Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sheria za vita zinakiukwa Gaza, huku uchafuzi wa hewa ukilighubika eneo hilo: UN

Maeneo ya mji wa Khan Younis sasa karibu hayatambuliki baada ya zaidi ya miezi minane ya mashambulizi makali ya mabomu, maafisa wa Umoja wa Mataifa wanaripoti.
© UNICEF/Tess Ingram
Maeneo ya mji wa Khan Younis sasa karibu hayatambuliki baada ya zaidi ya miezi minane ya mashambulizi makali ya mabomu, maafisa wa Umoja wa Mataifa wanaripoti.

Sheria za vita zinakiukwa Gaza, huku uchafuzi wa hewa ukilighubika eneo hilo: UN

Amani na Usalama

Uchunguzi wa Umoja wa Mataifa kuhusu shambulio la bomu lililofanywa na jeshi la Israel huko Gaza umeashiria kuwa sheria za vita "zinakiukwa mara kwa mara kuhusiana na utumiaji wa mabomu yenye nguvu kubwa na madai ya ukosefu wa tofauti kati ya wapiganaji na raia”, amesema leo Kamishina Mkuu wa haki za binadamu Volker Türk

Ugunduzi huo unafuatia uchunguzi wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, kuhusu mashambulizi sita ambayo imeeleza kuwa kama "nembo ya mbinu za Israel katika vita vya zaidi ya miezi minane, vinavyohusisha tuhuma za utumiaji wa mabomu yenye uzito wa hadi pauni 2,000 au sawa na kilo 920. kwenye majengo ya makazi, shule, kambi za wakimbizi na masoko.”

Silaha hizi zenye ukubwa wa takriban futi 12 sawa na mita 3.4 pamoja na matoleo madogo zilitumwa kuanzia tarehe 9 Oktoba hadi 2 Desemba 2023 na kusababisha vifo 218 vilivyothibitishwa, imebainisha OHCHR na kuongeza kuwa idadi halisi ya waliofariki dunia huenda ilikuwa kubwa zaidi.

Volker Türk amesema "Sharti la kuchagua njia na mbinu za vita ambazo zinaepuka au angalau kupunguza kwa kila kiwango madhara ya kiraia linaonekana kukiukwa mara kwa mara katika kampeni ya Israel ya kuvurumisha mabomu,"

Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk
UN Geneva
Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk

Watu wanalengwa kwa elfu

Ripoti ya OHCHR imenukuu taarifa ya  vikosi vya ulinzi vya Israeli tarehe 11 Novemba 2023 kwamba Jeshi la anga "limepiga shabaha zaidi ya 5,000 kuondoa vitisho kwa wakati muafaka" tangu lilipoanza kulipua Gaza mwezi mmoja kabla. Kufikia wakati huo, mamlaka ya afya ya Gaza ilikuwa imeorodhesha kuuawa kwa Wapalestina 11,078, na wengine 2,700 walipotea na takriban 27,490 waliripotiwa kujeruhiwa.

Wakielezea kuhusushambulio dhidi ya kitongoji cha Ash Shuja katika Jiji la Gaza, waandishi wa ripoti hiyo walibaini kuwa muda wa uharibifu ulifikia takriban mita 130, na kuharibu majengo 15. 

Kiwango cha uharibifu wa majengo na volkano kilionyesha kuwa takriban mabomu tisa ya pauni 2,000 GBU-31 yalitumiwa, imsema ofisi ya OHCHR na kuongeza kuwa watu wasiopungua 60 waliripotiwa kuuawa.

Ripoti imedai kuwa "Chaguo la Israeli za mbinu na njia za kufanya uhasama huko Gaza tangu Oktoba 7, ikiwa ni pamoja na matumizi makubwa ya silaha za milipuko na athari za eneo kubwa katika maeneo yenye wakazi wengi, zimeshindwa kuhakikisha kuwa zinatofautisha kati ya raia na wapiganaji," 

Ripoti hiyo imesisitiza kuwa "Maisha ya raia na miundombinu inalindwa chini ya sheria ya kimataifa ya Kibinadamu (IHL). Sheria hii inaweka wazi wajibu wa pande zote kwenye migogoro ya kivita ambayo inafanya ulinzi wa raia kuwa kipaumbele."

Msichana mwenye umri wa miaka 11 ameketi kwenye vifusi vya nyumba huko Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.
© UNICEF/Eyad El Baba
Msichana mwenye umri wa miaka 11 ameketi kwenye vifusi vya nyumba huko Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Sauti zisizokoma za vita

Ajith Sunghay, Mkuu wa Ofisi ya OHCHR katika eneokaliwa la Palestina amesema “Wakati huo huo huko Gaza, hii leo watu ​​​​wanalazimishwa kusaka hifadhi huku kukiwa na sauti zisizokoma za vita na uhuharibifu usiofikirika.”

Akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya video kutoka Amman baada ya ya tathmini katika maeneo mengi katika eneo hilo, Bwana. Sunghay ameelezea jinsi watu wa Gaza wanavyoishi kwa shida baada ya kuhamishwa mara kwa mara na ghasia na maagizo ya jeshi la Israel ya kuondoka.

"Hospitali zimejaa na kufurika pomoni na harufu yake haivumiliki, maji taka yanamwagika kwenye mahema, hakuna maji safi. Ikiwa mabomu hayataua, magonjwa yatatokea," Bw. Sunghay amesema, baada ya kutembelea Khan Younis, Rafah na Deir. -Al-Balah.

Ameongeza kuwa "Sauti za mabomu, milioni ya bunduki, na ndege zisizo na rubani ni za mara kwa mara. Sauti ya vita haikomi mchana na usiku. Katika miaka yangu 22 ya kazi katika Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na katika hali nyingi za kuona na baada ya vita, sijawahi kushuhudia changamoto kama hizo za kufikisha misaada kwa Umoja wa Mataifa na washirika wa haki za binadamu na Uharibifu huo hauelezeki."

Mandhari ya Khan Younis sasa imebadilishwa, kabisa amesema afisa huyo wa OHCHR   akiongeza kuwa "Imejaa majengo yaliyoharibiwa kabisa na kwa kiasi. Watu niliokutana nao wamenieleza jinsi walivyohama mara 10 wamepona kwa shida."

Zaidi ya tani 330,000 za uchafu zimerundikana katika maeneo mbalimbali Gaza na kusababisha hatari za kimazingira na kiafya
© UNRWA
Zaidi ya tani 330,000 za uchafu zimerundikana katika maeneo mbalimbali Gaza na kusababisha hatari za kimazingira na kiafya

Tani milioni 39 za uchafu zimetotokana na mzozo wa Gaza: UNEP

Mbali ya kupotea kwa Maisha ya watu na hali mbayá ya kibinadamu Gaza inakabiliwa na janga lingine ambalo ni uchafu wa kila aina.

Zaidi ya tani milioni 39 za uchafu zimezalishwa na mzozo kati ya Israel na Hamas tangu Oktoba 7, 2023, kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira UNEP na kubainisha kuwa mgogoro wa mazingira katika eneo la Palestina bado ni uharibifu wa dhamana ya vita, na hatari mpya kwa afya ya binadamu na kukujikwamua kwa muda mrefu.

Ripoti ya UNEP inaangazia madhara makubwa ya kimazingira ya mzozo unaoendelea huko Gaza, ikisisitiza haja ya tathmini za haraka za kisayansi na mipango ya uokoaji ambayo ni suluhisho endelevu ili kukabiliana na uchafuzi wa maji, udhibiti wa taka na udhibiti wa uchafu hatari.

Kwa shirika hilo la Umoja wa Mataifa lenye makao yake makuu Nairobi Kenya, kiasi cha uchafu ni sawa na kilo 107 za kifusi kwa kila mita ya mraba. Hii ni zaidi ya mara tano ya uchafu uliotokana na mzozo wa 2017 huko Mosul, Iraq.

Lakini uchafu huo unahatarisha afya ya binadamu na mazingira, kutokana na vumbi na uchafuzi kutoka kwa vifaa visivyolipuka, asbesto, taka za viwandani na matibabu na vitu vingine vya hatari.

Uchafuzi wa hewa kutoka kwa viwanda unasababisha mabadiliko ya tabianchi.
© Unsplash/Ella Ivanescu
Uchafuzi wa hewa kutoka kwa viwanda unasababisha mabadiliko ya tabianchi.

Udongo na mifumo ya ikolojia iliyoathiriwa sana

Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP amesema: "Wakati maswali mengi yanasalia kuhusu aina na wingi wa uchafu unaoathiri mazingira huko Gaza, watu leo ​​tayari wanaishi na matokeo ya uharibifu wa mifumo ya usimamizi wa mazingira na uchafuzi wa mazingira." 

Athari za kimazingira za vita huko Gaza hazijawahi kushuhudiwa, inasema UNEP, zikiianika jamii katika ongezeko la uchafuzi wa udongo, maji na hewa na hatari za uharibifu usioweza kurekebishwa kwa mifumo ya ikolojia.

“Maji na usafi wa mazingira vimeporomoka. Miundombinu muhimu inaendelea kuharibiwa. Maeneo ya pwani, udongo na mifumo ya ikolojia imeathirika pakubwa. Yote haya yanadhuru sana afya ya watu, uhakika wa chakula na uthabiti wa Gaza,” ameongeza kusema Bi Andersen.

Kuchapishwa kwa utafiti huu mpya kunakuja wakati kwa miongo kadhaa, mazingira ya Gaza yamekabiliwa na uharibifu na shinikizo kwa mifumo yake ya ikolojia, kama matokeo ya migogoro ya mara kwa mara, ukuaji wa haraka wa miji, na msongamano mkubwa wa watu. hali ya kisiasa na mazingira magumu ya eneo hilo kutokana na mabadiliko ya tabianchi.