Hali ya walioyakimbia makazi yao Msumbiji iangaliwe upya
Hali ya walioyakimbia makazi yao Msumbiji iangaliwe upya
Jumuiya ya kimataifa inapaswa kujitolea upya katika kutafuta suluhu kwa watu waliokimbia makazi yao nchini Msumbiji, Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Filippo Grandi, na Mshauri Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Suluhu za Wakimbizi wa Ndani, Robert Piper, leo Machi 8 wametoa wito.
Msumbiji imekabiliwa na changamoto kubwa zinazohusiana na ghasia kutoka kwa vikundi visivyo vya serikali tangu mwaka 2017 pamoja na athari mbaya za dharura ya tabianchi, na matokeo yake zaidi ya watu milioni 1.2 wamekuwa wakimbizi wa ndani.
Serikali imefanya maendeleo muhimu kusaidia waliofurushwa nchini Msumbiji huku ikijitahidi kushughulikia sababu za kukimbia kwao. Zaidi ya watu 600,000 wamerejea katika maeneo yao ya asili - wengi wao mnamo 2023 - lakini changamoto bado. Wengi bado hawana huduma za msingi na hali ya kutosha ya maisha, imeeleza taarifa ya UNHCR iliyotolewa leo Machi 8 mjini Geneva Uswisi.
Katika ziara ya pamoja nchini humo, viongozi hao walisisitiza dhamira yao ya kufanya kazi na Serikali na wadau wengine ili kuimarisha suluhu kwa waliokimbia makazi yao nchini Msumbiji.
Msumbiji ni nchi ya majaribio chini ya Ajenda ya Utekelezaji ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi wa ndani, juhudi za kurekebisha jinsi mfumo wa Umoja wa Mataifa unavyokabiliana na watu waliokimbia makazi yao kwa muda mrefu, kupitia njia zinazoongozwa na Serikali, zinazozingatia maendeleo kwa ufumbuzi wa muda mrefu kwa wakimbizi wa ndani.
"Msumbiji kwa ujasiri inatayarisha njia ya ufumbuzi wa muda mrefu kwa maelfu ya familia zilizofurushwa, licha ya utata wa mazingira ambapo vurugu na maafa husababisha watu kuhama, mara nyingi katika jamii ambazo tayari zimeathirika," Piper anasema na kuongeza, "Ninawaomba washirika wote wa kimataifa kuunga mkono juhudi hizi ili mafanikio yaliyopatikana hadi sasa yasipotee."
Piper na Grandi walikutana na Rais Filipe Jacinto Nyusi, na maafisa wakuu wa serikali huko Maputo kabla ya kutembelea jamii zilizofurushwa huko Cabo Delgado, ambapo kumekuwa na mashambulio mapya ya hivi karibuni kutoka kwa vikundi visivyo vya serikali na kusababisha watu kutakimbia makazi yao.
Pia Grandi na Piper walikutana na wakimbizi wa ndani na mamlaka za mitaa katika wilaya za Pemba na Mueda, kuchunguza makazi ya mpito, mipango ya ulinzi na vituo vya jamii na kukutana na wajasiriamali wanawake waliopatiwa mafunzo ya usimamizi wa biashara. Pia walitembelea programu ya maendeleo na kukutana na waliorejea Mocimboa da Praia.
IOM
Wakati huo huo Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) limetoa takwimu kwamba nchini humo Msumbiji zaidi ya watu 110,000 wameyakimbia makazi yao tangu mwishoni mwa mwaka jana (Desemba 22) kutokana na kuzuka upya kwa mashambulizi ya makundi yenye silaha yasiyo ya serikali katika hali mbaya ya kuongezeka kwa ghasia katika Mkoa wa Cabo Delgado. Idadi hii ya kutisha inawakilisha wimbi la pili kwa ukubwa la watu waliokimbia makazi yao huko Cabo Delgado tangu kuanza kwa mzozo mnamo 2017, ikisisitiza kuongezeka kwa mzozo wa kibinadamu katika eneo hilo.
Taarifa ya IOM iliyotolewa leo Geneva-Uswisi na Maputo-Msumbuji inaesema ghasia hizo zimeweka ongezeko la kutisha, huku jamii zilizoathirika zikibeba mzigo mkubwa wa mashambulizi haya yasiyokoma.
Kushughulikia dharura hii ya kibinadamu, IOM imekuwa mstari wa mbele, kutoa misaada muhimu kwa zaidi ya watu 22,000 waliokimbia makazi hivi karibuni. Mtazamo wa shirika wenye nyanja nyingi unajumuisha kudhibiti maeneo ya watu waliofurushwa, kusambaza makazi, huduma za afya, usaidizi wa afya ya akili, na kuratibu mwitikio wa pande nyingi ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka. Licha ya juhudi hizi, ukubwa wa mgogoro unaendelea kushinda rasilimali zilizopo, na kuonesha pengo ambalo linahitaji kutatuliwa kwa haraka.