Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Simulizi kutoka Sudan: Wapiganaji walitupokonya vitu vyetu 

Watoto wapumzika kwa kivulini katika kituo cha Tambasi huko El Fasher, Darfur Kaskazini.
© UNICEF/Mohamed Zakaria
Watoto wapumzika kwa kivulini katika kituo cha Tambasi huko El Fasher, Darfur Kaskazini.

Simulizi kutoka Sudan: Wapiganaji walitupokonya vitu vyetu 

Amani na Usalama

Nchi ya Sudan inakabiliwa na hatari inayoongezeka ya njaa inayosababishwa na migogoro ambayo itakuwa na matokeo mabaya ikiwa ni pamoja na watu kupoteza maisha, haswa kwa watoto wadogo. Hata pale wananchi wanapojaribu kukimbia vita ili kwenda kusaka msaada maeneo mengine wanakumbana na changamoto lukuki ikiwemo kuporwa mizigo yao na makundi ya wapiganaji. 

Kiujumla hali ni mbaya nchini Sudan kutokana na mapigano yanayoendelea baina ya makundi mawili ambayo ni vikosi vya kijeshi vya serikali na vikosi vya msaada wa haraka. Wananchi maisha yao yamebadilika kabisa maana sasa hawawezi kuendelea na shughuli zao za kawaida kama vile kilimo. 

Mmoja wa waathirika wa vita nchini Sudan ni Bi. Thuraya mwenye umri wa miaka 37 aliyekimbia eneo la El Fasher Kaskazini mwa Darfur na watoto wake kwenda kusaka hifadhi katika kambi ya wakimbizi ya Zamzam anasema maisha yamekuwa magumu hawana hata chakula cha kuwapikia watoto. “Tumekuja kutokea Tawila, tulilazimika kuondoka usiku, hatukuweza kuondoka mchana sababu tulikuwa tunaogopa mapigano na silaha nzito. Walitukagua na kututishia, mnaenda wapi? mmebeba nini kwenye mabegi yenu?. Walichukua vitu vyetu na kutuacha na vitu vichache, na hela kidogo tulizokuwa nazo tuliweza kufika katika kambi hii ya wakimbizi.”

Masikini Bi.Thuraya anatamani maisha yake kabla ya vita. “Kabla ya vita maisha yetu yalikuwa ya furaha, tulikuwa tunaenda shambani, hatukuwa tunanunua mkate wala chochote sokoni. Tulikuwa tukienda huko tunanunua nguo. Tulikula nyama kutoka kwenye mifugo yetu majumbani lakini wameiiba yote. Tulivyofika hapa kambini walitupa vitu vichache lakini vimeisha vyote. …… Ujumbe wangu kwa dunia ni watusaidie tupate amani. Hilo ndilo jambo letu Pekee.”

Uchambuzi wa hivi karibuni uliofanywa na Mashirika ya Umoja wa Mataifa, ikijumuisha lile la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Mpango wa Chakula (WFP) na la Afya Duniani (WHO) unaonesha kwamba uhasama unaoendelea unazidisha visababishi vya utapiamlo kwa watoto.