Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakazi wa Kaunti ya Ikotos wapigwa msasa jinsi ya kuandaa miradi itakayovutia ufadhili

Viongozi wa jamii na wadau wengine katika Kaunti ya Ikotos walijifunza zaidi kuhusu jinsi ya kujipanga na kupendekeza miradi midogo ambayo ina uwezekano mkubwa wa kupokea ufadhili.
UNMISS
Viongozi wa jamii na wadau wengine katika Kaunti ya Ikotos walijifunza zaidi kuhusu jinsi ya kujipanga na kupendekeza miradi midogo ambayo ina uwezekano mkubwa wa kupokea ufadhili.

Wakazi wa Kaunti ya Ikotos wapigwa msasa jinsi ya kuandaa miradi itakayovutia ufadhili

Ukuaji wa Kiuchumi

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) umeendesha mafunzo kwa wananchi wa kaunti ya Ikotosi iliyoko katika jimbo la Equatoria ya Mashariki ili kuwawezesha wananchi wa eneo hilo kunufaika na ufadhili wa miradi unayotolewa na shirika hilo, mashirika ya kitaifa na hata yale ya kimataifa. 

Taarifa ya UNMISS kutoka Equatorial Mashariki imeeleza kuwa warsha ya kutoa mafunzo hayo iliwaleta pamoja washiriki wapatao 55 wakiwemo viongozi wa jumuiya, viongozi wa mamlaka za mitaa na wawakilishi wa kiraia ambao walipatiwa mbinu bora za kuboresha maandiko yao kuhusu miradi ya ufadhili na kuelimishwa maeneo waliyokuwa wakikosea na kuwafanya kukosa ufadhili wa kifedha. 

Kumekuwa na ushindani mkali kwa fedha za miradi midogo midogo ya haraka inayofadhiliwa na UNMISS yenye malengo ya kuboresha hali ya maisha ya jamii za wenyeji. Wananchi wa Ikotos wamekuwa wakikosa ufadhili lakini baada ya mafunzo hayo sasa wanaamini wataweza kupata ufadhili. 

"Sasa tunaelewa vyema umuhimu wa kuwashirikisha wanawake katika kutambua na kutekeleza miradi ambayo inaweza kumnufaisha kila mtu, bila kutuacha sisi wanawake," anasema Alice Nabol, ambaye alirejea Sudan Kusini mwaka jana, baada ya kukaa kwa muda kwenye kambi ya wakimbizi katika nchi jirani ya Uganda.

 Bi. Nabol na wenzake waliohudhuria mafunzo hayo walijifunza kwamba mipango ambayo ni jumuishi ina uwezekano mkubwa wa kupokea rasilimali.

 Kwa upande wake, Chifu wa kijiji Paul Lomudang naye anasema "Tunahitaji kumiliki miradi yetu wenyewe na kushirikiana kwa karibu na UNMISS na washirika wengine. Tunaweza kusaidia kwa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mipango hii, kwa kutoa usalama, na kwa njia nyinginezo.”

 Watu wa Ikotos County wana changamoto ya kijiografia kutokana na umbali wao kutoka mji mkuu wa Torit. Umbali huo umefanya jamii hizi kukosa miundombinu ya kutosha ili kuwezesha upatikanaji wa huduma za msingi, na hivyo kufanya iwe vigumu kwa washirika wa maendeleo wa kitaifa na kimataifa kufanya kazi katika eneo hilo.

"Kuimarisha uwezo na ujuzi wa wadau wetu wa ndani katika kaunti ya Ikotos kutachangia pakubwa katika kuongeza nafasi zao za kupata fedha kwa ajili ya mipango ya maendeleo inayohitajika wakati tutakapoanza kupokea mapendekezo mapya ya mradi," ameeleza  afisa ujumuishi wa UNMISS Christine Fone.

 Baada ya warsha hiyo, Kamishna wa Kaunti Timon Loboi alijawa na furahana kueleza kuwa "hili limekuwa kifungua macho kwetu sote huko Ikotos. Sasa tunaelewa ni kwa nini mapendekezo yetu ya awali hayajafanikiwa na sasa yameandaliwa vyema zaidi tunaposonga mbele.”