Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WMO: Pembe ya Afrika kushuhudia mvua juu ya kiwango mwezi Juni- Septemba

Watu hutembea kwenye barabara yenye vumbi huko West Gonder, Ethiopia, wakiwa wamepiga picha nyeusi na nyeupe kwa ajili ya Shindano la Kalenda la WMO 2024.
© WMO/Abenezer Israel Watu wa Gondar Kusini mwa eneo la Amhara la Ethiopia wakitembea vijijini.

WMO: Pembe ya Afrika kushuhudia mvua juu ya kiwango mwezi Juni- Septemba

Tabianchi na mazingira

Shirika la Umoja wa Mataifa la hali ya hewa WMO limetangaza kuwa katika kipindi cha mwezi Juni mpaka Septemba nchi zilizoko katika pembe ya Afrika zinatabiriwa kuwa na mvua kubwa  na hii ikijumuisha nchi za Djibouti, Eritrea, Ethiopia ya kati na kaskazini, magharibi na pwani ya Kenya, sehemu kubwa ya Uganda, Sudan Kusini, pamoja na Sudan.

Taarifa iliyochapishwa kwenye wavuti wa WMO imeeeleza kuwa utabiri huo ni kwa mujibu wa Kituo cha Utabiri wa Hali ya Hewa cha IGAD (ICPAC), ambacho kinatumika kama kituo cha kikanda cha WMO.

“Hali iliyotabiriwa ya mvua kuliko kawaida kati ya Juni hadi Septemba 2024 inalingana na mifumo ya mwaka 1998 na 2010, yenye hatari ya mafuriko hasa katika nchi za Sudan Kusini na Sudan” amesema Dkt. Guleid Artan, Mkurugenzi wa ICPAC.

Utabiri huu wa hali ya hewa ni muhimu kwaajili ya kufanya maamuzi katika sekta kama kilimo, afya na usimamizi wa rasilimali za maji. Pia ni utekelezaji wa mpango wakutoa Maonyo ya Mapema kwa Wote.

Juni hadi Septemba ni msimu muhimu wa mvua katika maeneo ya kaskazini na magharibi ya Pembe Kubwa ya Afrika, ambapo kwa ujumla huchangia zaidi ya 90% ya mvua kwa mwaka katika sehemu ya kaskazini ya eneo hilo na 40% katika maeneo ya kusini.

Nchi ambazo zimekumbwa na mafuriko hivi karibuni huenda mwezi Juni mpaka Septemba zitakuwa katika msimu wa kiangazi. Nchi hizo ni pamoja na Burundi, Kenya, Rwanda, Tanzania na sehemu za Ethiopia, Somalia na Uganda.

Mvua zinatarajiwa kuanza hadi kuwa za kawaida katika maeneo kadhaa ya kanda ikiwa ni pamoja na Kati pamoja na Kaskazini mwa Ethiopia, Eritrea, Sudan, na Sudan Kusini. Hata hivyo, zinatarajiwa kuchelewa kuanza katika maeneo ya Djibouti, sehemu za mashariki na magharibi mwa Ethiopia, kati na magharibi mwa Sudan, na kusini mwa Sudan Kusini.

WMO wametoa utabiri wa hali ya joto unaoonesha uwezekano wa hali ya joto kuliko kawaida katika eneo lote, hasa kaskazini mwa Sudan, kati na magharibi mwa Ethiopia, Somalia, Kenya, Rwanda, Burundi na Tanzania.

Utabiri huu ulitolewa katika Kongamano la Mtazamo wa Hali ya Hewa wa Pembe ya Afrika, ambalo linawaleta pamoja wanasayansi wa hali ya hewa, mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali, na sekta zinazoathiriwa na hali ya hewa.