Athari kali ya vita yawabana raia huko El Fasher, aonya afisa wa Umoja wa Mataifa
Athari kali ya vita yawabana raia huko El Fasher, aonya afisa wa Umoja wa Mataifa
Afisa wa ngazi ya juu wa misaada wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan siku ya Alhamisi alionya kwamba athari kali ya vita imewabana raia huko El Fasher, akielezea kusikitishwa kwake na hali mbaya ya kibinadamu iliyo katika eneo hilo.
Mapigano kati ya jeshi la Sudan na jeshi pinzani la Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), ambao wamekuwa wakipigana kwa zaidi ya mwaka, hivi karibuni yalizidi katika mji wa Kaskazini wa Darfur.
Katika taarifa yake, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa wa Misaada ya Kibinadamu nchini Sudan Clementine Nkweta-Salami alisema kuwa raia wanashambuliwa kutoka pande zote na habari za vifo zinavyoripotiwa huku ukiukwaji wa haki za binadamu ukiwa wa kutisha.
Taarifa zinazotia wasiwasi mkubwa
"Familia, ikiwa ni pamoja na watoto na wazee, wanazuiwa kutoka nje ya jiji wanapotafuta usalama," anasema Bi Nkweta-Salami.
"Tunapokea ripoti za kutisha sana kwamba vituo vya matibabu, kambi za watu waliohama makazi yao na miundombinu muhimu ya kiraia imekuwa ikilengwa na wahusika kwenye mzozo."
Bi. Nkweta-Salami aliongeza kuwa maeneo mengi ya El Fasher yameachwa bila umeme wala maji na idadi inayoongezeka ya watu ina upungufu wa upatikanaji wa chakula, huduma za afya na mahitaji mengine muhimu Pamoja na huduma muhimu.
Wito kwa pande husika
"Baada ya zaidi ya mwaka mmoja wa vita vya kikatili, familia zimemaliza rasilimali zao adimu na ustahimilivu wao unapungua kwa kila siku ya vurugu," anasema.
Afisa huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kutoa misaada nchini humo alisisitiza kuwa pande zote lazima ziepuke kutumia silaha za milipuko katika maeneo yenye watu wengi na kuchukua tahadhari zote zinazowezekana kulinda raia na miundombinu ya kiraia.
"Vita vina sheria ambazo lazima ziheshimiwe na wote, licha ya chochote," anasema.
Migogoro huhamisha mamilioni ya watu
Wakati huo huo, vita hivyo vimehamisha zaidi ya watu milioni saba ndani ya Sudan, zaidi ya nusu yao wakiwa watoto, kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya kibinadamu, OCHA, ikinukuu data kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji ( IOM ).
Hii ni pamoja na makadirio ya watu milioni mbili ambao wamekimbilia nchi jirani tangu mgogoro huo ulipozuka Aprili 2023.
Umoja wa Mataifa na washirika wanaendelea kuongeza juhudi za kukabiliana na ongezeko la njaa na uhaba wa chakula nchini Sudan. Baadhi ya watu milioni 18 kote nchini wanakabiliwa na njaa na milioni tano wako ukingoni mwa njaa.
Chakula kusafirishwa
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) liliripoti kwamba tani 1,200 za bidhaa za chakula kwa ajili ya watu takriban 116,000 zinasafirishwa katika eneo la Darfur na zinaelekea maeneo ya mwisho huko Darfur ya Kati na maeneo 12 kote Darfur Kusini, ikiwa ni pamoja na kambi za wakimbizi huko Nyala.
Bidhaa hizo ni za msafara wa WFP uliovuka hadi Sudan kutoka Chad wiki iliyopita.
Ugawaji wa chakula pia unaendelea kwa watu 135,000 katika jimbo la Kordofan Kusini huku WFP ikikariri kuwa msaada lazima ufikie jamii zilizo hatarini kwa usalama.
Utapiamlo
Nayo mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa leo yametoa onyo kali kwamba dalili zote zinaonesha kuzorota kwa kiasi kikubwa kwa hali ya lishe kwa watoto na wanawake katika nchi ya Sudan inayokumbwa na vita. Uchambuzi wa hivi karibuni uliofanywa na Mashirika hayo matatu la Kuhudumia Watoto (UNICEF), la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na la afya ulimwenguni (WHO) unaonesha kwamba uhasama unaoendelea unazidisha visababishi vya utapiamlo kwa watoto. Mashirika hayo yamesema hatua za haraka zinahitajika kulinda kizazi kizima dhidi ya utapiamlo, magonjwa na vifo.