Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tanzania yalalamikiwa kuhusu maisha ya watu wenye ualbino

Nchini Tanzania, chama cha watu wenye ualbino, TAS kinaendesha programu za kuelimisha watu kuhusu haki za watu wenye ualbino. Pichani ni mkoani Morogoro, mashariki mwa Tanzania, mafunzo yakiendelea kwa wanafunzi.
UN News
Nchini Tanzania, chama cha watu wenye ualbino, TAS kinaendesha programu za kuelimisha watu kuhusu haki za watu wenye ualbino. Pichani ni mkoani Morogoro, mashariki mwa Tanzania, mafunzo yakiendelea kwa wanafunzi.

Tanzania yalalamikiwa kuhusu maisha ya watu wenye ualbino

Haki za binadamu

Kushindwa kwa Tanzania kulaani na kuchunguza mashambulizi dhidi ya watu wenye ualbino kunaweza kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa wajibu wake wa kuwalinda watu wenye ulemavu, wamesema wataalamu wa Umoja wa Mataifa leo katika Ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi.

Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Watu Wenye Ulemavu (CRPD) imeeleza masikitiko yake leo kwa Tanzania kutokuwa tayari kufuatilia maombi matatu yaliyowasilishwa kwenye Kamati hiyo kuhusu ukataji wa viungo vya watu wenye ualbino na kutowajibika kwa Tanzania dhidi ya unyanyasaji huo.

"Tunatoa wito kwa (Tanzania) kulaani kwa haraka na bila utata mashambulizi yoyote dhidi ya watu wenye ualbino na kuchunguza mashambulizi yoyote kama hayo kwa haraka na kwa ufanisi," amesema mjumbe wa Kamati Amalia Gamio Ríos akiongeza kwamba, "kukosa kufanya hivyo kunatoa ujumbe kwamba mauaji ya kishirikina na ukataji viungo yamesamehewa, ambayo ni sawa na ukiukaji mkubwa wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu.”

Kamati ilikuwa imechunguza matukio matatu yaliyotokea nchini Tanzania kati ya mwaka 2008 na 2010. Katika kisa kimoja, mkulima X alivamiwa na wanaume wawili Aprili mwaka 2010 wakati akichanja kuni. Waliukata mkono wake wa kushoto, ambao haukupatikana kamwe. Licha ya kuripoti shambulio hilo kwa polisi, X alidai kuwa mamlaka haikuchunguza suala lake.

Katika tukio la pili, Y na kaka yake walitelekezwa na familia yao kwa sababu ya ualbino. Walilazimika kuacha kuhudhuria shule ya msingi kutokana na kukithiri kwa mauaji na ukatili dhidi ya watu wenye ualbino. Akiwa na umri wa miaka 12, Y alivamiwa na mtu mmoja kwa panga Mkoani Geita, na kuchukua vidole vitatu vya mkono wa kulia na kumkata bega la kushoto na kusababisha kushindwa kutumia kiganja cha kulia na mkono wa kushoto.

Mama asiye na mume, Z alivamiwa Oktoba 2008 na wanaume wawili ambao walimkata mkono mmoja kwa mapanga na kumlemaza mwingine. Walikimbia na mkono wake. Mkono mwingine ulikatwa baadaye. Z alikuwa mjamzito wakati huo, lakini kwa sababu ya shambulio hilo, alipoteza mimba. Uchunguzi ulifunguliwa, lakini mashtaka ya washtakiwa wawili yaliondolewa, na mtu wa tatu akaachiliwa.

Kamati iliona kuwa mashauri ya kimahakama yalirefushwa isivyostahili na yalionekana kutofaa. Kamati iliona kuwa walalamikaji walikuwa waathirika wa ubaguzi wa moja kwa moja na uhalifu wa kikatili dhidi ya watu wenye ualbino. Kamati ilitambua kuwa waathirika wana uwezo mdogo wa kupata haki na kuna kutokuadhibiwa kwa waliowatendea ukatili huo.

Kwa kuzingatia kuwa mamlaka za ndani hazijachukua hatua madhubuti za kuzuia ukatili dhidi ya watu wenye ualbino, Kamati iligundua kuwa Tanzania ilikiuka wajibu wake chini ya Mkataba wa kesi hizo tatu za mwaka 2017, 2018 na 2019 kwa mtiririko huo.

Katika uamuzi wake wa kesi hizo tatu, Kamati iliitaka Tanzania kuwapatia wahanga hao suluhisho madhubuti, ikiwa ni pamoja na fidia na msaada unaohitajika ili kuwawezesha kuishi tena kwa uhuru. Pia ilihimiza chama cha Serikali kufanya uchunguzi usio na upendeleo, wa haraka, na madhubuti wa mashambulizi hayo na kurekebisha hatua za kisheria za kukabiliana na ukatili dhidi ya watu wenye ualbino na usafirishaji haramu wa viungo vyao vya mwili.

"Tunasikitika Tanzania kukosa ushirikiano na Kamati, ikiwa ni pamoja na kushindwa kwake kushiriki katika mazungumzo ili kuhakikisha utekelezaji wa haraka wa mapendekezo yetu na kutoa fidia ya kutosha kwa waathiriwa," Gamio Ríos ameeleza.

Kamati iliamua kusitisha ufuatiliaji wa kesi hizo tatu kwa tathmini ya alama "D", kutokana na kutokuwa na ushirikiano wa Serikali ya Tanzania.