Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuna hatua zimepigwa katika miaka 10 ya uelimishaji kuhusu Ualbino lakini changamoto bado zipo: UN

Elizabeth Ayebare, (mwenye fulana ya manjano) akiwa darasani na wanafunzi wengine kwenye shule ambayo ilimkubali. (Maktaba)
OHCHR Video
Elizabeth Ayebare, (mwenye fulana ya manjano) akiwa darasani na wanafunzi wengine kwenye shule ambayo ilimkubali. (Maktaba)

Kuna hatua zimepigwa katika miaka 10 ya uelimishaji kuhusu Ualbino lakini changamoto bado zipo: UN

Haki za binadamu

Mtaalam Huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu kufurahia haki za binadamu kwa watu wenye ualbino, Muluka-Anne Miti-Drummond leo katika siku ya kimataifa ya kuelimisha kuhusu ualibino  amesema "Kwa muongo mmoja uliopita, tumepiga hatua kubwa katika kuangazia masuala ya haki za binadamu kwa watu wenye ualbino. Mafanikio haya yasingeweza kupatikana bila ushirikiano muhimu na ubia ulioundwa kati ya watu wenye ualbino na wadau ambao wamekuwa washirika muhimu katika juhudi hizi.” 

Akizungmza kutoka ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Geneva Uswisi, Muluka-Anne amepongeza maendeleo ya pamoja yaliyopatikana katika kufuatilia haki za binadamu kwa watu wenye ualbino, tangu Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipoitangaza rasmi tarehe 13 Juni kuwa Siku ya Kimataifa ya uelimishaji kuhusu Ualbino (IAAD) mwaka 2014.

Ni vyema kwamba mwaka huu tunaadhimisha kwa kaulimbiu ya Miaka 10 ya IAAD: Muongo wa Maendeleo ya Pamoja. Hatua muhimu zimepigwa katika kupambana na unyanyapaa, ubaguzi na ukatili unaowakumbwa na watu wenye ualbino.

Ushirikishwaji wa watu wenye Ualibino

Katika muongo uliopita, mtaalamu huyo anasema ushirikishwaji wa watu wenye ualbino katika mazungumzo na maamuzi ya haki za binadamu, pia ndani ya harakati za ulemavu, imekuwa ya kutia moyo kushuhudia. 

Hata hivyo, tunatambua pia kwamba safari ya kuelekea katika  ulimwengu wa haki sawa kwa watu wenye ualbino bado inakumbwa na changamoto na ugumu mkubwa.

Ameendelea kusema kuwa watu wenye ualbino bado ni miongoni mwa wale wanaoachwa nyuma zaidi linapokuja suala la ahadi za  maendeleo endelevu (SDG). 

Kwa hivyo, amesisitiza kuwa kuna haja kubwa ya kuimarisha ulinzi wao katika sheria na sera, pamoja na ushirikishwaji wao katika ukusanyaji wa takwimu, kampeni za uhamasishaji umma na uwakilishi katika nyanja zote za jamii. 

Juhudi hizi zote amesema zinachangia kutambua vyanzo na imani potofu ambazo zimekuwa miongoni mwa sababu kuu za ubaguzi na kutengwa dhidi ya watu wenye ualibino.

Muluka-Anne Miti-Drummond amesema “Tunahitaji kutumia mafanikio ambayo yamepatikana kufikia lakini pia kutambua kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya.”

Kuendelea kwa ukatili na unyanyapaa kwa wenye ualibino  inasikitisha

Tweet URL

Mtaalam huyo huru wa Umoja wa Mataifa amesema Ubaguzi na ukatili unaoendelea dhidi ya watu wenye ualbino katika sehemu mbalimbali za dunia bado ni jambo la kusikitisha. 

“Ninaendelea kupokea kesi za mashambulizi na mauaji, mara nyingi yakifanywa dhidi ya walio hatarini zaidi katika jamii zetu, watoto wetu.”

Kuhusu changamoto za kiafya, amesema ni vigumu sana kupata mafuta yaliyo na kinga ya jua kwa watu wengi wenye ualbino. Kuipata chupa ya mafuta haya yaliyo na kinga ya jua inayookoa maisha ni kama anasa ammbayo wengi hawawezi kuimdudu katika baadhi ya maeneo. Hii inaonyesha kiasi cha kazi inayohitajika katika jitihada zetu za kupunguza shida za watu wenye ualbino.

Kwa kutafakari  juu ya mafanikio ya miaka 10 iliyopita, amesema tunapaswa pia kufufua dhamira yetu ya kushughulikia changamoto zinazoathiri haki na ustawi wa watu wenye ualbino. Hii inahitaji mbinu mbalimbali zitakazo tuhusisha sisi sote kwa pamoja na ambazo zitahitaji uhamasishaji zaidi, elimu, utetezi, marekebisho ya sheria na sera, na ushirikishwaji wa jamii.

Katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Uelimishaji kuhusu Ualbino leo, tunasherehekea mnepo, nguvu, na michango iliyotolewa na watu wenye ualbino kwa jamii zetu, huku tukiendelea kujitahidi kwa ajili ya ulimwengu ambapo utu, usawa, na haki za binadamu zinatimizwa kikamilifu na kwa watu wote wenye ualbino."