Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR inataka hatua za kina kwa mgogoro wa kibinadamu uliopuuzwa Sahel

Mji wa Dori ukanda wa Sahel nchini Burkina Faso lilikuwa linahifadhi wakimbizi wengi zaidi. (Maktaba)
© UNHCR/Sylvain Cherkaoui
Mji wa Dori ukanda wa Sahel nchini Burkina Faso lilikuwa linahifadhi wakimbizi wengi zaidi. (Maktaba)

UNHCR inataka hatua za kina kwa mgogoro wa kibinadamu uliopuuzwa Sahel

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR leo  limeelezea wasiwasi mkubwa kuhusu janga la kibinadamu lililopuuzwa na ambalo linaendelea kwa kasi katika eneo la Sahel.

Katika nchi za Sahel ya kati ambazo ni Burkina Faso, Mali na Niger UNHCR inasema , zaidi ya watu milioni 3.3 wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na migogoro inayoendelea, ikichochewa na athari mbaya za janga la mabadiliko ya tabianchi, kulingana na takwimu zilizotolewa mwezi Aprili 2024.

Alpha Seydi Ba, msemaji wa ofisi ya kanda ya UNHCR Afrika Magharibi na Kati amesema katika mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva kwamba "Idadi hii kubwa ya raia waliokimbia makazi yao inahitaji hatua za haraka za kimataifa ili kuzuia hali kuwa mbaya zaidi," 

Kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa UNHCR, hali ya usalama katika eneo la Sahel ya kati si shwari, na ni hali inayowalazimu watu kukimbia makazi yao kwenda kutafuta usalama na ulinzi wakati hatari za ulinzi zikienea kila kona.

Wakimbizi wa ndani ni milioni 2.8 nchini Burkina Faso, Mali na Niger

Takwimu za utafiti kutoka robo ya kwanza ya 2024 zinaonyesha kuwa jamii zilizofurushwa makwao na jamii zinazowapokea zinshuhudia wizi, mashambulizi dhidi ya raia na unyanyasaji wa kijinsia kama hatari kuu. 

Pia wanawake na watoto wako katika hatari kubwa ya kukatiliwa, kunyanyaswa na usafirishaji haramu wa binadamu.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa Wakati watu milioni 2.8 wamekuwa wakimbizi wa ndani nchini Burkina Faso, Mali na Niger katika kipindi cha miaka minne iliyopita, idadi ya wakimbizi kutoka nchi hizi tatu imeongezeka hadi 550,000 katika kipindi hicho.

Kwa mujibu wa UNHCR nchini Burkina Faso, tishio maradufu la vurugu na hali duni ya maisha huendeleza mzunguko wa hali tete. 

Na katika mwaka uliopita, uhamisho wa wakimbizi wa Burkina faso umekuwa muhimu, na zaidi ya watu 117,000 walifika katika nchi jirani za pwani, kulingana na orodha iliyochukuliwa Aprili 2024.

Shirika hilo la wakimbizi duniani limesema hivi sasa kuna zaidi ya wakimbizi 200,000 wa Mali nchini Mauritania, 130,000 nchini Niger na karibu 40,000 nchini Burkina Faso, pamoja na 50,000 ambao wamekimbilia Algeria lakini hawana njia za kupata hifadhi.

Wakati huo huo, Mali inawahifadhi karibu wakimbizi 94,000, hasa kutoka Burkina Faso, Niger na Mauritania, huku wakikabiliwa na wakimbizi wa ndani zaidi ya 354,000.

Mtazamo wa pamoja kati ya wadau wa kibinadamu, maendeleo na amani

Kulingana na UNHCR, ongezeko la kuvuka mpaka linaonyesha hali mbaya zaidi na haja ya kukabiliana na mahitaji ya Sahel kwa kuwekeza katika ulinzi, usaidizi na ufumbuzi wa kudumu. Juhudi kubwa zinafanywa, lakini bado kuna mengi ya kufanywa.

UNHCR inaishauri jumuiya ya kimataifa kudumisha misaada wakati wa machafuko ya kisiasa katika eneo la Sahel ili kuepuka kuzidisha matatizo yaliyopo na kuongeza uwezekano wa migogoro ya siku zijazo. 

Inatoa wito wa uwekezaji katika mifumo muhimu ya kijamii na ulinzi, pamoja na kusaidia jamii kabla ya kulazimishwa kuhama.

Pia inasema ni kuhusu kuzingatia mbinu ya pamoja kati ya wadau wa misaada ya kibinadamu, maendeleo na amani, huku ikielekeza fedha kwa mashirika ya ndani yanayofanya kazi kwa bidii mashinani, kwa ajili ya hatua za ufanisi zaidi kwa mahitaji.

UNHCR inahitaji zaidi ya dola milioni 443 kugharamia mahitaji ya dharura ya kibinadamu nchini Burkina Faso, Mali, Niger, Mauritania na nchi za Ghuba ya Guinea.