Haiti: UN yapongeza kuundwa kwa serikali mpya, yasisitiza udharura wa usaidizi wa kiusalama
Haiti: UN yapongeza kuundwa kwa serikali mpya, yasisitiza udharura wa usaidizi wa kiusalama
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ameelezea kuunga kwake mkono kwa uthabiti serikali mpya iliyoundwa nchini Haiti, akisema ni hatua muhimu ya kwanza kuelekea kurejesha utawala wa kidemokrasia kwenye taifa hilo la Karibea lililogubikwa na mzozo na mapigano.
Jumanne wiki hii ya tarehe 11 mwezi Juni, Waziri Mkuu mpya wa Haiti, Garry Conille aliunda serikali mpya kwa kutangaza Baraza la Mawaziri, ikiwa ni wiki mbili tu baada ya Baraza la Mpito nchini humo kumteua kuwa Kaimu Waziri Mkuu kuchukua nafasi ya Ariel Henry.
“Amepongeza pia hatua ya wanawake kujumuishwa kwenye Baraza la Mawaziri, hatua ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya taifa hilo,” amesema Farhan Haq, Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa, akimnukuu Katibu Mkuu.
Guterres amepongeza wadau wa Haiti kwa juhudi zao kwenye mpito wa kisiasa nchini humo akiwasihi waendeleze kasi hiyo kuelekea kufanyika kwa uchaguzi, hatua ambayo ni muhimu sana katika kurejesha taasisi za kidemokrasia nchini humo.
"Hatua hiyo ya uongozi wa mpito wa kisiasa inapaswa kuambatana na hatua muhimu inayotakiwa ya uaslama,” amesema Katibu Mkuu akisisitiza umuhimu wa utulivu kwa ajili ya utawala endelevu.
Wito wa hatua za haraka za usalama
Guterres amesisitiza ombi lake la kupelekwa haraka kwa Kikosi cha Kimataifa cha Usaidizi wa Usalama, Haiti, MSS. Amesema kikosi hicho cha kimataifa ni muhimu katika kusaidia Polisi wa Kitaifa Haiti kudhibiti hali ya janga la usalama inayozidi kuzorota kila uchao, janga ambalo linazidi kudhihirika kupitia ghasia zinazofanywa na magenge ya uhalifu kwenye mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince.
Katibu Mkuu amesisitiza udharura pia usaidizi wa kifedha na vifaa kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ili kuhakikisha operesheni ya MSS inakuwa ya mafanikio.
"Kupelekwa haraka kwa kikosi hicho cha kimataifa na kuweko kwa usaidizi wa kutosha ni muhimu ili kutatua hali mbaya ya usalama,” amesema Katibu Mkuu.
Juhudi zinazoendelea za usaidizi
Licha ya changamoto za usalama, mashirika ya Umoja wa Mataifa ya usaidizi wa kiutu yameendelea kutoa misaada muhimu kwa wale waliokumbwa na ghasia na ukimbizi wa ndani.
Mathalani, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu misaada ya kiutu, OCHA, imeripotiwa kufikisha misaada ya kiutu siku za karibuni. Kuanzia Juni 8 hadi leo Juni 12, shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP limesambaza zaidi ya milo 40,000 ya moto kwa zaidi ya wakimbizi 9,000 wa ndani kwenye mji mkuu Port-au-Prince.
Huku mfumo wa huduma za afya ukizidi kudhoofika nchini Haiti, na ombi la mwaka huu kwa usaidizi kwa Haiti likiwa limefadhiliwa kwa asilimia 23 ya dola milioni 674 zinazohitajika, Katibu Mkuu ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kama njia mojawapo ya serikali mpya ya Haiti kuweza kufanya kazi kwa ufanisi kwa ajili ya maslahi na ustawi wa watu wake.