Shambulizi dhidi ya walinda amani DRC, UN yalaani
Shambulizi dhidi ya walinda amani DRC, UN yalaani
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amelaani shambulizi ambalo limetokea jana Jumamosi Machi 16 na kujeruhi wanajeshi wanane wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, wakati wa mapigano kati ya waasi wenye nguvu wa M23 na wanajeshi wa Serikali.
Tukio hilo limetokea katika eneo la Sake, kilomita 20 tu kutoka Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini.
Walinda amani waliojeruhiwa, ambao walikuwa sehemu ya Operesheni Springbok iliyoanzishwa Novemba mwaka jana kulinda raia katika eneo hilo, wamepata majeraha huku mapigano yakiendelea, ambapo wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wamekuwa wakisaidia vikosi vya Serikali ili kuwalinda raia walio hatarini.
Katika taarifa yenye maneno makali iliyotolewa na Msemaji wake usiku wa kuamkia lewo Jumapili, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amelaani shambulizi hilo akisisitiza kuwa linaweza kuwa uhalifu wa kivita chini ya sheria za kimataifa.
Amewatakia kupona haraka walinda amani waliojeruhiwa, akisisitiza wito kwa makundi yote yenye silaha, wapiganaji wa DRC na wa kigeni kusitisha mara moja uhasama na kushiriki katika mchakato wa kupokonya silaha.
Zaidi ya hayo, mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza ulazima wa M23 kujiondoa kabisa katika eneo ililokalia na kuendana na makubaliano yaliyoainishwa katika taarifa ya Luanda ya Novemba 2022, ili kutetea uhuru na uadilifu wa eneo la DRC.
Bintou Keita, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC na mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo (MONUSCO) naye amelaani mashambulizi hayo.
Bi. Keita amesema mmoja wa walinda waliojeruhiwa amepata majeraha makubwa na wote wamehamishwa kwa ajili ya matibabu yanayofaa.
Walinda amani hao walikuwa wametumwa kwa wiki kadhaa kama sehemu ya Operesheni Springbok katika eneo lisilo na utulivu la Kivu Kaskazini, wakifanya kazi kwa pamoja na wanajeshi wa Serikali katika operesheni za kijeshi. Bi. Keita amethibitisha kujitolea kwa MONUSCO kusaidia uchunguzi kwa matumaini ya kuwafikisha waliohusika mbele ya sheria.
Katibu Mkuu na Mwakilishi wake Maalum wamesisitiza azimio la MONUSCO la kutekeleza zaidi jukumu lake la ulinzi wa raia kutoka kwa Baraza la Usalama na kufanya kazi pamoja na vikosi vya ulinzi na usalama vya DRC kuimarisha doria za pamoja na za upande mmoja ili kulinda raia.