Elimu ya awali kwa watoto bado ‘kizungumkuti’ – UN
Elimu ya awali kwa watoto bado ‘kizungumkuti’ – UN
- Kuna uhaba wa sio tu walimu wa kufundisha bali pia wenye sifa na vigezo
- Ufadhili ni mdogo kupindukia kwenye elimu ya awali
- UNESCO inasema kuwekeza kwa watoto wadogo ni faida kubwa
Iwapo hali ya sasa ya elimu ya awali kwa watoto itaendelea kama ilivyo, ifikapo mwaka 2030 zaidi ya watoto milioni 300 hawatakuwa na uwezo wa kusoma hata kwa kiwango cha chini kabisa, imesema ripoti mpya iliyotolewa na mashiriak ya Umoja wa Mataifa lile la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO na la kuhudumia watoto, UNICEF.
Taarifa iliyochapishwa na UNESCO inasema ripoti hiyo ya kwanza kabisa kuhusu Huduma za awali za malezi na elimu kwa mtoto, ECCE inasema kiwango hicho cha watoto ni sawa na asilimia 37 ya watoto duniani kote na hivyo mashirika hayo yanapendekeza ni lazima hatua zichukuliwe haraka.
Katika ripoti hii inaelezwa bayana kwamba mawka 2022 mkutano wa Dunia kuhusu Elimu na Malezi ya Awali kwa Mtoto, ECCE nchi 155 ziliahidi kuhakikisha kila mtoto angalau anapata mwaka mmoja wa elimu ya bure ya awali, kabla ya kuingia elimu ya msingi, na vile vile ziliahidi kuhakikisha angalau asilimia 10 ya bajeti ya elimu kwenye elimu ya awali ambayo ni muhimu.
Kilichobainika na kinachotakiwa kupatiwa kipaumbele
Kufikia na kupata elimu ya awali inasalia kuwa ni changamoto kwani ripoti inasema hali ya sasa ni janga la kujifunza. Ili kufikia lengo dogo namba 4.2 la lengo namba 4 la Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs kuhusu elimu, ripoti inataka kuandikisha watoto milioni 1.4 kwenye elimu ya awali kila mwaka hadi 2030.
Suala la pili ni Uhaba wa sio tu walimu, bali pia wenye vigezo na sifa za kufundisha elimu ya awali. Ripoti inasema watoto wengi, hasa wale walio kwenye mazingira magumu, wanafundishwa na walimu wasio na sifa. Katika nchi za kipato cha chini, ni asilimia 57 tu ya walimu wa shule za msingi ndio wenye mafunzo yanayohitajika. “Tunahitaji zaidi ya walimu milioni 6 wa elimu ya awali ifikapo mwaka 20230.
Jambo la tatu ni ufadhili ambapo elimu hii ya awali haipatiwi ufadhili wa kutosha. “Tunahitaji nyongeza ya dola bilioni 21 kila mwaka ili kukidhi malengo ya elimu ya awali hadi mwaka 20230.”
Sasa serikali zifanye nini?
Kuna mapendekezo ya kina ya ni kwa jinsi gani serikali na jamii ya kimatifa zinapaswa kutatua janga hili la kujifunza kwa kujumuisha mfumo wa elimu ya awali na malezi ya awali ya watoto kwenye mfumo wa elimu unaosaidia watoto na familia zao.
Watoto wawe kitovu cha sera za serikali, ziongeze pia ufadhili kutoka vyanzo vya ndani na vya nje, na pia kupanua wigo wa haki ya elimu ili kuhakikisha kila mtoto ana msingi thabiti wa elimu.
Kauli ya Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa UNESCO
“Kuwekeza kwa watoto wetu wadogo kuna faida kubwa, iwe kijamii na kiuchumi. Ni uwekezaji bora zaidi ambao nchi inaweza kufanya. Gharama ya kutochukua hatua ni inaweza kuwa kubwa kama vile ambavyo kazi yetu imeonesha,” amesema Stefania Giannini, Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa U NESCO wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo.
Amesema kuna matumaini kwani idadi ya nchi zinazoripoti kuchukua hatua kuboresha elimu ya awali na malezi ya mtoto tangu mwaka 2022 imeongezeka kutoka asilimia 40 hadi 95.