Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwakilishi Maalum wa UN: Kuna 'Taarifa za wazi na zenye kushawishi' kwamba mateka wanaoshikiliwa Gaza walifanyiwa ukatili wa kingono

Pramila Patten, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ukatili wa Kingono kwenye mizozo, akihutubia waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York.
UN Photo/Mark Garten
Pramila Patten, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ukatili wa Kingono kwenye mizozo, akihutubia waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York.

Mwakilishi Maalum wa UN: Kuna 'Taarifa za wazi na zenye kushawishi' kwamba mateka wanaoshikiliwa Gaza walifanyiwa ukatili wa kingono

Wanawake

Kufuatia ziara ya siku 17 nchini Israel, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ukatili wa Kingono kwenye mizozo Pramila Patten ameripoti hii leo kwamba yeye na timu ya wataalam wamekuta "taarifa za wazi na za kushawishi" za ubakaji, na mateso ya kijinsia yaliyofanywa dhidi ya mateka waliokamatwa wakati wa mashambulio ya kigaidi ya Oktoba 7, 2023 huko Israel.

Katika taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu ripoti hiyo Bi. Patten ameeleza pia kuna sababu za kuridhisha za kuamini kwamba ghasia hizo, ambazo ni pamoja na "matendo mengine ya kikatili, ya kinyama na ya kudhalilisha", zinaweza kuwa zinaendelea dhidi ya wateka wanashikiliwa na Hamas na watu wengine wenye msimamo mkali huko katika Ukanda wa Gaza.

Ripoti kutoka Ofisi yake, ilitokana na ziara rasmi nchini Israel kwa mwaliko wa Serikali, ambayo ni ilihusisha pia kutembelea Ukingo wa Magharibi, kati ya tarehe 29 Januari na 14 Februari 2024.

Katika muktadha wa shambulio lililoratibiwa la Hamas na wengine la tarehe 7 Oktoba, timu ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa iligundua kuwa kuna misingi ya kuridhisha na kuamini kwamba unyanyasaji wa kingono unaohusiana na migogoro ulitokea katika maeneo mengi, ikiwa ni pamoja na ubakaji na ubakaji wa kundi la watu wengi katika angalau maeneo matatu kusini mwa nchi Israeli.

Timu pia ilipata mwelekeo wa waathirika, wengi wao wakiwa wanawake, waliopatikana wakiwa hawajavaa nguo, au kiasi hawakuwa na nguo, wakiwa wamefungwa na kupigwa risasi katika maeneo mengi ambayo "inaweza kuwa dalili ya aina fulani za unyanyasaji wa kijinsia".

Katika baadhi ya maeneo, tume hiyo ilisema haikuweza kuthibitisha matukio yaliyoripotiwa ya ubakaji.

Kiwango kamili hakiwezi kujulikana kamwe

Timu ya Umoja wa Mataifa imetoa maoni yake kwamba kiwango cha kweli cha unyanyasaji wa kijinsia uliofanywa wakati wa mashambulizi ya Oktoba 7 na matokeo yake, inaweza "kuchukua miezi au miaka kuibuka na inaweza kamwe kutojulikana kikamilifu", kulingana na taarifa kwa vyombo vya habari.

Ujumbe huo unaojumuisha Bi. Patten na wataalam tisa - ambao haukuwa wa uchunguzi - ulifanya mikutano 33 na wawakilishi wa Israeli, kuchunguza zaidi ya picha 5,000 za video za saa 50. walifanya mahojiano 34 ya siri ikiwa ni pamoja na walionusurika na mashahidi wa shambulio la Oktoba 7, walioachiliwa mateka, wahojiwa wa kwanza na wengine.

Ripoti hiyo inasema kuwa mamlaka za Israel zimekabiliwa na changamoto nyingi katika kukusanya ushahidi.

Madai yanayohusisha vikosi vya usalama vya Israel na walowezi

Timu hiyo pia ilitembelea eneo la Ramallah katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, ili kusikiliza maoni na wasiwasi wa maafisa na wawakilishi wa mashirika ya kiraia tangu tarehe 7 Oktoba, ambayo inadaiwa kuhusisha vikosi vya usalama vya Israel na walowezi.

Bi. Patten alisikia wasiwasi ulioibuliwa nao kuhusu ukatili, unyama na udhalilishaji wa Wapalestina waliowekwa kizuizini, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kingono kwa njia ya upekuzi wa kivamizi, vitisho vya ubakaji na kuachwa bila nguo kwa kulazimishwa kwa muda mrefu.Taarifa zilizokusanywa zitakamilisha zile ambazo tayari zimekusanywa na maafisa wengine wa Umoja wa Mataifa kuhusu madai ya unyanyasaji wa kingono unaohusiana na migogoro ndani ya Gaza, kwa uwezekano wa kujumuishwa katika ripoti ya mwaka ya Katibu Mkuu kuhusu suala hilo.

Mapendekezo ya awali

Mapendekezo ya Bi. Patten yanajumuisha wito kwa Serikali ya Israel kutoa idhini kamili kwa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR) na Tume huru ya Uchunguzi iliyopewa mamlaka na Baraza la Haki za Kibinadamu kuhusu eneo linalokaliwa kwa mabavu la Wapalestina, “kufanya uchunguzi huru kamili kuhusu mambo yote ya madai ya ukiukaji”.

Alitoa wito kwa Hamas kuwaachilia mara moja na bila masharti wale wote wanaoshikiliwa kama mateka na kuhakikisha ulinzi wao, ikiwa ni pamoja na ulinzi dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia.

Bi. Patten pia alitoa wito kwa vyombo vyote vinavyohusika na vyenye uwezo kuwafikisha wahusika wote wa unyanyasaji wa kijinsia mbele ya sheria, na ofisi yake itatoa msaada kamili ili kuimarisha juhudi za kitaifa.

Pia alitoa wito wa viwango vya juu zaidi vya uadilifu wa taarifa katika kuripoti na kushughulikia kesi za unyanyasaji wa kijinsia, kama taarifa ya vyombo vya habari inavyosema, "kutokana na hatari za maneno ya uchochezi na vichwa vya habari vya kusisimua na kuongezeka kwa mivutano" pamoja na vyombo vya habari au shinikizo la kisiasa ambalo litazidisha kiwewe na unyanyapaa wa waathirika.

Mwakilishi huyo Maalum aliunga mkono wito wa Katibu Mkuu wa kusitishwa kwa mapigano kwa sababu za kibinadamu na akahimiza makubaliano yoyote ya kusitisha mapigano kutambua umuhimu wa kutambua unyanyasaji wa kijinsia kama suala kuu, na kuruhusu jamii zilizoathirika kusikilizwa.

Alieleza kuwaonea huruma na mshikamano wake na raia wote walioathiriwa na "vurugu za kikatili katika eneo" tangu 7 Oktoba.

Tazama mkutano wa waandishi wa habari wa Bi. Pramila Patten akitangaza matokeo ya timu yake katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani hapa chini: (Taarifa hii ilirushwa mubashara unaweza kutazama kuanzia dakika 16:55 anapoanza kuzungumza)

Link: live video from UNWEB TV: https://webtv.un.org/en/asset/k1w/k1wee1dcdl