Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Malawi: Hali ya chakula ni tete, WFP yaomba jamii ya kimataifa ichukue hatua

Nchini Malawi, mwanamke anapokea mgao wake wa kila mwezi wa nafaka.
WFP/Gregory Barrow
Nchini Malawi, mwanamke anapokea mgao wake wa kila mwezi wa nafaka.

Malawi: Hali ya chakula ni tete, WFP yaomba jamii ya kimataifa ichukue hatua

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP linatoa wito wa upelekaji wa haraka wa misaada ya chakula kwa ajili ya kuokoa maisha kwa watu milioni mbili wanaokabiliwa na njaa iliyochochewa na ukame. Ukame umesababishwa na hali ya El Niño.

El Nino ni mwenendo wa tabianchi unaoambatana na maji ya baharí kuwa ya joto kuliko kawaida kwenye maeneo ya mashariki mwa bahari ya Pasifiki na kusambaa maeneo mengine ya dunia. 

Taarifa ya WFP iliyotolewa Lilongwe, mji mkuu wa Malawi inasema ombi hilo linakuja siku chache baada ya Rais wa Malawi Lazarus Chakwera kutangaza hali ya dharura. 

Hali halisi Malawi, bei ya mahindi yaongezeka maradufu

Madhara ya El Niño yanaripotiwa kuongeza janga la tabianchi Malawi, taifa la kusini mwa Afrika ambalo limekuwa likiathiriwa na vimbunga vya kitropiki tangu mwaka 2022 hadi 2023 na hivyo kutumbukiza asilimia 40 ya wananchi wa Malawi kwenye njaa na kupoteza mbinu zao za kujipatia kipato.

Ukame wa muda mrefu umeharibu mazao kwenye mikoa ya kusini na kati mwa Malawi, ilhali mafuriko yamesomba mazao kwenye maeneo ya Kaskazini na Kati mwa Malawi.

Hifadhi ya mahindi katika ghala la taifa inazidi kupungua na hivyo Malawi imelazimika kuagiza kutoka nje chakula hicho kinachotegemewa zaidi nchini humo.

“Bei ya mahindi imeongezeka takribani maradufu katika kipindi cha mwaka mmoja na mara tatu kwa wastani wa miaka mitano. Asilimia 80 ya wananchi wakitegemea kilimo ili kukidhi mahitaji yao ya msingi, kupungua kwa mazao tegemezi kama vile mahindi, mchele, maharage ya soya, mbaazi na karanga  kumewaweka mamilioni ya watu katika hali mbaya,” imesema WFP.

WFP inafanya nini?

Akizungumzia athari hasi za hali hiyo, Mkurugenzi Mkazi wa WFP nchini Malawi Paul Turnbull, amesema jamii ya kimataifa inaweza kuepusha baa la njaa kwa familia zilizoathiriwa zaidi, lakini muda unayoyoma. “Natoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua zaidi na kutusaidia kuokoa maisha.”

Tarehe 23 mwezi Machi, Rais Chakwera alitangaza hali ya dharura kwenye wilaya 23 kati ya 28 za Malawi ambazo zimeathiriwa na hali ya El Niño.

Tathmini ya awali ya serikali inaonesha kuwa takribani kaya milioni mbili za wakulima na ekari 749,000, zikiwasilisha asilimia 44 za eneo la kilimo la Malawi zimeathiriwa.

Matokeo yake, msimu wa mwambo wa mwaka 2024/2025 unatarajiwa kufika haraka kuliko ilivyozoeleka.

WFP inasema itasaidia sehemu ya mahitaji na inahitaji dola milioni 70 kufikisha misaada ya chakula kwa watu milioni mbili kwa kipindi cha miezi mitatu, msaada ambao ni vyakula na vile vile fedha taslimu.