WEIF2024 yaanza Bahrain ikilenga kuchochea ugunduzi na ujasiriamali
WEIF2024 yaanza Bahrain ikilenga kuchochea ugunduzi na ujasiriamali
Jukwaa la tano la kimataifa la uwekezaji kwa ujasiriamali, WEIF2024 linaloungwa mkono na Umoja wa Mataifa limeanza leo huko Manama, Bahrain likiwa na wawakilishi wa serikali, mashirika ya kiraia, wawekezaji, wasomi na wabunifu na wakitoka pembe zote za dunia kwa lengo la kusaka mbinu za kuchochea ubunifu na ugunduzi ili hatimaye kusaidia kusongesha malengo ya maendeleo endelevu.
Likiwa na maudhui Kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu kwa kuchochea ubunifu na ukuaji wa kiuchumi, jukwaa linafanyika kwa siku tatu likimulika majawabu ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi, umaskini, ukosefu wa usawa, katika muktadha wa SDGs.
Dhima muhimu
Akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa kando mwa mkutano huo, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la maendeleo ya viwanda, UNIDO, moja ya wawezeshaji na waandaji wa jukwaa hilo, Bi. Fatou Haidara amesisitiza nafasi muhimu ya sekta binafsi katika maendeleo ya kiuchumi hasa katika nchi zinazoendelea.
Ameesma “hii inaonesha umuhimu wa jukwaa hili, kwa kuwa sio tu sekta binafsi bali pia sekta zote, watunga sera, wanazuoni, taasisi za uwekezaji na za kifedha na jinsi gani zinaweza kuchagiza utekelezaji wa SDGs.
Akimulika umuhimu wa hatua za pamoja, Bi. Haidara amesisitiza kuwa, “changamoto tunazokabili leo hii haziwezi kutatuliwa na shirika au kundi moja. Tunahitaji juhumu za pamoja.”
Likiwa linajikita kewnye kuchochea ubia, WEIF 2024 inalenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kwa kuunganisha wadau wa nchi za kiarabu na wale wa Afrika na kusongesha uwekezaji na maendeleo ya ujasiriamali.
Bi. Haidara ameendelea kusisitiza dhima muhimu ya sekta binafsi katika kushochea uwekezaji, teknolojia, na kusisitiza kuwa mambo hayo ni muhimu katika kusongesha utekelezaji wa SDGs.
"Uwekezaji katika maeneo ista”
Wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Rola Dashti, Katibu Mtendaji wa Tume ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi na Kijamii kwa nchi za Magharibi mwa Asia, ESCWA amezungumzia azma ya jukwaa ya kutafsiri SDGs katika matokeo dhahiri.
Amesihi wadau kutumia mabadiliko ya kiditali na kuimarisha mifumo ya elimu ili kukabili mabadiliko ya tabianchi na kuanzisha ajira jumuishi, akiongeza juu ya udharura wa ubia wa kimkakati na kutatua changamoto kubwa zinazokabili dunia.
"Waumbaji wa mapinduzi yajayo”
Bi. Dashti amezungumzia dhima muhimu ya viongozi na wajasiriamali vijana na kusisitiza kuwa wao ni waumbaji wa mapinduzi yajayo ya maendeleo duniani.. Hebu na tuhamasike na nia ya pamoja ya jukwaa hili na tukumbuke kuwa kazi yetu inaanzia hapa.
Dhima ya Vyuo Vikuu
WEIF 2024 inasisitiza umuhimu wa ubia katika sekta zote ikiwemo Vyuo Vikuu. Dkt. Lydia Takyi, kutoka Chuo Kikuu cha AAMUSTED nchini Ghana amesisitiza kuwa jukwaa limefanyika wakati muafka kutatua changamoto lukuki zinazokabili wahitimu wa Vyuo Vikuu.
Ilikuwa muhimu, amesema, kupatia wanafunzi stadi za ujasiriamali na kuwapatia stadi za kupata fedha, kujenga mitandao huku akisisitiza umuhimu wa Vyuo Vikuu katika kukuza uchumi.