Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chai ni sehemu ya urithi na historia yetu, Je ilianzia wapi?

Mkurugenzi Mkuu wa FAO Qu Dongyu atembelea tukio la kuonja chai na kahawa katika makao makuu ya FAO mjini Rome, Italia.
©FAO/Alessia Pierdomenico
Mkurugenzi Mkuu wa FAO Qu Dongyu atembelea tukio la kuonja chai na kahawa katika makao makuu ya FAO mjini Rome, Italia.

Chai ni sehemu ya urithi na historia yetu, Je ilianzia wapi?

Masuala ya UM

Je! unajua kuwa watu wengi ulimwenguni hutumia maneno mawili sawa kwa chai? Tofauti moja ni ile inayotumika katika Kiingereza (Tea), Kifaransa (thé), Kihispania (té) na Kiholanzi (thee). 

 

 

Tofauti nyingine ni ya chá (katika Mandarin na Cantonese), kama vile chai katika Kihindi, shay katika Kiarabu na chay katika Kirusi. Kuna sababu ya kuvutia kwa jambo hili. 

Maneno yote mawili yanatoka China, nchi ambayo inaaminika sana kuwa 'nyumbani kwa chai' na ambapo mmea ulikuzwa kwa mara ya kwanza. Maneno haya yanatoka kwa herufi  za Kichina: 茶.  Katika Mandarin na Cantonese, hutamkwa 'cha'. Nchi mbalimbali duniani zinazotumia neno ‘cha’ ziliagiza chai kwa njia ya ardhi, kupitia Barabara ya Hariri, kutoka maeneo ya kaskazini mwa China ambapo wanasema neno ‘cha’.

Hata hivyo, katika lahaja inayozungumzwa katika jimbo la kusini la pwani la Fujian, neno hilo linatamkwa ‘te’. Bandari hii ndiyo mahali wafanyabiashara wa Kiholanzi wa karne ya 17 walibadilishana chai na kuileta Ulaya, wakiwa na matamshi ya ‘tea’. Bila shaka, kuna tofauti za hili. Lakini kwa sehemu kubwa, popote ulipo duniani, kuna nafasi nzuri utaweza kuomba kikombe cha chai kwa kutumia maneno hayo mawili tu!

Asili ya chai ni moja tu ya vipengele vya urithi wake wa kuvutia. Ukuaji na uzalishaji wake umekuwa sehemu ya tamaduni kote ulimwenguni kwa karne nyingi. Kwa kutambua hili, Shirika la Umoja wa Mataifala la Chakula na Kilimo (FAO) limepanga maeneo matano ya uzalishaji wa chai kuwa Mifumo Muhimu ya Urithi wa Kilimo Ulimwenguni  (GIAHS) kufuatia mchanganyiko wao wa mandhari ya kipekee, urithi wa kilimo, na njia za kilimo za jadi zilizopitishwa kizazi baada ya kizazi.

Mfumo wa Jadi wa Kilimo cha Chai wa Pu'er Mkoani Yunnan, Uchina 

Mkoa wa Yunnan unachukuliwa kuwa mahali chai ilikozaliwa ulimwengu. Mfumo wa Kilimo wa Chai wa Pu'er huko Yunnan ndio eneo kubwa zaidi ulimwenguni la mashamba ya misitu ya chai, ambapo miti mingi ya chai hupandwa pamoja kwa kuiga mfumo ikolojia wa msitu, ulioanzishwa na mababu wa kijiji maelfu ya miaka iliyopita na kulimwa kwa kutumia mbinu za kitamaduni. Mfumo huu una wingi wa baionuai za kitamaduni na unajumuisha miti ya zamani ya chai ya mwituni na mashamba ya zamani ya chai yaliyolimwa.

Udhibiti wa wadudu unafanywa kwa njia za asili ambazo pia husaidia kuboresha ladha ya chai.

Kuonja chai ya Jasmine ya Kichina. Mkutano wa Kamati ya Uongozi na Kisayansi ya Mifumo ya Urithi Muhimu wa Kilimo Duniani (GIAHS), makao makuu ya FAO.
FAO/Alessandra Benedetti.

Mfumo wa Utamaduni wa Chai ya Jazamini katika Jiji la Fuzhou, China 

Mfumo wa chai ya jasmine ni chanzo kikuu cha riziki kwa jamii za eneo hilo na mfumo wa ikolojia unaokua nao unasaidia ukuaji wa mazao mbalimbali. Uyoga, chai ya jasmine, maziwa na nyama vyote huzalishwa katika eneo hilo kutokana na miti ya jasmine na chai ambayo inaboresha uhifadhi wa maji na udongo kwa njia nyingi. Miti ya jasmine pia hutoa ulinzi dhidi ya vipengele vya mazingira. Ikipandwa kwenye nyanda za mto na kingo, huzuia mvua kunyoosha moja kwa moja kingo za mto, na hivyo kupunguza mmomonyoko wa udongo na maji. 

Mfumo wa Utamaduni wa Chai wa Anxi Tieguanyin, China 

Mti wa chai wa Tieguanyin, uliogunduliwa kwanza katika bustani za chai za Anxi, Uchina, ndiko asili ya chai pendwa ya Oolong

Kupitia desturi za kitamaduni kama vile roho ya chadao (Njia ya Chai, inayorejelea njia ya kisanii, ya sherehe ya kutengeneza chai, kunywa chai na taratibu zinazohusiana) na kile kinachoitwa Vita vya Chai (njia ambayo wakulima wa chai wanawasiliana, kujifunza na kushindana kwa kila mmoja kuhusu mbinu za kutengeneza chai), utamaduni wa chai wa Anxi Tieguanyin unaendelea kuathiri desturi za kijamii na mbinu za kutengeneza chai duniani kote leo. 

Mfumo wa Utamaduni wa Kuzalisha Nyasi za Chai huko Shizuoka, Japani   

Mkoa wa Shizuoka ndio eneo kubwa zaidi la uzalishaji wa chai nchini Japani, na takriban asilimia 78 ya wakulima wa eneo hilo hutegemea chai kwa kipato. Eneo hilo linajulikana kwa chai yake iliyokaushwa kwa mvuke mwingi, ambayo ina harufu tofauti na rangi ya kijani kibichi.

Wakulima wa chai pia hutumia mashamba ya pamoja yanayoitwa Chagusaba kukuza na kuvuna nyasi asilia ambazo hukatwa na kutandazwa kwenye shamba la chai kwa usimamizi bora wa udongo na kuboresha ubora wa chai. Baadhi ya Chagusaba ni maeneo ya kawaida ambapo wanajamii wanaweza kupata rasilimali za nyasi wanapohitaji, wakati baadhi ya Chagusuba wanasimamiwa kwa njia iliyopangwa zaidi.

Chai ikivunwa huko Fuzhou, Uchina.
FAO/Fuzhou Agricultural and Rural Bureau
Chai ikivunwa huko Fuzhou, Uchina.

Mfumo wa Kilimo cha Chai wa Kiasili wa Hadong katika Hwagae-myeon, Jamhuri ya Korea  

Mfumo wa kilimo cha chai wa kiasili wa Hadong ni mfumo wa kilimo ulioundwa na jamii za wenyeji kwa misingi ya miaka 1,200 ya kuzoea mazingira kame ya Mlima Jiri. Zaidi ya asilimia 90 ya eneo la Hwagae-myeon ni ardhi yenye milima mikali na mafuriko ya mara kwa mara wakati wa msimu wa mvua, na kufanya shughuli za kilimo kuwa ngumu sana. Watu wa Hwagae hutegemea kilimo cha chai badala ya mashamba ya mpunga ili kujipatia riziki. 

Uzalishaji wa chai ni muhimu katika kupambana na njaa, kupunguza umasikini uliokithiri, kuwawezesha wanawake na matumizi endelevu ya ardhi. Hii ndiyo sababu Umoja wa Mataifa uliteua tarehe 21 Mei kuwa Siku ya Kimataifa ya Chai,, ili kusherehekea uzalishaji wa chai na kuongeza uelewa wa umma kuhusu umuhimu wa chai kwa maendeleo ya vijijini, riziki endelevu na mchango wake katika Malengo ya Maendeleo Endelevu. .