Watu 80,000 wamefungasha virago Rafah makombora ya Israel yakiendelea kumiminika: UN
Watu 80,000 wamefungasha virago Rafah makombora ya Israel yakiendelea kumiminika: UN
Takriban watu 80,000 wamekimbia Rafah tangu Jumatatu wiki hii huku kukiwa na mashambulizi yanayoendelea ya Israel ndani na katika viunga vya mji huo wa kusini mwa Gaza usiku kucha kuamkia leo Alhamisi, yameripoti mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa.
Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA “Wengi wa wale waliotimuliwa na amri ya kuondoka ya jeshi la Israel Mashariki mwa Rafah tayari wamefurushwa kutoka maeneo mengine ya Gaza sasa wanaondoka na kila kitu wanachoweza kubeba wakitumia magari, malori, bodaboda na mikokoteni ya punda.”
Zaidi ya watu 47,500 wanakadiriwa kuondoka kwenye makazi yao huko Rafah siku ya jana Jumatano pekee, limesema shirika la UNRWA, huku baadhi ya familia zikikaribia makazi ya shirika hilo huko Tel Sultan, pamoja na Al Mawasi magharibi mwa Rafah.
Mabomu kila kona
Katika tarifa yake UNRWA imebainisha kuwa "Kumekuwa na kiwango kikubwa kinachoendelea cha mashambulizi mashariki mwa Rafah mapema Alhamisi na usiku kucha kuamkia leo".
Haya yanajiri huku wahudumu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wakirudia kuonya kuhusu ukosefu wa misaada inayohitajika sana kuwafikia watu walio hatarini zaidi huko Gaza, licha ya ripoti kwamba kivuko cha Kerem Shalom karibu na Rafah kimefunguliwa tena.
"Tunashirikiana na wote wanaohusika katika kurejesha uingiaji wa bidhaa na misaada, ikiwa ni pamoja na mafuta, na ili tuanze tena kusimamia vifaa vinavyoingia," imesema ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura, OCHA."
Hata hivyo, sofisi hiyo imeongeza kuwa hali inasalia kuwa tete sana na tunaendelea kukabiliana na changamoto mbalimbali, huku kukiwa na uhasama mkali.
Tunategemea ushirikiano na uwezeshaji kufanya kazi hizi za kuvuka tena kwa kuwa hifadhi ya vifaa muhimu, ikiwa ni pamoja na mafuta, inapungua kwa saa.
Kivuko cha Kerem Shalom kilikuwa kimefungwa kufuatia shambulio baya la roketi lililodaiwa na Hamas mwisho wa wiki iliyopita.
Ni karibu na Rafah ambayo ni kitovu kikuu cha kuingilia Gaza na ambacho kilitekwa siku ya Jumanne na wanajeshi wa Israel, na hivyo kukatisha matumaini ya kusitisha mapigano.
Ucheleweshaji wa misaada ya Kaskazini
Kwa mujibu wa OCHA, zaidi ya robo ya operesheni za kibinadamu kaskazini mwa Gaza mwezi wa Aprili "zilizuiliwa na mamlaka ya Israeli, na asilimia 10 ilikataliwa. Umoja wa Mataifa na washirika wa kibinadamu wanaendelea na jitihada za kuongeza shughuli za misaada wakati wowote na popote iwezekanavyo."
Siku ya Jumatano Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa duniani WFP liliripoti kwamba lilifika Beit Hanoun, kaskazini mwa Gaza eneo ambalo lilikuwa hafikiki kwa miezi kadhaa".
Katika ujumbe kwenye mtandao wa X, shirika hilo limesema kuwa liko tayari kuongeza msaada wa chakula kaskazini mwa Gaza, "lakini kubadili mwenendo wa miezi sita ya njaa kunahitaji mtiririko wa kutosha wa chakula. Ufikiaji salama na wa kudumu unahitaji kudumishwa kwa muda”.
Vurugu Ukingo wa Magharibi zimeshamiri
Wakati vita ikiendelea Gaza, ofisi ya haki za Umoja wa Mataifa, OHCHR, imeonya kwamba ukiukwaji wahaki dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu pia umeongezeka kwa kiasi kikubwa.
"Jeshi la Ulinzi la Israel IDF linafanya kana kwamba kuna mzozo wa silaha katika Ukingo wa Magharibi," amesema Ajith Sunghay, mkuu wa ofisi ya OHCHR katika eneo linalokaliwa la Palestina, wakati wa mahojiano na UN News.
Bwana Sunghay ameeleza kuwa hali katika Ukingo wa Magharibi tayari ni mbaya sana hata kabla ya mapigano kuzuka huko Gaza kufuatia mashambulizi ya Hamas kusini mwa Israel na kusababisha vifo vya watu 1,250 na zaidi ya 250 kuchukuliwa mateka.
Katika taarifa yake ya hivi karibu kuhusu hali ya Ukingo wa Magharibi, ofisi ya OCHA imebainisha kuwa Mahakama ya Juu ya Israel imetoa uamuzi wa kuunga mkono kurejeshwa kwa Wapalestina 360 katika makazi yao katika jamii ya wafugaji ya Khirbet Zanouta huko Hebron, miezi sita baada ya kufurushwa katika makazi yao na mashambulizi ya walowezi.