Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakati umewadia wa kusitisha uhasana na kuachilia mateka wote Gaza: Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres atoa hotuba nchini Jordan akitoa wito wa hatua ya dharura ya kushughulikia hali mbaya ya kibinadamu Gaza.
UN Photo/Mohammad Ali
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres atoa hotuba nchini Jordan akitoa wito wa hatua ya dharura ya kushughulikia hali mbaya ya kibinadamu Gaza.

Wakati umewadia wa kusitisha uhasana na kuachilia mateka wote Gaza: Guterres

Amani na Usalama

Usitishaji kamili wa mapigano huko Gaza unaohusishwa na kuachiliwa kwa mateka wote waliosalia hauwezi kuja haraka na wakati muafaka kama sasa amesema, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres hii leo, alipokuwa akikaribisha azimio la Baraza la Usalama lililopitishwa siku moja mapema kutaka kumalizika kwa vita huko Gaza.

Akizungumza nchini Jordan katika mkutano wa kimataifa uliochochewa na hali mbaya ya kibinadamu Gaza, Bwana Guterres amesisitiza kwamba baada ya zaidi ya miezi minane ya mapigano makali, "Jinamizi hilo la kutisha lazima likomeshwe. Ninakaribisha mpango wa amani ulioainishwa hivi karibuni na Rais Biden na kuzitaka pande zote kuchukua fursa hii na kufikia makubaliano," 

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameendelea akisema "Na ninatoa wito kwa pande zote kuheshimu majukumu yao chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu. Hii ni pamoja na kuwezesha uwasilishaji wa misaada ya kibinadamu kuingia na kusambazwa ndani ya Gaza, kama walivyojitolea wahudumu wa kibinadamu. Vivuko vyote vinavyopatikana vya kuingia Gaza lazima vifanye kazi na njia za nchi kavu ni muhimu sana."

Jana Jumatatu, mswada ulioandaliwa na Marekani umeitaka Hamas kukubali pendekezo la kusitisha mapigano lililotangazwa tarehe 31 Mei na Rais Joe Biden ambalo tayari limekubaliwa na Israel, kulingana na Ikulu ya Marekani.

Maandishi yanahimiza pande zote mbili kutekeleza kikamilifu masharti ya pendekezo "bila kuchelewa na bila masharti". 

Mswada huo wa azimio ulipitishwa kwa kura 14 za ndio na Urusi ilijizuia kupiga kura ikichagua kutotumia mamlaka yake ya kura ya turufu.

Kusimama na UNRWA

Akiangazia jukumu muhimu linalotekelezwa na shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA katika eneo hilo la Ukanda wa Gaza linalokaliwa kimabavu, shirika ambalo limeshambuliwa na kutengwa na viongozi wa Israel Katibu Mkuu amesisitiza kuwa uwepo wake utaendelea kuwa muhimu sana sio tu wakati wa vita, lakini baadaye.”

Ripoti za hivi karibuni kutoka Gaza zinaonyesha kuwa karibu asilimia 60 ya majengo yote ya makazi na angalau asilimia 80 ya vituo vya biashara vimeharibiwa na mashambulizi ya mabomu ya Israel, mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema, huku vituo vya afya na taasisi za elimu zikisambaratishwa na kusalia vifusi.

Mbali na hayo amesema, zaidi ya watoto milioni moja "walioathrika sana huko Gaza wanahitaji msaada wa kisaikolojia na usalama na matumaini ambayo shule zao zilikuwa zikitoa, 

Bwana Guterres amesisitiza kwamba "UNRWA pekee ndiyo yenye uwezo, ujuzi, na mitandao inayohitajika kusaidia. watu wa Palestina kukabiliana na changamoto kubwa ya afya, elimu na mengine mengi.”

Vikwazo vya upatikanaji wa misaada havielezeki

Akirejea onyo la mara kwa mara kutoka kwa wahudumu wa kibinadamu juu ya ukubwa wa dharura kubwa kote Gaza inayohusishwa na ukosefu wa upatikanaji wa misaada.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema "angalau nusu ya operesheni zote za misaada ya kibinadamu zimenyimwa fursa ya kuingia au , kuzuiwa, au kufutwa kutokana na uendeshaji au sababu za usalama”.

Huko Geneva, wakati huo huo, ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, imeonyesha mshtuko mkubwa juu ya athari ya operesheni ya kuwaachilia mateka katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat iliyofanyika Gaza mwishoni mwa wiki.

Msemaji wa OHCHR Jeremy Laurence amesema mamia ya Wapalestina, wengi wao wakiwa ni raia waliripotiwa kuuawa na kujeruhiwa na kwamba jinsi uvamizi huo ulivyofanywa "katika eneo lenye watu wengi inatia shaka endapo vikosi vya Israeli vinaheshimu kanuni za utofauti, uwiano na tahadhari, kama ilivyoainishwa chini ya sheria za vita.