Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNRWA yazindua kampeni ya Zaka ili kusaidia raia Gaza

Watoto wa Kipalestina wa Ukanda wa Gaza wakiwa na taa kusherehekea mwezi tukufu wa Ramadhani.
© UNRWA Watoto wa Kipalestina wa Ukanda wa Gaza wakiwa na taa kusherehekea mwezi tukufu wa Ramadhani.

UNRWA yazindua kampeni ya Zaka ili kusaidia raia Gaza

Msaada wa Kibinadamu

Kampeni ya kila mwaka ya utoaji zaka inayoendeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA, imezinduliwa hii leo kwa lengo la kuwezesha shirika hilo kusambaza misaada ya dharura inayohitajika kwenye eneo lililozingirwa na Israeli huko Ukanda wa Gaza.

Taarifa ya  UNRWA iliyotolewa leo mjini Aman, Jordan inasema kampeni hiyo iliyopatiwa jina Kampeni ya Ramadhanii ambayo huendeshwa wakati wa mfungo wa mwezi mtufuku wa Ramadhani, itaendelea hadi mwisho wa mfungo na asilimia 100 ya zaka itakayopatikana itaelekezwa moja kwa moja kwa wakimbizi wa ndani Ukanda wa Gaza. 

Halikadhalika michango ya zaka itakwenda pia kwa wakimbizi wa kipalestina wanaokidhi vigezo ambao wanaishi kwenye maeneo mengine kwenye ukanda wa Mashariki ya Kati ambapo watapatiwa chaklua cha msaada na fedha taslimu. 

Hali halisi Gaza

Kampeni hii ya Zaka inakuja wakati zaidi ya wapalestina 30,000 wameuawa Gaza tangu mapigano yaanze tarehe 7 Oktoba 2023. Njaa imefikia kiwango cha juu ambapo zaidi ya asilimia 90 ya wakazi wa eneo hilo hawana uhakika wa chakula. 

Wazazi wanalisha watoto wao vyakula vya Wanyama na mimea ya porini hali inayochochea uwezekano wa utapiamlo na ukosefu wa lishe. 

Likiwa ndio shirika kubwa zaidi la misaada linaloendesha shughuli huko  Gaza, UNRWA iko kwenye nafasi ya kupokea, kusafirisha na kusambaza misaada kwa wakimbizi wa ndani wa kipalestina zaidi ya milioni 1.7  kwenye ukanda huo na maeneo mengine manne ya Mashariki ya Kati. 

“Watu wa Gaza na wakimbizi wa kipalestina kwenye ukanda wa Mashariki ya Kati wameanza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani huku kukiwa na janga la kibinadamu Gaza, ongezeko la ghasia Ukingo wa Magharibi, na changamoto kubwa za kiuchumi Lebanon, Syria, na Jordan. Msaada wako unahitajika ili kusaidia UNRWA kusambaza misaada ya kibinadamu inayohitajika na huduma muhimu. Asilimia 100 ya mchango wako utafikia wahitaji. Changia kwa ukarimu na tunashukuru kwa msaada wako,” amesema Philippe Lazzarini, Kamishna Mkuu wa UNRWA. 

Kuchangia Zaka yako hii leo bofya hapa

UNRWA inasema mpango wa Zaka unaendana sheria ya kiislamu ambapo hakuna makato yoyote ya fedha inayochangiwa kama Zaka. Fedha zinaingizwa moja kwa moja kwenye akaunti iliyoko Benki ya Kiislamu ya Safwa.

Kampeni hii inakuja wakati UNRWA inakabiliwa na ukata kufuatia baadhi ya wafadhili wake kusitisha michango kutokana na tuhuma ya kwamba baadhi ya wafanyakazi wake walishiriki katika mashambulizi ya tarehe 7 Oktoba mwaka 2023 yaliyofanywa na wanamgambo wa Hamas dhidi  ya Israel.