Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Janga la Sudan kuwafungisha virago maelfu zaidi ya watu: Grandi

Wakimbizi wa Sudan wakiishi katika mahema katika mji wa mpakani na Chad wa Andre
© UNHCR/Ying Hu
Wakimbizi wa Sudan wakiishi katika mahema katika mji wa mpakani na Chad wa Andre

Janga la Sudan kuwafungisha virago maelfu zaidi ya watu: Grandi

Amani na Usalama

Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi duniani UNHCR, Filippo Grandi, ambaye leo amehitimisha ziara yake ya pili nchini Sudan tangu kuzuka kwa vita mwaka jana, ameonya kwamba bila juhudi za pamoja za kutafuta amani, watu wengi zaidi watalazimika kufangasha virago na kukimbia vita vya kikatili nchini Sudan na kuelekea nchi jirani.

Bwana Grandi akiwa nchini humo amepata fursa kutembelea kambi za wakimbizi na vituo vya wakimbizi huko Kosti, katika Jimbo la White Nile nchini humo ambako zaidi ya watu milioni moja wametafuta hifadhi tangu mapigano yalipoanza.

Alibainisha kuwa kiwango cha mateso kwa kweli hakiwezi kutambulika, akiongeza kuwa Sudan ndiyo tafsiri ya dhoruba kamili, ukatili wa kutisha wa ukiukwaji wa haki za binadamu, huku mamilioni ya watu wakifurushwa na vita hivi vya kiwendawazimu na vita vingine vilivyotangulia.

Bwana Grandi ameonya kuwa janga baya zaidi la njaa mbaya linakaribia, na mafuriko makubwa hivi karibuni yatazuia utoaji wa misaada zaidi. 

Mkuu huyo wa shirika la wakimbizi ameonyesha wasiwasi mkubwa juu ya ukubwa wa dharura ya kibinadamu nchini Sudan.

Kamishina Mkuu wa wakimbizi Filippo Grandi alipozuru kambi ya wakimbizi wa ndani ya Al-Salam mjini Kassala Sudan
© UNHCR/Omer Elnaiem
Kamishina Mkuu wa wakimbizi Filippo Grandi alipozuru kambi ya wakimbizi wa ndani ya Al-Salam mjini Kassala Sudan

Kusambaa kwa machafuko

Grandi amesema ghasia zimeongezeka huko El Fasher, Darfur Kaskazini, na ukatili umeripotiwa dhidi ya raia katika jimbo la Al Jazira.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi na washirika wake wameongeza juhudi za kukabiliana na hali ya kibinadamu katika jimbo la White Nile na maeneo mengine.

Tangu kuanza kwa mzozo huo, UNHCR imewafikia Wasudan wapatao 800,000 waliokimbia makazi yao kwa msaada wa ulinzi, huduma, misaada mingine, pesa taslimu, misaada muhimu na makazi ya dharura.