Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalamu wa haki za binadamu wanalaani jukumu la AI kwa uharibifu unaofanywa na jeshi la Israel Gaza

Gari linaendeshwa kupitia vifusi huko Khan Younis.
© UNOCHA/Themba Linden
Gari linaendeshwa kupitia vifusi huko Khan Younis.

Wataalamu wa haki za binadamu wanalaani jukumu la AI kwa uharibifu unaofanywa na jeshi la Israel Gaza

Amani na Usalama

Wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akirejelea ombi lake la hali ya kujizuia kwa kiwango cha juu zaidi Mashariki ya Kati kufuatia shambulio la ndege zisizo na rubani na kombora la Iran dhidi ya Israeli, wataalam huru wa haki za binadamu wamesema madai ya utumiaji wa kijasusi wa akili mbemba au bandia kwenye maeneo ya Gaza unaofanywa na jeshi la Israeli umesababisha athari zisizo na kifani kwa raia, nyumba na huduma.

Kwa mujibu wa wataalam hao "Miezi sita baada ya mashambulizi ya sasa ya kijeshi, nyumba zaidi na miundombinu ya kiraia kwa asilimia kubwa sasa imeharibiwa huko Gaza, ikilinganishwa na migogoro yoyote ya kumbukumbu," wataalam hao, ambao ni pamoja na Francesca Albanese, Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa juu ya hali ya haki za binadamu katika eneo la Palestina lililokaliwa kwa mabavu tangu 1967.

Katika taarifa yao iliyotolewa leo, wataalam hao wamekadiria kuwa asilimia 60 hadi 70 ya nyumba zote huko Gaza, na hadi asilimia 84 ya nyumba kaskazini mwa Gaza, zimeharibiwa kabisa au zingine kuharibiwa kwa kiasi.

Gari lililosheheni mali na vifaa vya nyumbani linapita kwenye mitaa ya Khan Younis.
© UNOCHA/Themba Linden
Gari lililosheheni mali na vifaa vya nyumbani linapita kwenye mitaa ya Khan Younis.

Nyumba zilizo ufukweni mwa Gaza

"Uharibifu huo wa kimfumo na ulioenea ni uhalifu dhidi ya ubinadamu” wamesisitiza wataalam  hao ambao sio wafanyikazi wa Umoja wa Mataifa na hawalipwi mshahara kwa kazi yao 

Ameyasema hayo kabla ya kutaja kuhusu"uhalifu mwingi wa kivita na mauaji ya kimbari unaodaiwa na Bi. Albanese ndani ya ripoti yake kwa Baraza la Haki za Binadamu.

Wataalam hao wameweka bayana kwamba "Pamoja na maafisa wa umma wa Israel kuungana na wito wa kuwataka Wapalestina kuondoka Gaza, kuirudisha Gaza mikononi mwao ili kujenga tena makazi ya walowezi wa Kiyahudi, na shauku kubwa iliyoonyeshwa na maafisa mashuhuri wa zamani wa serikali ya Marekani kuhusu mali na nyumba za kwenye ufukwe wa Gaza, hakuna shaka kwamba dhamira ya Israel inakwenda mbali zaidi ya malengo ya kushindwa kijeshi kwa Hamas”.

Uharibifu wa Ukanda huo unakadiriwa kuwa dola bilioni 18.5 sawa na asilimia 97 ya uchumi wote wa Gaza na Ukingo wa Magharibi. 

Zaidi ya asilimia 70 ya makadirio haya yanachukua nafasi ya makazi, wakati asilimia 19 nyingine ni gharama ya miundombinu ya kiraia, ikiwa ni pamoja na maji na usafi wa mazingira, umeme na barabara.

"Nyumba zimepotea, na hiyo inaambatana na kumbukumbu, matumaini na matarajio ya Wapalestina na uwezo wao wa kutambua haki nyingine, ikiwa ni pamoja na haki zao za ardhi, chakula, maji, usafi wa mazingira, afya, usalama na faragha hasa wanawake na wasichana, elimu, maendeleo, mazingira mazuri na kujitawala.” 

Picha ya kutoka angani iliyopigwa na ndege zisizo na rubani za majengo yaliyoharibiwa huko Jabalia, kaskazini mwa Gaza.
UNICEF
Picha ya kutoka angani iliyopigwa na ndege zisizo na rubani za majengo yaliyoharibiwa huko Jabalia, kaskazini mwa Gaza.

Kurejea kaskazini

Ndani ya Gaza mwishoni mwa juma, maelfu ya watu waliripotiwa kujaribu kurejea makwao kaskazini mwa eneo hilo.

Picha kutoka Gaza zilionyesha watu wa rika zote wakisongamana kando ya barabara ya pwani kuelekea kaskazini, wengi kwa miguu, wengine kwenye mikokoteni ya punda.

Kwa mujibu wa duru za habari, vifaru vya Israel vilifunga barabara na kuwalazimu Wapalestina kugeuka.

Ripoti nyingine zilionyesha kuwa mashambulizi ya Israel yaliendelea siku ya Jumatatu kote Ukanda wa Gaza, huku kambi ya wakimbizi ya Nuseirat katikati mwa Gaza nayo ikipigwa, na kusababisha vifo vya watu watano na makumi kadhaa kujeruhiwa.

Takwimu za hivi karibuni kutoka kwa mamlaka ya afya ya Gaza zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 33,200 wameuawa katika eneo hilo tangu Oktoba 7, wengi wao wakiwa wanawake na watoto. 

Mashambulizi yaliyoongozwa na Hamas nchini Israel yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 1,250 huku zaidi ya 250 wakichukuliwa mateka.

Duka la mikate mkombozi wa maisha  

Katika tukio linalohusiana na hilo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP, limetangaza Jumapili kwamba limesaidia kuanzisha upya uzalishaji wa mikate katika Jiji la Gaza, baada ya kutoa mafuta na ukarabati wa mashine za kuoka katika duka la mikate.

Kabla ya mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel kuanza ili kujibu mashambulizi ya kigaidi yaliyoongozwa na Hamas tarehe 7 Oktoba nchini Israel, Ukanda wa Gaza ulikuwa na viwanda 140 vya kuoka mikate.

Katika ujumbe wake kupitia ukurasa wa X,  zamani Twitter WFP, imesema kuwa imepeleka mafuta kwenye duka moja la kuoka mikate ambalo lilikuwa limefungwa kwa miezi kadhaa, na hivyo kuchangia hali mbaya ya kibinadamu kaskazini mwa eneo hilo, ambapo watu wa Gaza wamekatiliwa mbali na misaada.

"WFP itaendelea kutoa unga wa na rasilimali nyingine ili mikate ipatikane, lakini kiasi hiki kitadumu kwa siku nne tu," shirika la Umoja wa Mataifa lilisema, katika ombi lililotolewa upya la "upatikanaji salama, endelevu na ulioongezwa ili kuzuia njaa.”

Wapalestina wengi sasa wanaishi katika makazi katika mazingira machafu kwa sababu nyumba zao ziliharibiwa.
© UNDP/Abed Zagout
Wapalestina wengi sasa wanaishi katika makazi katika mazingira machafu kwa sababu nyumba zao ziliharibiwa.

Hali ua sintofahamu Rafah 

Na huku kukiwa na hali ya sintofahamu kuhusu iwapo vikosi vya Israel vinaweza kushambulia Rafah, mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, Filippo Grandi ameonya dhidi ya kuanzisha mgogoro mpya wa watu waliokimbia makazi yao kutoka mji wa kusini mwa eneo hilo hadi nchi jirani ya Misri.

"Mgogoro mwingine wa wakimbizi kutoka Gaza kwenda Misri ninaweza kukuhakikishia kwamba ku kuwa niliwahi kuwa mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA, mwenyewe nazungumza kutokana na uzoefu hii itafanya utatuzi wa swali la wakimbizi wa Palestina na kama matokeo ya mzozo wa Israeli na Palestina kuwa haiwezekani," 

Ameendelea kuongeza kuwa "Kwa hivyo lazima tufanye kila kitu kinachowezekana ili hili lisitokee. Na hii ndiyo sababu mara kwa mara tumekuwa tukisema kipaumbele ni kupata fursa ya ufikiaji ndani ya Gaza, kwa sababu hiyo ndiyo njia pekee ambayo tunaweza kuzuia hili kutokea."