Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC: Watoto 12 waliokuwa wanatumishwa Kivu Kaskazini waokolewa- MONUSCO

MONUSCO na wadau wamefanikisha kuachiwa huru kwa watoto 12 waliokuwa wanashikiliwa na kikundi kilichojihami cha UFDPC huko Kivu Kaskazini nchini DRC kupitia mpango wa PDDRCS.
MONUSCO
MONUSCO na wadau wamefanikisha kuachiwa huru kwa watoto 12 waliokuwa wanashikiliwa na kikundi kilichojihami cha UFDPC huko Kivu Kaskazini nchini DRC kupitia mpango wa PDDRCS.

DRC: Watoto 12 waliokuwa wanatumishwa Kivu Kaskazini waokolewa- MONUSCO

Amani na Usalama

Huko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO umeendelea kuunga mkono juhudi za serikali za kujumuisha kwenye jamii wapiganaji wa zamani, hatua inayofanyika kupitia programa ujumbe huo ya Kupokonya silaha, Kuvunja Makundi na Kujumusha wapiganaji kwenye jamii, PDDRCS.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amewaambia waandishi wa habari mjini New York, Marekani hii leo kuwa kwa kushirikiana na wadau, MONUSCO ilitia saini makubaliano na kikundi kilichojihami kiitwacho Union of Congolese Patriotic Defense Forces au UFDPC, makubaliano yaliyowezesha kuachiliwa huru kwa watoto 12 waliokuwa wanatumikishwa vitani na kundi hilo.

“Kwa sasa watoto hao watapatiwa msaada wa kujumuishwa tena kwenye jamii na vile vile kuunganishwa na familia zao,” amesema Dujarric.

Kupitia mtandao wake wa Twitter, MONUSCO imesema watoto hao walikuwa wanatumikishwa na huko eneo la Nyiragongo, jimboni Kivu Kaskazini.  

Katika hatua nyingine, walinda amani wa Umoja wa Mataifa walipelekwa kuimarisha doria kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani huko mashariki mwa mji wa Djugu, jimboni Ituri, mashariki mwa DRC.

“Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya walinda amani hao kupatiwa ripoti ya kwamba wapiganaji wa kundi la CODECO walikuwa wanajiandaa kushambulia kambi hiyo,” amesema Bwana Dujarric.

Walinda amani pia waliendesha doria sambamba na jeshi la serikali ya DRC, FARDC kwa lengo la kulinda raia huko eneo la Drodro-Maze-Lida, kusini-mashariki mwa Djugu ambako kulikuweko wanamgambo waliojihami.

TAGS: Amani na Usalama, Ituri, Kivu Kaskazini, AFRIKA, DRC, MONUSCO