Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Machafuko Gaza: Makumi ya watoto waripotiwa kuuawa katika usiku mmoja

Mtoto mdogo wa Kipalestina mwenye mguu uliokatwa ameketi kwenye kiti katika hospitali ya uwanja huko Gaza, akiwa amevaa kifaa cha matibabu kwenye kiungo chake kilichobaki. Mtoto mwingine aliyejeruhiwa anakaa kitandani nyuma.
© WHO/Christopher Black Watoto wanatibiwa katika hospitali ya muda huko Mouraj, kitongoji kilichoko kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Machafuko Gaza: Makumi ya watoto waripotiwa kuuawa katika usiku mmoja

Msaada wa Kibinadamu

Wakati uhasama mkali huko Gaza ukiendelea kati ya wapiganaji wa Hamas na vikosi vya Israeli, mashirika ya Umoja wa Mataifa ya misaada ya kibinadamu yamesema "makumi ya watoto wameuawa usiku mmoja" na vizuizi vinavyoendelea vya utoaji wa misaada vinachangia uwepo wa hali inayokaribiana na uwepo wa baaa la njaa.

Kuendelea kwa ghasia hizo kumekuja licha ya wito wa kusitishwa mapigano mara moja kwa muda uliosalia wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kutoka kwa Baraza la Usalama siku ya Jumatatu, na kufuatia ombi la haraka kutoka kwa mashirika ya misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa kutaka azimio hilo liheshimiwe mara moja, ili kuzuia watu wengi zaidi kufa.

Akizungumza kutoka Rafah kusini mwa Gaza, msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF James Elder amesema kwa mujibu wa mamalaka ya afya ya Gaza, watoto 13,750 mpaka sasa wameuawa huku kukiwa na mashambulizi ya anga na mabomu yaliyofanywa na Israel kujibu mashambulizi yanayoongozwa na Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba, 2023.

Akitoa ripoti za "makumi ya watoto waliouawa usiku kucha", Elder alibainisha kuwa hii imetokea "saa chache tu baada ya azimio la (Baraza la Usalama) kupitishwa".

Khan Younis imesambaratishwa

Mji wa kusini mwa Gaza wa Khan Younis "haupo tena", msemaji wa UNICEF aliongeza, kabla ya kuelezea "maangamizi makubwa" ya mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel ambayo yameacha idadi isiyoripotiwa ya watoto na familia kuzikwa chini ya vifusi vya nyumba zao.

"Katika miaka yangu 20 ya kufanya kazi Umoja wa Mataifa sijawahi kuona uharibifu kama huu, ni machafuko tu, uharibifu, uchafu na vifusi kila upande, kila mahali ninapotazama," alisema, akiripoti juu safari yake ya hivi karibuni kaskazini mwa Gaza.

Hospitali ya Nasser huko Khan Younis - "mahali pa uhitaji sana kwa watoto walio na majeraha ya vita" - sasa haifanyi kazi tena, afisa huyo wa UNICEF aliripoti, akiongeza kuwa ni theluthi moja tu ya hospitali za Gaza "zinafanya kazi kwa kiasi" sasa. 

WFP wafanikiwa kufikisha misaada kaskazini mwa Gaza

Katika eneo la mbali la Kaskazini, ambapo Shirika La umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP limefanikiwa kufikisha malori 96 yaliyokuwa yamebeba vifaa vya msaada siku ya Jumatatu - kwa mara ya kwanza katika muda wa siku tano – Bwana Elder alielezea kuona watu wakitoa "ishara inayofahamika ulimwenguni ya mkono kuupeleka kwenye mdomo, wakimaanisha wanaomba sana na wanatafuta chakula”.

Hii ni pamoja na ukweli kwamba mamia ya malori yenye misaada ya kibinadamu ya kuokoa maisha yamesalia kwenye mpaka wa Misri, mashirika ya Umoja wa Mataifa yamedokeza.

Akinukuu uchanganuzi wa ukosefu wa chakula uliochapishwa hivi karibuni ukionya juu ya "eneo hilo la Gaza kushuka kwa kasi kuelekea kwenye  janga la ", afisa huyo wa UNICEF pia alibainisha kuwa takwimu za shirika hilo zilionesha kuwa mtoto mmoja kati ya watatu walio chini ya umri wa miaka miwili sasa wanakabiliwa na utapiamlo mkali. Kabla ya mzozo huo, chini ya mtoto mmoja kati ya 100 chini ya miaka mitano walikuwa na utapiamlo, Elder alisema.

"Hii inazungumzia kunyimwa kabisa, hii inazungumzia uharibifu wa vitu ambavyo watoto wanategemea - maji na mifumo ya afya - lakini pia inazungumzia kile idadi inazungumzia, ambayo ni ukosefu mbaya wa chakula na lishe, misaada bado haifiki kaskazini.”

Kabla ya vita, karibu malori 500 yaliyo sheheni bidhaa za kibiashara na za kibinadamu yalifika katika eneo hilo kila siku, lakini wastani leo ni karibu theluthi moja ya idadi hiyo lakini pia kumekuwa na vipindi vya "wiki ambapo hakuna kitu kilichoingia kaskazini", afisa wa UNICEF aliongeza.

Mgogoro wa kiafya

Akeleza wasiwasi mkubwa kuhusu matukio ya kukatisha tamaa yanayoendelea Gaza, msemaji wa Shirika Umoja wa Mataifa la Afya Duniani WHO Tarik Jazarevic aliripoti kwamba wagonjwa wengi katika hospitali ya Al Amal kusini sasa wameondoka kwenye kituo hicho.

Ripoti za vyombo vya habari zilionesha kuwa agizo la kuhamishwa kwa kituo hicho lilitolewa na jeshi la Israeli, huku kukiwa na uhasama mkali magharibi mwa Khan Younis. 

Hali pia inaaminika kuwa mbaya katika Hospitali ya Al Shifa ya kaskazini mwa Gaza ambayo pia ililengwa na uvamizi wa kijeshi wa Israel, lakini WHO haina uwezo wa kufika huko, Bw. Jasarevic alisema.

"Una wafanyakazi wa afya wanaokufa, una hospitali ambazo zimezingirwa, una watu ambao wanatafuta makazi katika maeneo haya na ikiwa huwezi kupata makazi hospitalini unaweza kwenda wapi?" aliwaambia waandishi wa habari mjini Geneva.

Ripoti za vyombo vya habari zilionesha mashambulizi ya anga usiku wa kuamkia leo Jumanne karibu na mji wa kusini kabisa wa Rafah ambapo takriban watu milioni 1.5 sasa wanajihifadhi huko, wengi wao baada ya kuhamishwa kutoka kwa makazi yao mahali pengine kwenye eneo hilo.

Israel ondoeni marufuku ya UNRWA kupeleka misaada kaskazini

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada, OCHA, pia limeitaka Israel kuondoa marufuku yake kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la kusaidia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA kupeleka misaada kaskazini mwa Gaza ikirejelea wito wa awali wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.

"Tunahitaji kuondoa dhana ya kwamba jukumu lao la kupata misaada kwa namna fulani linasimama kwa kupata lori chache – sehemu kidogo sana ya kile kinachohitajika - kuvuka mpaka na mara tu itakapofika kama nilivyoona ilivyoripotiwa, basi sio shida yetu tena, ni tatizo la mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa. Hiyo si sahihi.”

Aliongeza: "Huwezi kudai kufuata masharti haya ya sheria ya kimataifa unapozuia misafara ya chakula ya UNRWA, wakati wiki iliyopita ulikataa misheni tano kwenda kaskazini, wakati sasa tuna ripoti za mashambulio ya Israeli kwenye maghala na polisi ambao wanapaswa kusaidia kulinda misaada ndani ya Gaza."