Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC: MONUSCO yapatia wanajeshi 30 wa FARDC mbinu za kukabili waasi msituni

Hapa ni Beni, jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Brazil wanaohudumu kikosi cha kujibu mashambulizi FIB cha MONUSCO wakipatia mafunzo wanajeshi 30 kutoka jeshi la serikali, FARDC j…
MONUSCO/Ado Abdou
Hapa ni Beni, jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Brazil wanaohudumu kikosi cha kujibu mashambulizi FIB cha MONUSCO wakipatia mafunzo wanajeshi 30 kutoka jeshi la serikali, FARDC juu ya mbinu za kupambana msituni.

DRC: MONUSCO yapatia wanajeshi 30 wa FARDC mbinu za kukabili waasi msituni

Amani na Usalama

Siku zikizidi kuhesabiwa kwa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO, kuondoka nchini humo, ujumbe huo unaendelea kutekeleza wajibu wake wa kujengea uwezo jeshi la serikali, FARDC kuweza kukabili vikundi vilivyojihami ambavyo vinatajwa kuhusika na asilimia 65 ya matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini humo mwezi Februari mwaka huu, kwa mujibu wa ripoti ya pamoja ya Umoja wa Mataifa na serikali. 

Video ya MONUSCO inaonesha wanajeshi hao 30 wakiwa kwenye uwanja wa mafunzo hayo ya kulenga shabaha ambapo kuna karatasi lililochorwa binadamu na sasa wanatakiwa kulenga maeneo mbali mbali ya mwili yaliyowekwa alama.

Ni mbinu wanazopatiwa na walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Brazil, hapa Beni jimboni Kivu Kaskazini ili waweze kukabiliana na waasi kwenye maeneo misituni.

Mbinu hizo za medani ni mpya kwa wanajeshi wetu- FARDC

 Kapteni Rombaut Mukoka ni Afisa wa jeshi la FARDC na anasema,“mafunzo haya ni muhimu sana. Yanapaswa kuendelea ili hatimaye wanajeshi wetu waweze kunufaika. Hizi mbinu walizojifunza ni mpya sana kwetu na zinatambulika katika medani za kimataifa.”

Mafunzo ya kulenga shabaha yanaendelea na kisha mkufunzi kutoka Brazil anajongea kwenye picha ile akiwa na mmoja wa wanafunzi ili kuonesha ni wapi haswa wanapaswa kulenga. 

Hapa ni Beni, jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Brazil wanaohudumu kikosi cha kujibu mashambulizi FIB cha MONUSCO wakipatia mafunzo wanajeshi 30 kutoka jeshi la serikali, FARDC j…
MONUSCO/Ado Abdou
Hapa ni Beni, jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Brazil wanaohudumu kikosi cha kujibu mashambulizi FIB cha MONUSCO wakipatia mafunzo wanajeshi 30 kutoka jeshi la serikali, FARDC juu ya mbinu za kupambana msituni.

Mbinu zitawawezesha kupigana msituni na waasi- MONUSCO

Jenerali Luciano Alfred Matamba ni Mkuu wa kikosi cha kujibu mashambulizi, FIB cha MONUSCO mjini Beni na anafafanua lengo la mafunzo hayo yaliyofanyika kwa wiki tatu akisema “lengo la mafunzo haya ni kuwapatia mbinu na ufundi za kuendesha operesheni msituni. Kama unavyofahamu hapa Kivu Kaskazini tuko kwenye eneo la operesheni ambalo kwa kiasi kikubwa ni pori.”

Amesema mashambulizi yanayofanywa na waasi wa ADF yanahitaji mtu kuwa na hizo mbinu za kupigana msituni. 

Hivyo anasema “FARDC ni wadau wetu ambao tunapaswa kushirikiana nao kwa mujibu wa azimio la Umoja wa Mataifa namba 2717. Ni pale tu ambapo tutajifunza pamoja na kuwa na mbinu sawa ndio tutaweza kutatua matatizo yaliyoko hapa.”

Azimio la kuondoka kwa MONUSCO nchini DRC

Tarehe 20 mwezi Desemba mwaka jana Baraza la Usalama la Umoja wa Matafa lilipitisha azimio la kuongeza muda wa MONUSCO hadi tarehe 20 Desemba mwaka huu wa 2024, muda ambao ndio mwisho wa kuweko kwa ujumbe huo uliokuweko nchini humo tangu mwaka 2000.

Azimio linatambua mpango wa kina wa awamu tatu uliowasilishwa kwa Baraza la Usalama na serikali ya DRC na Umoja wa Mataifa kwa mujibu wa nyaraka namba S/PRST/2023/5, na inatambua mpango wa MONUSCO wa kuanza kuondoa vikosi vyake jimboni Kivu Kusini ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2023 na kitakuwa kimekamilika kuondoka eneo hilo mwishoni mwa Aprili 2024.

Pamoja na kutakiwa kuondoka, MONUSCO ina wajibu wa kujengea uwezo vikosi vya jeshi na polisi ili viweze kubeba jukumu la ulinzi na usalama baada ya ujumbe huo kukamilisha majukumu yake.