Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Juhudi za Kimataifa Kukomesha Ukeketaji wa Wanawake huathiriwa na ukeketaji wakati wa likizo

Mama wa wasichana wawili kutoka Hadhramaut, Yemen, alipoteza mmoja wa binti zake kutokana na ukeketaji (FGM).
© UNFPA Yemen
Mama wa wasichana wawili kutoka Hadhramaut, Yemen, alipoteza mmoja wa binti zake kutokana na ukeketaji (FGM).

Juhudi za Kimataifa Kukomesha Ukeketaji wa Wanawake huathiriwa na ukeketaji wakati wa likizo

Haki za binadamu

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za kibinadamu (OHCHR) kupitia ripoti yake iliyochapishwa tarehe 14 mwezi Juni, imezionya familia kutoka mataifa mbalimbali hasa barani Ulaya na Amerika Kaskazini kutokuendelea na harakati za kuwavusha wasichana nje ya mipaka kwaajili ya kwenda kufanyiwa ukeketaji wakati wa likizo.

Inakadiriwa kuwa wasichana milioni 4.3 wapo walikuwa hatarini kukabiliwa na ukeketaji mwaka 2023. 

Utafiti huo uliohusisha taarifa zilisowasilishwa na nchi pamoja na asasi za kiraia umebainisha kuwa ingawa mataifa mengi yameongeza juhudi za kutokomeza ukeketaji lakini tabia hiyo inaendelea duniani kote kwa siri kwa kuwavusha mipaka wasichana kwenda kueafanyia ukeketaji kimataifa. 

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk akizungumzia ripoti hiyo amesema “ Ukeketaji ni sehemu ya mwendelezo wa ukatili wa kijinsia na hauna nafasi katika ulimwengu unaoheshimu haki za binadamu.

Ripoti hiyo imezitaka nchi kuhakikisha wanaweka njia za kuzuia vitendo hivyo na kutengeneza mazingira ya kuwasaidia wahanga wa vitendo vya ukeketaji kwa kushirikiana na asasi za kiraia, mashirika yasiyo ya kiserikali, jamii, bila kusahau viongozi wa dini na viongozi wengine ndani ya jamii. 

Nalo Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni (WHO) linataja zaidi ya wanawake 600,000 kutoka Muungano wa Ulaya wanadhaniwa kuishi na matokeo ya ukeketaji huku shirika hilo likieleza kuwa taratibu zote zinazohusisha kuondoa sehemu au viungo vya jinsia ya kike, au kusababisha madhara mengine kwenye viungo vya jinsia ya kike kwa sababu zisizo za kitiba ni uvunjifu wa haki za binadamu.

“kitendo hiki hakina faida kiafya kwa wasichana na wanawake na husababisha kutokwa damu kwa wingi, matatizo ya mkojo na maambukizi, pamoja na matatizo wakati wa kujifungua na hatari zaidi ya vifo vya watoto wachanga,” WHO.


Nini kifanyike?

Kutokana na ukeketaji kuwa na madhara kwa wanawake na wasichana, OHCHR imepenedkeza hatua mbalimbali kuchukuliwa ili kukabiliana na uendelevu wa jambo hili ikiwemo kutenga rasilimali za kutosha kwa ajili ya kuanzisha na kutekeleza mifumo ya sera za kikanda na makubaliano ya ushirikiano ili kukabiliana na janga hilo na kuwasaidia waathirika.

Pia, nchi zinahimizwa kuhakikisha kuwa hatua thabiti za kuzuia zinawekwa, zikiundwa kwa kushauriana na waathirika na mashirika husika ya kiraia kwa kushirikiana na jamii zilizoathirika, viongozi wa kidini na viongozi wa kimila.