Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika inaweza kuwa jabalí la nishati jadidifu- Guterres

Katibu Mkuu UN Antonio Guterres akizungumza kwenye jukwaa wakati wa Kongamano la Mashirika ya Kiraia UMOJA WA MATAIFA ya 2024 jijini Nairobi.
UNEP/Duncan Moore Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza na waandishi wa habari jijini Nairobi, Kenya.

Afrika inaweza kuwa jabalí la nishati jadidifu- Guterres

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyeko Nairobi Kenya kushiriki mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mashirika yasiyo ya kiserikali, UNCSC amezungumza na waandishi wa habari ambapo pamoja na mambo mengine amesema wakati huu ambapo bara la Afrika linakabiliwa na madhara ya mabadiliko ya tabianchi, bara hilo linaweza kuwa jabalí wa uzalishaji nishati jadidifu duniani iwapo litawezeshwa.

Afrika ina rasilimali lakini hakuna usawa kwenye uwekezaji

Tweet URL

Katibu Mkuu Guterres amesema dunia inakabiliwa na majanga lukuki, lakini Afrika ndio inaathiriwa vibaya kwa kiasi kikubwa.

Bara la Afrika linatikiswa na hali mbayá ya hewa kupindukia, ikichochewa na janga la tabianchi ambalo halijasababishwa na bara hili. Kuanzia mafuriko makubwa mashariki hadi ukame mkali kusini.

Afrika inaweza kuwa jabali la nishati jadidifu, amesema Guterres,  kwani ina hifadhi ya asilimia 30 ya madini muhimu kwa ajili ya nishati jadidifu, na asilimia 60 ya rasilimali ya sola au nishati ya jua. Lakini katika dunia hii isiyo ya haki kwenye miongo ya karibuni, imepokea asilimia mbili tu ya uwekezaji kwenye nishati jadidifu.

Amesema jopo la mpito muhimu wa madini husika kwenye nishati litaandaa kanuni za hiari ili nchi zinazoendelea zinufaike na rasilimali hizo.

Ametoa wito kwa nchi zilizoendelea kutimiza ahadi zao za ufadhili kwa tabianchi ikiwemo kusaidia nchi kujiandaa kwa madhara makubwa ya tabianchi, na serikali za Afrika ziunge mkono juhudi za kuondokana na mafuta kisukuku.

“Nchi hizo zichangie ipasavyo kwenye mfuko wa Hasara na Uharibifu, marekebisho ya mifumo ya benki za kimataifa za maendeleo ili fedha ziweze kuelekezwa kwenye hatua kwa tabianchi,” amesema Katibu Mkuu.

Umuhimu wa Mkutano wa UN wa Mashirika ya Kiraia

Guterres amewaambia waandishi wa habari kuwa mkutano huo wa mashirika ya kiraia unaofanyika Kenya kwa mara ya kwanza una mchango mkubwa katika mkutano wa zama zijazo au Summit of The Future utakaofanyika mwezi Septemba mwaka huu kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa.

Katibu Mku amesema mashirika ya kiraia ni kitovu cha malengo ya mkutano huo ambayo ni kusongesha malengo ya maendeleo endelevu, kufanikisha upatikanaji wa fedha na kuumba upya ushirikiano wa kimataifa kwa karne hii ya 21.

“Nimefurahishwa sana na uwepo wa washiriki tofauti tofauti katika mkutano huu, wakiwemo vijana wengi na wawakilishi kutoka nchi za Afrika. Mchango wao ni muhimu.”

Katibu Mkuu UN António Guterres akipitia ukumbi wa mkutano jijini Nairobi akiwa na wajumbe wengine.
UN Nairobi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (katikati) akihudhuria Kongamano la Asasi za Kiraia ya Umoja wa Mataifa mjini Nairobi, Kenya.

Gaza na Sudan

Katika hotuba yake hiyo, Katibu Mkuu amerejelea wito wa kutaka serikali ya Israel na wanamgambo wa Hamas waoneshe ujasiri wao wa kisiasa wa kutumia juhudi zote kufikia makubaliano na kukomesha umwagaji damu, sambamba na kuachilia huru mateka wote.

Amerejea tena kuwa shambulio la ardhini huko Rafahm, kusini mwa Gaza kutasababisha janga kubwa la kibinadamu.

Kuhusu mizozo Afrika amesema Umoja wa Mataifa unaunga mkono kazi ya Muungano wa Afrika ya kunyamazisha silaha. Tuko tayari kushirikiana na kuhamasisha jamii ya kimataifa iunge mkono mchakato wa kusaka amani kuanzia Sahel, Pembe ya Afrika, Maziwa Makuu na kwingineko.

Amesema anaumizwa zaidi na vita inayoendelea Sudan ambako tunashuhudia mashambulizi holela dhidi ya raia, ukatili wa kingono dhidi ya wanawake na wasichana huku watoa huduma za kiutu wakiwa wamewekewa vikwazo kufanya kazi yao.

Guterres ametaka pande husika kwenye mzozo Sudan kuzingatia sheria ya kimataifa ya kibinadamu na haki za binadamu.

Kenya kwenda Haiti

Ametumia pia hotuba yake kupongeza Kenya kwa kukubali kuongoza juhudi za kimataifa za kukabili ghasia nchini Haiti, wakati huu ambapo taifa hilo linakumbana na madhara ya mafuriko yaliyosababisha vifo, ukimbizi na uharibifu wa mali.

“Punde polisi wa Kenya watakuwa Haiti kusaidia kuimarisha amani, tunaipongeza Kenya kwa hatua hiyo.” Amesema Guterres alipoulizwa kwa nini mkutano umefanyika Kenya na ndipo akasema umuhimu wa Kenya kwenye ushirikiano wa kimataifa na pia hatua hiyo ya kuamua kuongoza kikosi cha kimataifa cha kuleta amani Haiti.

Katibu Mkuu UN António Guterres na Rais wa Kenya William Ruto wameketi na kutabasamu wakati wa mkutano katika Kongamano la Mashirika ya Kiraia jijini Nairobi.
UN Nairobi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akutana na Rais William Ruto wa Kenya.

Guterres azungumza na Rais Ruto

Mapema Katibu Mkuu Guterres alikuwa na mazungumzo na Rais wa Kenya Dkt. William Ruto ambapo pamoja na kumpatia salamu za rambirambi kwa vifo vya watu na uharibifu wa mali uliosababishwa na mafuriko makubwa nchini humo, amemshukuru kwa kazi ya taifa hilo la Afrika Mashariki ya kuandaa mkutano huo wa mashirika ya kiraia.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Umoja wa Mataifa imesema Guterres ameshukuru Kenya kwa uongozi wake kwenye kikosi cha kimataifa cha usaidizi wa usalama huko Haiti. 

Viongozi hao pia wamejadili amani na usalama Pembe ya Afrika na Maziwa Makuu. 

Halikadhalika Katibu Mkuu amerejelea umuhimu wa Nairobi kama kituo cha makao makuu ya Umoja wa Mataifa na kuelezea shukrani zake kwa Rais Ruto kwa msaada ambao Umoja huo unapokea kutoka serikali ya Kenya.

Asasi za kiraia mchango wenu ni muhimu 

Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo wa kwanza kabisa kufanyika Afrika, Katibu Mkuu na Rais Ruto wamepongeza juhudi za mashirika ya kiraia na umuhimu wao pamoja na michango yao ya kipekee.
 
Guterres amesema kila wakati nimeshuhudia mchango wa asasi za kiraia kwenye pembe zote za dunia; zikipunguza machungu, zikishinikiza amani na haki, zikisimamia ukweli na kusongesha usawa wa jinsia na maendeleo endelevu, nyingi zao zikifanya kazi zikihatarisha mustakabali wao.
 
Amesema kuwa ushiriki wa mashirika hayoya kiraia ni muhimu katika kutatua changamoto nyingi zinazokabili dunia leo hii, ikiwemo utatuzi wa majanga, kupunguza pengo la kidijitali na kuchochea juhudi za pamoja za amani na usalama.