Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jinsi Afrika Inavyoweza Kutumia Utajiri wa Madini Muhimu ili Kufufua Uchumi- UNCTAD

Mwanamume mmoja akifanya kazi katika mgodi huko DR Congo.
© UNDP
Mwanamume mmoja akifanya kazi katika mgodi huko DR Congo.

Jinsi Afrika Inavyoweza Kutumia Utajiri wa Madini Muhimu ili Kufufua Uchumi- UNCTAD

Ukuaji wa Kiuchumi

Utajiri wa madini wa Afrika haupingiki. Kuanzia kwenye migodi ya kobalti ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC hadi maeneo ya madini ya manganizi a Afrika Kusini, bara hili lina hazina ya madini muhimu kwa ajili ya mabadiliko ya kimataifa kuelekea nishati salama yenye kiwango kidogo cha hewa ya kaboni na maendeleo ya kiteknolojia.

Hiyo ni kauli ya Paul Akiwumi, Mkurugenzi wa Masuala ya Afrika na nchi zenye Maendeleo Duni, LDCs kwenye Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo ya Biashara na Maendeleo, UNCTAD, kwenye makala iliyochapishwa kwenye wavuti wa UNCTAD.

Bwana Akiwumi anasema bara la Afrika ni kivutio kikuu kutokana na akiba yake kubwa ya madini yanayohitajika kwa teknolojia za nishati mbadala kama vile paneli za jua na magari ya umeme: Bara hilo lina hifadhi ya 55% ya kobalti, 47.65% ya manganizei na 5.9% ya shaba, miongoni mwa mengine. 

Kadri janga la tabianchi linavyozidi kuongezeka, mahitaji duniani ya madini haya muhimu katika mabadiliko ya nishati yanaweza kuongezeka karibu mara nne kufikia 2030. Mahitaji haya yanayoongezeka yanawasilisha fursa ya kipekee kwa Afrika kuyatumia vizuri ili kuzalisha mapato zaidi na kuweka njia mpya kuelekea ustawi, ukuaji jumuishi na maendeleo endelevu. 

“Afrika sasa ina fursa ya kihistoria ya kuliwasilisha wimbi hili  la mabadiliko ya kimuundo katika baadhi ya nchi zinazohitaji sana. Makadirio yanaonesha kuwa nchi za Afrika zinazalisha karibu asilimia 40 tu ya mapato ambayo inaweza kukusanya kutokana na rasilimali hizi, kwani zinakwamishwa na ukosefu wa kuongeza   thamani kwa bidhaa, changamoto za utawala na miundombinu, miongoni mwa vikwazo vingine.” Imesema makala hiyo. 

Ni wakati wa kubadilisha mwelekeo

Fedha za misaada ya maendeleo zilizopunguzwa na zisizo na uhakika wa kupatikana zinakwamisha maendeleo ya Afrika, na kupunguza kasi ya maendeleo kuelekea kufikia malengo ya maendeleo endelevu, SDGs. Lakini katikati ya migogoro mingi iliyopo kwa sasa, nafasi finyu ya kifedha, ukuaji wa polepole na deni kubwa, ni wakati muafaka kwa nchi za Afrika kubadilisha hali kwa kutumia fursa inayotolewa na ongezeko la madini muhimu. 

Ili kufanya hivyo, mataifa ya Afrika yanapaswa yatumie mbinu ya kijumla ambayo haijumuishi tu uchimbaji na usafirishaji wa madini ghafi bali pia kuongeza thamani ndani ya nchi kupitia usindikaji na utengenezaji ili kupata sehemu kubwa ya soko la kimataifa. 

Usindikaji huo pia utasaidia kubadilisha aina ya bidhaa zinazosafishwa nje ya hizi na kuzifanya zisiathiriwe na kupanda na kushuka kwa bei za bidhaa. 

Nchi za Afrika pia zinapaswa kuunganisha kikamilifu sekta zao za madini katika shughuli za kiuchumi za kitaifa kwa kukuza uhusiano na sekta zingine za uchumi wao. 

Hili lazima liambatane na utekelezaji wa dira ya madini ya Afrika inayojumuisha ushirikiano wenye nguvu kwenye kanda na uwekezaji zaidi katika miundombinu na mtaji wa kibinadamu. 

Bwana AKiwumi anasema Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika, AfCFTA linatoa jukwaa la ushirikiano wa kiuchumi wa kina, hivyo kuunda mazingira wezeshi kwa nchi kushirikiana kwa rasilimali na utaalamu, kushinda changamoto za miundombinu, kuongeza upatikanaji wa masoko na kukuza uhamishaji wa teknolojia.

Nchi za Afrika pia zinapaswa kuepuka mitego ya awali ya utegemezi wa bidhaa na kuupa kipaumbele usimamizi endelevu wa rasilimali unaopunguza uharibifu wa mazingira na kuheshimu haki za jamii za wenyeji. 

Ni muhimu pia kwa nchi kuongeza uwezo wao wa uzalishaji, kwani bila kuhamia kwenye sekta za uzalishaji wa juu, hawataweza kufikia malengo yao ya maendeleo. 

Marekebisho ya uongozi ni muhimu

Marekebisho kwa ajili ya usimamizi bora wa kifedha, halikadhalika utawala bora ni muhimu kwa sekta za uchimbaji wa madini wenye uwajibikaji yanapaswa kuwa kipaumbele, ili kuhakikisha kwamba uchimbaji wa madini unachangia badala ya kudhoofisha malengo ya maendeleo endelevu ya muda mrefu. 

Kukuza uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za madini, kuondoa rushwa na kupambana na mtiririko haramu wa fedha ni hatua muhimu pia za kuhakikisha kwamba faida za uchimbaji madini zinagawanywa kwa usawa kati ya raia wote. 

Bara linapaswa pia kutumia hazina zake kubwa za madini muhimu kuchora njia yake mwenyewe ya mabadiliko ya nishati safi, inayojikita katika malengo yake ya viwanda, huku likijidhihirisha kama mchezaji muhimu katika hatua za kimataifa za mabadiliko ya tabianchi. 

Mabadiliko kuelekea nishati safi ni muhimu kwa Afrika, eneo linalowakilisha asilimia 80 ya watu milioni 733 duniani wasio na upatikanaji wa umeme na asilimia 39 ya watu bilioni 2.4 wasio na upatikanaji wa nishati safi ya kupikia. 

Mkazo wa kimkakati

Afisa huyo wa UNCTAD anatamatisha akisema, mwaka huu tunasherehekea maadhimisho yetu ya miaka 60 kwa kutafakari masomo tuliyojifunza kwa miaka mingi na kuunda njia mpya itakayoongeza msaada wetu kwa nchi mbali mbali kujenga mustakabali ambao ni imara, wa haki na endelevu. 

Tukio hili litachunguza fursa ambazo bado hazijatumika katika sekta ya madini "safi" na kubuni njia kuelekea ongezeko la uongezaji wa thamani na uboreshaji wa mapato ili kuleta enzi mpya ya maendeleo katika bara hili.