Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Misaada ya kibinadamu isiyape kisogo mashirika ya wanawake Gaza na Ukingo wa Magharibi: UN Women

Wanawake wawili na mtoto wakiwa wameketi nje ya nyumba yao Gaza. Wazazi wengi hawawezi kukidhi mahitaji ya watoto wao ya kila siku kama chakula, maji, malazi ,afya na huduma zingine. (Maktaba)
WFP/Wissam Nassar
Wanawake wawili na mtoto wakiwa wameketi nje ya nyumba yao Gaza. Wazazi wengi hawawezi kukidhi mahitaji ya watoto wao ya kila siku kama chakula, maji, malazi ,afya na huduma zingine. (Maktaba)

Misaada ya kibinadamu isiyape kisogo mashirika ya wanawake Gaza na Ukingo wa Magharibi: UN Women

Wanawake

Mashirika yanayoongozwa na wanawake wa Palestina lazima yawekwe katika  mstari wa mbele Kwenye suala la misaada ya kibinadamu huko Gaza na Ukingo wa Magharibi limesema leo shirika la Umoja wa Mataifa linalohusikana mwasuala ya wanawake UN Women.

Katika tahadhari yake mpya ya masuala ya jinsia kuhusu vita dhidi ya Gaza iliyotolewa leo mjini New York na Cairo imefichua kuwepo kwa changamoto kubwa ambazo mashirika yanayoongozwa na wanawake wa Palestina yanakabiliana nayo, ikinaangazia dhamira yao isiyoyumba ya kuokoa maisha, na kutoa wito wa kuwekeza haraka na kuratibiwa kwa shughuli zao mashinani.

Tahadhari hiyo imeongeza kuwa asilimia 80 ya wanawake huko Gaza wanategemea msaada wa chakula ili kuishi, na mashirika yanayoongozwa na wanawake yana vifaa vya kipekee vya kuwasaidia yakifanya kazi katika baadhi ya maeneo hatari na yenye changamoto kubwa Gaza na Ukingo wa Magharibi.

Yako katika nafasi nzuri ya kusaidia

Taarifa hiyo ya UN Women imesema Ufikiaji wao mkubwa wa jamii unawafanya wawe na nafasi nzuri zaidi kufikia wanawake na wasichana wanaohitaji zaidi msaada. 

Katika kipindi cha miezi minane ya vita, UN Women imechapisha mfululizo wa tahadhari za kijinsia zikiandika jinsi maisha ya wanawake na wasichana yalivyozorota katika sekta mbalimbali kuanzia uhakika wa chakula hadi makazi, afya na usalama. 

Takwimu mpya za UN Women zilizokusanywa mwezi Aprili 2024, zinaonyesha kuendelea kuzorota kwa hali ya msingi ya maisha ya wanawake, huku zaidi ya asilimia 80 ya wanawake waliohojiwa huko Gaza wakiripoti kuwa tegemezi wa msaada wa chakula, na asilimia 83.5 wakiripoti kwamba msaada waliopokea hautoshi kukidhi mahitaji yao ya msingi ya familia.

Tahadhari hiyo ya UN Women imefafanua matokeo ya tathmini ya mashirika 25 ya Wapalestina yanayoongozwa na wanawake Gaza na Ukingo wa Magharibi. Na inaonyesha kuwa, pamoja na hali hii mbaya, mashirika haya yako mstari wa mbele katika kukabiliana na utoaji wa misaada ya kibinadamu. Kwa pamoja, mashirika haya 25 yanadumisha mtandao wa wafanyikazi 1,575 kote Gaza na Ukingo wa Magharibi. Tathmini hiyo inaonyesha kuwa asilimia 89 ya mashirika yaliyofanyiwa utafiti yamepata uharibifu wa ofisi zao, na asilimia 35 zikisambaratishwa kabisa.

Ofisi hizi hutumika kama vitovu vya uendeshaji, na ni muhimu kwa kuratibu na kutoa msaada.

Asilimia 60 ya mashirika hayo yameweza kufanyakazi

Katikati ya changamoto za sasa, UN Women imesema karibu asilimia 60 ya mashirika hayo yanaripoti kufanya kazi kwa uwezo kamili. 

Kujitolea kwa mashirika yanayoongozwa na wanawake kwa jumuiya zao ni dhahiri, huku asilimia 88 yakiwa yamejikita kwenye msaada wa dharura, yakitoa huduma muhimu kama vile usambazaji wa bidhaa zisizo za chakula asilimia 64 ya mashirika, bidhaa za chakula asilimia 56, usaidizi wa pesa taslimu asilimia 48 na huduma zinazohusiana na ulinzi, ikijumuisha msaada wa kisaikolojia na usimamizi wa kesi. 

Ingawa huduma zao ni muhimu na wanaendelea kubadilika na kurekebisha utendakazi wao, changamoto ya kifedha ni kubwa huku asilimia 56 ya mashirika hayo yanayoongozwa na wanawake yakiripoti kupungua kwa ufadhili na asilimia 88 yanakabiliwa na matatizo makubwa ya kifedha, ambayo yanatatiza uwezo wao wa kutoa huduma muhimu.

Sima Bahous Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women amesema "Kazi ya mashirika yanayoongozwa na wanawake huko Gaza na Ukingo wa Magharibi inahusu zaidi maisha ya wanawake na wasichana kama vile kudumisha matumaini, utu, na uwezekano wa maisha bora ya baadaye kwa wale wanaowahudumia. Kuwekeza katika mnepo wao sio muhimu tu ni ufunguo wa jawabu shirikishi ambalo haliachi mtu yeyote nyuma."