Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Operesheni za kibinadamu Gaza zinakaribia kusambaratika: WFP

Mtoto akiwa ameshika ndoo kwenye mstari wa usambazaji wa chakula WFP huko Khan Younis, Gaza.
© WFP/Ali Jadallah Mtoto akipokea chakula katika jiko linaloungwa mkono na WFP huko Khan Younis, Gaza.

Operesheni za kibinadamu Gaza zinakaribia kusambaratika: WFP

Amani na Usalama

Wakati maelfu ya familia zikiendelea kukimbia Rafah, zikijikuta na maji ya kunywa na chakula kidogo, operesheni za kibinadamu huko Gaza zinakaribia kuporomoka, limesema leo Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP likibainisha kuwa eneo la Palestina linahitaji haraka mtiririko mkubwa wa misaada ili kukabiliana na hali hiyo. 

Shirika la WFP linaonya kwamba mashambulizi ya Israel kaskazini na kusini mwa Ukanda wa Gaza, pamoja na kufungwa kwa vivuko vya mpakani, "vitasababisha maafa ya kibinadamu na janga baya zaidi la njaa."

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X Abeer Etefa, msemaji wa Ofisi ya WFP Mashariki ya Kati amesema "Operesheni za kibinadamu huko Gaza ziko karibu kuporomoka, na ikiwa chakula na vifaa vingine havitaanza tena kwa wingi, hali ya janga la njaa itasambaa." 

Kuelekea janga la kibinadamu

Tahadhari hii inakuja wakati "kwa mara nyingine tena, karibu nusu ya wakazi wa Rafah, ambao ni zaidi ya watu 800,000, wako kwenye harakati, wakitafuta chakula na malazi katika maeneo ya kati ya ukanda huo wa Gaza na Khan Younis.”

Hata hivyo, kwa sasa hakuna usambazaji wa chakula kusini mwa Gaza, isipokuwa akiba chache ambayo hutolewa katika majikoni ya jumuiya kwa ajili ya milo ya moto. "Chini ya malori 100 yameingia kusini mwa Ukanda wa Gaza tangu Mei 6."

Hiki ndicho kiwango cha chini kabisa cha bidhaa za kibinadamu zinazoingia Gaza tangu Desemba mwaka jana, "na kufanya hatari ya njaa kuwa hali halisi", limeongeza shirika hilo.

WFP ilitoa chakula cha moto milo milioni 4.4 mwezi Mei

WFP imesema haikuweza kufikia ghala lake kuu huko Rafah kutokana na uhasama unaoendelea, wakati kufungwa kwa vivuko vya mpaka kusini kunamaanisha "hakuna chakula, hakuna mafuta au misaada haijawasilishwa.”

Licha ya vikwazo hivi vya ufikiaji, WFP inafanya kazi ya kusambaza bidhaa zilizosalia kwa watu wengi iwezekanavyo. 

Maduka manne ya kuoka mikate pia yamefunguliwa na yanafanya kazi katika Jiji la Gaza, yakitoa mkate ambayo ni chakula muhimu kaskazini. 

Kati ya viwanda 16 vya kuoka mikate ambavyo WFP inaviendesha huko Gaza, ni kumi pekee vinavyofanya kazi kutokana na ukosefu wa mafuta na mahitaji mengine ya msingi.

Tangu mwanzoni mwa mwei Mei, WFP imetoa takriban milo milioni 4.4 ya chakula cha moto kupitia majiko 70 ya jumuiya katika Ukanda wa Gaza, wakati viwanda vya kuoka mikate vimezalisha zaidi ya pakiti milioni 1 za mikate ya bapa.

Wakimbizi wa ndani wakitembea katika eneo la Al Mawasi, Khan Younis, wakipitia rundo kubwa la takataka karibu na mahema ya muda katika mazingira ya mgogoro wa kibinadamu.
© WHO Wapalestina waliokimbia makazi yao wanaishi miongoni mwa milundo ya taka katika eneo la Al Mawasi magharibi mwa Khan Younis.

Watu waliokimbia makazi yao wanaishi kwenye vifusi

Ripoti za vyombo vya habari zinaonyesha kuendelea kwa mapigano huko Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza, na Jabalia, kaskazini, huku wanajeshi wa Israel wakisonga mbele katika maeneo yote mawili.

Mapigano haya yamesababisha robo tatu ya wakazi wa Gaza kulazimika kuhama mara nyingi wengine hadi mara 4 au 5, kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA.

"Kwa maelfu ya familia za Wapalestina, hakuna mahali pa kwenda tena, operesheni za kijeshi na milipuko ya mabomu ni tishio la kudumu, majengo yamesalia kuwa magofu. Hakuna mahali salama katika eneo la Gaza."

Katika hali hizi, watu waliofurushwa na amri ya jeshi la Israeli ya kuondoka Rafah sasa wanaishi katika hali mbaya katika mji wa karibu wa Khan Younis. 

Wale wanaohitaji usaidizi ni "familia zinazoishi katika vifusi kenye shule zilizoharibiwa, huku wakikosa mahema, huduma muhimu na vifaa muhimu," limeeleza shirika la UNRWA.

WHO yazindua ombi la dharura kwa ajili ya hospitali ya al-Awda

Katika hali nyingine, Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO linaripoti kwamba magonjwa ya kuambukiza, ikiwa ni pamoja na kuhara na homa ya ini aina A au hepatitis A, yanaongezeka katika Ukanda wa Gaza. 

"UNRWA inaendelea kutoa huduma za afya, lakini makazi yenye msongamano mkubwa wa watu na usafi mdogo kutokana na kulazimishwa kuhama huleta hatari kubwa kiafya."

Hatari hizi za kuenea kwa magonjwa zinakuja wakati ambapo vikosi vya Israel vilivamia hospitali ya al-Awda huko Gaza, ambayo imekuwa ikizingirwa na wanajeshi wa Israel na vifaru tangu Jumapili iliyopita. Umesema ujumbe uliochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa X wa shirika hilo.

Kulingana na Dkt.  Tedros Adhanom Ghebreyesus ambaye ni mkurugenzi mkuu wa WHO, wahudumu wa afya 140, wagonjwa na wenzao raia walikuwa ndani ya hospitali hiyo ilipovamiwa na wanajeshi wa Israeli mapema asubuhi. 

Wanajeshi waliripotiwa kuamuru kila mtu kuondoka isipokuwa wafanyikazi 12, akiwemo mkurugenzi wa hospitali, wagonjwa 14 na wahudumu wanane.

Daktari aliyevaa vitambaa vya bluu na barakoa nyeupe akimsaidia mgonjwa aliyelala sakafuni katika Hospitali ya Al-Aqsa huko Gaza. Wafanyakazi wengine wa matibabu na watu wamekusanyika katika chumba cha hospitali.
WHO Daktari akimtibu mgonjwa mdogo katika hospitali ya Al-Aqsa katikati mwa Gaza. (Maktaba)

Hospitali nyingine huko Jabalia haifanyi kazi tena

Dkt. Tedros ametoa wito kwa watu walioamriwa kusalia na vikosi vya Israel walindwe na kuruhusiwa kuondoka salama. 

"WHO inatoa wito wa dharura ya ulinzi wa wagonjwa, waandamanaji wao na wahudumu wa afya ndani ya hospitali, pamoja na njia salama ya kuhamishwa kwa wagonjwa," ameongeza.

Katika ujumbe mwingine, mkuu huyo wa WHO pia amedai kuwa hospitali ya Kamal Adwan, ambayo pia iko katika eneo la Jabalia kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, "haijafanya kazi tena baada ya wagonjwa wote na wafanyikazi kuhamishwa kufuatia mashambulio mengi ya makombora ya Israeli kwenye eneo hilo na kituo hicho jana Jumatano.”

Baadhi ya wagonjwa walirejea nyumbani, huku wengi wao wakipewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Al-Ahli. Al-Ahli kisha iliwapeleka wagonjwa kwenye utulivu katika Hospitali ya Al Helou.

Kwa upana zaidi, upatikanaji wa huduma za afya huko Gaza unapungua zaidi limesema shirika la WHO. "Hospitali nyingi hazina mafuta na dawa kutokana na kuendelea kufungwa kwa kivuko cha Rafah," amesema Dk. Tedros.

Uchunguzi ufanyike dhidi ya madai ya utesaji wa mahabusu

Katika hatua nyingine Mtaalamu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mateso, Alice Jill Edwards, ameitaka Serikali ya Israel kuchunguza tuhuma nyingi za mateso na vitendo vingine vya kikatili, vya kinyama au vya udhalilishaji dhidi ya Wapalestina wanaozuiliwa tangu tarehe 7 Oktoba 2023.

Katika tarifa yake iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis Edwards amesema "Watu walionyimwa uhuru lazima kila wakati watendewe kiutu. Lazima wapewe ulinzi wote unaohitajika chini ya haki za binadamu za kimataifa na sheria za kibinadamu, bila kujali mazingira ya kuwekwa kizuizini."

Tangu mashambulizi ya tarehe 7 Oktoba 2023, inakadiriwa kuwa maelfu ya Wapalestina wakiwemo watoto wamezuiliwa mahabusu. 

Wapalestina kutoka Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki, na kutoka Gaza wanazuiliwa katika magereza yanayosimamiwa na Jeshi la Magereza la Israel na katika kambi za Jeshi la Ulinzi la Israel IDF.