Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uvamizi wa Israel ukiendelea Ukanda wa Gaza, vituo vya misaada vinafunga kimoja baada ya kingine: UN

Wakimbizi wa Kipalestina wanaishi katika kambi ya muda ya mahema ufukweni katika eneo la Mawasi, magharibi mwa Rafah, Gaza.
UN News/Ziad Taleb Hali katika kambi ya Al Mawasi kusini-magharibi mwa Gaza bado ni mbaya zaidi na haifai mamia ya maelfu ya watu wa Gaza walioondolewa na kuongezeka kufuatia ghasia karibu na Rafah na mahali pengine katika Ukanda wa Gaza.

Uvamizi wa Israel ukiendelea Ukanda wa Gaza, vituo vya misaada vinafunga kimoja baada ya kingine: UN

Amani na Usalama

Bila dalili ya yaliyoripotiwa mapigano mitaani na mashambulizi ya Israel Gaza leo, wahudumu wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wameonya kwamba mtiririko wa msaada muhimu wa kuokoa maisha katika eneo hilo umepungua kwa zaidi ya theluthi mbili tangu jeshi la Israel liongeze operesheni yake huko Rafah na kunyakua ufunguo huo wa mtiririko wa misaada.

"Vituo vya misaada ya kibinadamu huko Rafah vinalazimika kufungwa kimoja baada ya kiingine . Mtiririko wa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza, ambayo tayari haitoshi kukidhi mahitaji yanayoongezeka, umepungua kwa asilimia 67 tangu Mei 7," imeripoti ofisi ya uratibu wa misaada ya kibinadamu na masuala ya dhariura ya Umoja wa Mataifa, OCHA huku kukiwa na ripoti kwamba majiko, zahanati na hospitali zimefungwa.

Hadi wakati wanajeshi wa Israel walipokamata na kukifunga kivuko cha mpaka cha Rafah kilichoko kusini kabisa mwa Ukanda huo, ndicho kilikuwa kitovu cha kuingilia Gaza kwa chakula, maji, mafuta na dawa pamoja na njia ya wagonjwa na waliojeruhiwa kuondoka kwa ajili ya matibabu.

Hakuna uwezo wa kusaidia dhidi ya tishio la njaa

Likirejea wasiwasi huo, Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa Duniani WFP limeonya kuwa kuna mambo machache ambayo shirika "Linaweza kufanya hivi sasa huko Rafah, huku akiba ya hifadhi ni ndogo sana na uwezo wa kutoka sehemu moja kwenda nyingine umepunguzwa sana".

Kulingana na WFP, kivuko cha Erez Magharibi kaskazini mwa Gaza "kinafanya kazi, lakini si cha kutegemewa". 

Lango 96 kusini zaidi na kivuko cha Erez pia hakuwezi kufikiwa na ufikiaji umezuiliwa kuelekea sehemu za kusini za Gaza kwamba unahatarisha kusababisha viwango vya njaa sawa na vinavyoshuhudiwa kaskazini.

Mbinu muhimu

Hatua hiyo inakuja wakati jeshi la Israel lilisema kuwa limepata "udhibiti wa kimkakati wa eneo jembamba la kilomita 13 sawa na maili nane kati ya Gaza na Misri.

Katika taarifa yake  jana Jumatano, msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel aliripotiwa kudai kwamba warusha maroketi walitumiwa kushambulia Israeli kutoka Ukanda wa Philadelphi.

Afisa mkuu wa Israel pia aliripotiwa kuiambia redio ya taifa Jumatano kwamba mapigano huko Gaza yanaweza kutarajiwa kudumu hadi angalau mwisho wa mwaka.

Hali mbaya ya kibinadamu

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa baada ya karibu miezi minane ya vita, wakazi wote wa Gaza wa watu milioni 2.2 wanategemea tu misaada ya kibinadamu, ikiwa ni pamoja na chakula.

Ingawa vifaa vinavyohitajika sana vimewasilishwa kwa upande wa Wapalestina wa kivuko cha Kerem Abu Salem, au Kerem Shalom, kilicho karibu na Rafah, wahudumu wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wamesisitiza mara kwa mara kwamba si salama kuwaleta huku kukiwa na uhasama unaoendelea, barabara zisizopitika, silaha zisizolipuka, uhaba wa mafuta na ucheleweshaji katika vituo vya ukaguzi.

"Watu wazima na watoto wamechoka sana kutokana na kuhama mara kwa mara, njaa, na hofu," limesema shirika la WFP ilisema katika tarifa yake ya hivi karibuni. 

Limeongeza kuwa "Wanatamani sana vita viishe, kama wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu chini, ambao kwa kiasi kikubwa wamehamishwa na kutawanywa pamoja na watu wanaotakiwa kuwahudumia."

Maafisa wa misaada mara kwa mara wamesisitiza wajibu wa Israel kama mamlaka inayokalia kuhakikisha kwamba misaada inawafikia wanaoihitaji, kwa kuzingatia sheria za kimataifa za kibinadamu.

Wakati huo huo shirika la Umoja wa Mataifa la chakula limethibitisha kuwa misaada ya kuokoa maisha na mafuta kutoka Misri imevuka hadi Gaza kupitia kivuko cha Kerem Shalom.

"Hii ni hatua muhimu, lakini tunahitaji ufikiaji endelevu. Tunahitaji vivuko vyote vya mpaka na vivuko ndani ya Gaza viwe wazi," lilisema, na kuongeza kuwa ingawa baadhi ya bidhaa za kibiashara zimefika kwenye eneo hilo, "watu hawawezi kumudu bei ya juu. Tunahitaji msaada zaidi kuingia kusini kwa sababu watu wanahitaji utofauti wa lishe, upatikanaji wa huduma za afya na maji."

Katika tarifa yake ya hivi karibuni, shirika la chakula la Umoja wa Mataifa lilisema kuwa kaskazini, timu za misaada zinasambaza vifurushi vya chakula, unga wa ngano, milo moto na kusaidia uokaji wa mikate.

Katika maeneo ya kati, WFP inatanguliza chakula cha moto ili kuwafikia watu wengi walio na rasilimali chache. 

Shirika hilo limebainisha kuwa usaidizi wa haraka sasa unawezekana kutokana na zana iliyoanzishwa hivi karibuni ya kujiandikisha ambayo inaruhusu watu kusalia katika eneo lao.

Viwanda vinne tu vya kuoka mikate sasa vinafanya kazi katika Jiji la Gaza, na kimoja kilifunguliwa hivi karibuni huko Jabalia, kikitoa mkate kaskazini. 

Kati ya viwanda 17 vya kuoka mikate vya WFP vinavyofanya kazi huko Gaza, ni 11 pekee vinavyofanya kazi sasa kutokana na ukosefu wa mafuta na vitu vingine muhimu.

Huko Rafah hali ya huduma ya afya bado ni hatari, na hospitali moja tu ndio bado inafanya kazi, Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Ulimwenguni WHO limesema, likirejelea hospitali ya wazazi ya Al Emirati. 

Hii inalinganishwa na hospitali tatu ambazo hazifanyi kazi tangu mapema mwezi huu. "Hospitali ya Najjar ilihamishwa tarehe 7 Mei na Hospitali ya Al Kuwaiti huko Rafah iliacha kufanya kazi mnamo Mei 27," WHO imesema, kufuatia ripoti zilizomnukuu mkurugenzi wa hospitali hiyo kwamba hii ilitokea baada ya wafanyikazi wawili wa matibabu kuuawa wakati lango la hospitali hiyo lilipogongwa na kombora.

Operesheni zingine za msaada ambazo zimefungwa wiki hii huko Rafah zimeripotiwa kuwa ni pamoja na hospitali ya shamba na ya World Central Kitchen  inayoendeshwa na washirika wa Umoja wa Mataifa Hilali Nyekundu ya Palestina na World Central Kitchen.