OCHA: Hali ya ustawi na usalama bado ni tete kwa raia nchini Sudan
OCHA: Hali ya ustawi na usalama bado ni tete kwa raia nchini Sudan
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura OCHA hii leo imetoa taarifa mpya kuhusu hali ya vita huko nchini Sudan amabapo imeeleza kuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu ustawi na usalama wa raia wanaokabiliwa na mapigano makali yanayoendelea katika eneo la Al Fasher, lililoko katika mji mkuu wa Jimbo la Darfur Kaskazini mwa Sudan.
OCHA wameripoti kuwa takriban watu 130,000 wamekimbia makazi yao kutokana na ghasia hizo ndani na karibu na eneo la Al Fasher katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.
Wakati huo huo shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya watoto UNICEF nalo limeonya kuwa mapigano ya silaha kwa ajili ya kudhibiti bwawa la maji la Golo - lililoko magharibi mwa mji huo lipo hatarini kukata kutoa huduma ya maji salama na ya kutosha kwa watu wapatao 270,000 katika eneo la Al Fasher na maeneo jirani.
UNICEF imetoa wito kwa pande zote kutii wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu na kukomesha mashambulizi yote dhidi au karibu na miundombinu muhimu ya kiraia, ikiwa ni pamoja na mifumo ya maji na vifaa, hospitali, vituo vya afya na shule.
Taarifa za mashirika hayo mawili zinatolewa wakati huu ambapo uchambuzi wa washirika yanyaohusika na lishe unaonesha hali kuwa mbaya na ya kutisha kwa watoto na akina mama kote nchini Sudan. Hadi kufikia mwezi Machi 2024, inakadiriwa watoto milioni 3.7 walio chini ya umri wa miaka mitano, pamoja na wanawake wajawazito na wanaonyonyesha milioni 1.2, wana utapiamlo.
Mpango wa Mwitikio wa Kibinadamu wa 2024 kwa Sudan unaendelea kukabiliwa na ufadhili mdogo sana. Kati ya dola bilioni 2.7 zinazohitajika, ni asilimia 16 tu ambazo ni sawa na takriban dola milioni 430 zimepokelewa hadi sasa. Licha ya mapungufu ya ufadhili na changamoto zingine ikiwa ni pamoja na mapigano, ukosefu wa usalama, uporaji na vikwazo vya ufikiaji wadau wa masuala ya haki za binadamu wanajitahidi kufikia watu wenye uhitaji kote nchini Sudan.