Mulongwe huko Kivu Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. (Maktaba)
© UNHCR/Georgina Goodwin
Wakimbizi wa Burundi katika makazi ya Mulongwe huko Kivu Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. (Maktaba)

Sababu zinazochangia kuwepo kwa wakimbizi

Kwa mujishu wa shirika la UNHCR, kuna sababu nyingi kwa nini inaweza kuwa vigumu sana au hatari kwa watu kukaa katika nchi zao. 

Kwa mfano, watoto, wanawake na wanaume hukimbia vurugu, vita, njaa, umaskini uliokithiri, pia kwa sababu ya mwelekeo wao wa kijinsia, au kutokana na matokeo ya mabadiliko ya tabianchi kama vile ukame, mafuriko, vimbunga au majanga mengine ya asili kama matetemeko ya ardhi, moto wa nyika, Tsunami, momonyoko wa udongo na kadhalika.

Siku ya Wakimbizi Duniani ni lini na ilianza lini?

Siku ya Wakimbizi Duniani huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 20 Juni na ni maalumu kwa ajili ya wakimbizi kote duniani. 

Siku ya Wakimbizi Duniani ilifanyika duniani kote kwa mara ya kwanza tarehe 20 Juni 2001 ili kuadhimisha miaka 50 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 1951 unaohusiana na Hadhi ya Wakimbizi. 

Hapo awali ilijulikana kama Siku ya Wakimbizi Afrika, kabla ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuiteua rasmi kuwa siku ya kimataifa mwezi Desemba 2000.

Abdirahman Sheuna (mwenye jezi nyekundu) akiwania mpira dhidi ya wachezaji kutoka shule ya msingi ya mtaani kwenye "Tamasha la Kakuma la Kandanda kwa Shule"...
© UNHCR/Samuel Otieno
Abdirahman Sheuna (mwenye jezi nyekundu) akiwania mpira dhidi ya wachezaji kutoka shule ya msingi ya mtaani kwenye "Tamasha la Kakuma la Kandanda kwa Shule"...

Je, nini kinatokea katika Siku ya Wakimbizi Duniani?

Kila mwaka, Siku ya Wakimbizi Duniani huadhimishwa na matukio mbalimbali katika nchi nyingi duniani kote kuunga mkono wakimbizi. 

Shughuli hizi zinaongozwa na au kuhusisha wakimbizi wenyewe, maafisa wa serikali, jumuiya zinazowapokea na kuhifadhi wakimbizi, makampuni, watu mashuhuri, watoto wa shule na umma kwa ujumla, miongoni mwa wengine.