Mwaka 2023 ulikuwa shubiri kwa watoto katika maeneo yenye mizozo ya silaha: UN Ripoti
Mwaka 2023 ulikuwa shubiri kwa watoto katika maeneo yenye mizozo ya silaha: UN Ripoti
Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo kuhusu viwango vya ukatili dhidi ya watoto Kwenye maeneo ya mizozo ya silaha inaonyesha kuwa mwaka 2023 kulikuwa na ukatili wa kupindikia.
Ripoti hiyo “Viwango vya kutosha vya ukatili kwa watoto Kwenye maeneo ya mizozo ya silaha 2023” inayotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kila mwaka inasema “Mwaka wa 2023, watoto wanaoishi katika mazingira ya migogoro walikumbana na ukatili katika viwango visivyoweza kuvumilika. Watoto wameandikishwa na kutumika vitani ikiwa ni pamoja na kwenye mstari wa mbele, kushambuliwa majumbani mwao, kutekwa nyara wakielekea shuleni, shule zao zilitumiwa kijeshi, madaktari wao wakilengwa, na orodha ya kutisha inaendelea.”
Ripoti imeongeza kuwa hali inayoendelea kubadilika, changamoto, kuongezeka kwa migogoro ya silaha, pamoja na matumizi ya silaha za milipuko katika maeneo yenye watu wengi, vimesababisha ongezeko la kushtua la ukiukwaji mkubwa wa haki dhidi ya watoto mwaka 2023.
Ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Watoto na Migogoro ya Silaha (CAAC), ambayo imejumuisha kwa mara ya kwanza taarifa kuhusu Haiti na Niger kati ya hali 25 the changamoto kubwa na mpangilio mmoja wa ufuatiliaji wa kikanda kwenye ajenda ya Watoto na Migogoro ya vita vya silaha , imefichua kuwa ukiukwaji mkubwa wa visa 32,990 ulithibitishwa dhidi ya watoto 22,557.
Watoto waliuawa, kubwakwa na kufanyiwa ukatili mwingine
Ripoti imebainisha kuwa kiwango hiki cha mateso ambacho hakijawahi kushuhudiwa kiliwakilishwa na ongezeko la ukiukaji mkubwa zaidi wa haki za watoto na kuendelea kwa kiwango cha juu katika ukiukaji mwingine mbaya mwaka 2023.
Watoto waliteseka kutokana na kutozingatiwa waziwazi kwa haki zao na ulinzi uliowekwa katika sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na haki ya kuishi huku watoto 11,649 wakiuawa na kulemazwa, likiwa ni ongezeko la asilimia 35 ikilinganishwa na ripoti ya mwaka jana na kuwakilisha ukiukwaji mkubwa zaidi uliothibitishwa katika ripoti.
Idadi ya watoto waliouawa mwaka 2023 ambao ni 5,301ni sawa na karibu watoto 15 wanaouawa kila siku.
Hii ilifuatiwa na ukatili wa kuajiri na kutumia watoto 8,655 vitani na kutekwa nyara kwa watoto 4,356.
Idadi kubwa zaidi ya ukiukaji mkubwa wa haki za watoto ilithibitishwa nchini Israel na eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Myanmar, Somalia, Nigeria na Sudan.
Makundi yenye silaha yalitekeleza asilimia 50 ya ukiukwaji huo
Kwa mujibu wa ripoti takriban asilimia 50 ya ukiukaji huo ulifanywa na makundi yenye silaha, ikiwa ni pamoja na yale yaliyoorodheshwa kama magaidi na Umoja wa Mataifa, ambapo mengine yalifanywa na vikosi vya serikali, na wahalifu wasiojulikana, kama vile mabomu ya kutegwa ardhini na vilipuzi vilivyoboreshwa.
Vikundi vilivyojihami ripoti inasema vilihusika hasa na utekaji nyara, uandikishaji na matumizi ya watoto vitani, na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto, wakati vikosi vya serikali vilikuwa wahusika wakuu wa mauaji na ulemavu, mashambulizi dhidi ya shule, hospitali na wafanyakazi wanaohusiana, na kunyimwa haki za kibinadamu kwa watoto.
Pia matumizi ya silaha za milipuko yaliendelea kuwa na athari mbaya, kuua na kulemaza watoto na kuzuia utoaji wa misaada ya kibinadamu.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa kulikuwa na matukio 5205 ya kunyimwa huduma za kibinadamu ikiwa ni ongezeko la asilimia 32 mwaka 2023 ikilinganishwa na 2022. Kutoripoti sana kutokana na unyanyapaa, hofu ya kulipizwa kisasi, kanuni hatari za kijamii, ukosefu wa huduma, ukwepaji wa sheria na masuala ya usalama, kesi za unyanyasaji wa kijinsia unaohusiana na migogoro dhidi ya watoto zilizfikia 1,470 ikiwa ni ongezeko la asilimia 25 ikilinganishwa na 2022.
Hatimaye, upatikanaji wa elimu na huduma za afya uliathiriwa kwa maelfu ya watoto, na mashambulizi 1,650 yalithibitishwa kwenye shule na hospitali na wafanyakazi kuhusiana.
Elimu na huduma za afya zilikuwa njiapanda
Hatimaye ripoti inasema, upatikanaji wa elimu na huduma za afya uliathiriwa kwa maelfu ya watoto, na mashambulizi 1,650 yalithibitishwa kwenye shule na hospitali na wafanyakazi kuhusiana..
Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu kwa ajiliya Watoto na Migogoro ya Kivita, Virginia Gamba amesema “Idadi kubwa ya watoto waliopitia ukiukwaji mkubwa wa haki zao mwaka 2023 kama inavyotanabaishwa katika Ripoti ya Mwaka ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Watoto na Migogoro ya silaha ni kengele ya ktuamsha. Tunawaangusha watoto. Ninatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kujitolea tena kwa makubaliano ya kimataifa ya kuwalinda watoto dhidi ya migogoro ya silaha na ninatoa wito kwa Mataifa kutimiza wajibu wao wa msingi wa kulinda watu wao na kuheshimu kanuni na viwango vyote vinavyotumika katika hali ya migogoro ya silaha. Umoja wa Mataifa upo tayari kusaidia pande zinazozozana katika kuandaa mpango wa utekelezaji wa pamoja wa kukomesha na kuzuia utumiaji na unyanyasaji wa watoto katika hali za vita."
Matumaini japo kidogo kwa watoto kwenye mizozo ya silaha
Licha ya kusambaa na kuongezeka kwa migogoro, ripoti inasema zaidi ya watoto 10,600 ambao hapo awali walihusishwa na vikosi vya kijeshi au vikundi vyenye silaha walipata msaada wa ulinzi au kuunganishwa tena na familia zao mwaka 2023.
Ripoti imesisitiza kuwa msaada wa watoto kuunganishwa tena na familia zao na jamii ni muhimu kwa ustawi wao binafsi na kwa malengo mapana ya uwiano wa kijamii, maendeleo ya kiuchumi na amani endelevu.
Katika kipindi chote cha mwaka 2023, ripoti imesema Umoja wa Mataifa ulianza au kuendeleza ushirikiano na pande zinazozozana kama ilivyokuwa katika hali ya CAAC ya Burkina Faso, Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, Colombia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Iraq, Israel na eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu , Mali, Msumbiji, Nigeria, Ufilipino, Somalia, Sudan Kusini, Jamhuri ya Syria, Ukraine na Yemen, ambazo baadhi zilisababisha kupitishwa kwa hatua zinazolenga kutoa ulinzi bora kwa watoto walioathiriwa na migogoro ya silaha.
Pande zote zikishirikiana watoto wananusurika
Ripoti hiyo ya mwaka 2023 imehitimisha kwa kusema kwamba ushirikiano ulipofanikiwa na hatua zikawekwa ikijumuisha kupitia saini ya mipango ya utekelezaji na itifaki za makabidhiano, mipango ya kujenga uwezo, ahadi za kila upande na mazungumzo ya wahusika, ukiukwaji ulipungua na watoto waliachiliwa kutoka kwenye migogoro.
Kupungua huko kama matokeo ya ushirikishwaji na mipango ya utekelezaji kulibainika nchini Iraq, Msumbiji, Ufilipino, Sudan Kusini, Ukraine na Yemen.
Bi. Gamba amesema “Narudia wito wangu kwa pande zote zinazopingana ili kushirikiana nami na Umoja wa Mataifa kwa msingi wa kutambua na kutekeleza hatua za kuwalinda watoto dhidi ya ukiukwaji mkubwa wa haki zao.”
Amemalizia kwa kusema “Ni wakati wa kufanya kazi kuelekea amani endelevu na ni wakati wa kuunda ulimwengu bora kwa watoto wetu. Hakuna mtoto anayepaswa kubeba mzigo wa vita vya silaha”.