Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tushtue maono mapya kulinda baharí yetu tunayoitegemea - Guterres

Taka za plastiki baharini zimeathiri zaidi ya aina 600 ya viumbe vya bahari
Ocean Image Bank/Vincent Knee
Taka za plastiki baharini zimeathiri zaidi ya aina 600 ya viumbe vya bahari

Tushtue maono mapya kulinda baharí yetu tunayoitegemea - Guterres

Tabianchi na mazingira

Leo ni siku ya bahari duniani ujumbe ukiwa Shtua Maono Mapya ukilenga udharura wa kuimarisha kwa kina afya ya bahari kwani ina jukumu la kuendeleza na kuimarisha uhai duniani.

Katika ujumbe wake wa siku hii adhimu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema licha ya bahari kuwa na jukumu hilo, bado iko kwenye matatizo na kwamba “sisi binadamu ndio wa kulaumiwa.”

Mabadiliko ya tabianchi yanachochea ongezeko la kina cha maji ya bahari na kutishia uwepo wa nchi zinazoendelea za visiwa vidogo, halikadhalika jamii zinazoishi maeneo ya pwani.

Maji ya bahari yamekuwa na viwango vya juu vya joto vilivyovunja rekodi na kuchochea matukio ya hali ya hewa ya kupindukia yanayotishia kila mtu.

Guterres anaendelea kusema kuwa maji ya bahari yanazidi kuwa na tindikali na kuharibu matumbawe,  na kuharibu uhusiano muhimu wa upatikanaji wa chakula huku utalii wa bahari ukitishiwa halikadhalika mbinu za kujipitia vipato kwa jamii za maeneo ya pwani.

“Shughuli zisizo endelevu za kuendeleza maeneo ya pwani, uvuvi kupindukia, uchimbaji wa madini kwenye kina kirefu cha bahari, uchafuzi wa mazingira na utupaji wa taka za plastiki baharini vyote vinasababisha mvurugano wa mfumo anuai wa baharini duniani kote,” amesema Katibu Mkuu.

Taka za plastiki zinazokusanyika kwenye visiwa vya ndani zaidi baada ya kusombwa na mawimbi ya bahari kutoka pwani za maeneo ya bara.
Anant Shukla
Taka za plastiki zinazokusanyika kwenye visiwa vya ndani zaidi baada ya kusombwa na mawimbi ya bahari kutoka pwani za maeneo ya bara.

Lakini kuna nuru ya matumaini

Hata hivyo Katibu Mkuu anaona kuna nuru ya matumaini, akitaja makubaliano yaliyopitishwa mwaka jana na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa chini ya Mkataba wa Kimataifa wa Sheria ya Baharini kuhusu Uhifadhi na Matumizi Endelevu ya Maeneo ya Baharini yaliyo chini ya Mamlaka ya Kitaifa, akisema, ni  Mkataba mpya muhimu zaidi wa kuwahi kupitishwa katika miongo kadhaa kuhusu usimamizi wa bahari.”

Tumaini lingine ni mchakato unaoendelea wa kuandaa mkataba wenye nguvu kisheria wa kutokomeza uchafuzi utokanao na plastiki ambao ni fursa nyingine ya kusongesha lengo letu la pamoja la kulinda bahari yetu.

Ametaja pia tumaini lingine kuwa ni maoni ya hivi karibuni kwenye Mahakama ya Kimataifa kuhusu sheria za Bahari akisihi nchi zichukue hatua kupunguza, kudhibiti na kuzuia uchafuzi wa bahari unaotokana na utoaji wa hewa chafuzi.

Tushirikiane kulinda bahari zetu

Katibu Mkuu amesema mkutano wa mwaka huu wa viongozi kuhusu Zama zijazo na mkutano wa mwakani 2025 huko Ufaransa kuhusu Bahari ni fursa nyingine za kuahidi kurejesha na kulinda viumbe vya baharini na mifumo anuai ya pwani.

“Sas ani wakati wa serikali, wafanyabiashara, wawekezaji, wanasayansi na jamii kushirikiana kulinda bahari yetu,” amesema Guterres akitamatisha  “katika siku ya kimataifa ya bahari hebu na tuitikie wito wa ujumbe wa mwaka huu na tushtue maono mapya ya hatua kwa ajili ya bahari yetu.”