Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanasiasa acheni kueneza chuki mnaposaka wafuasi – Türk

Kamishna Mkuu Volker Türk akihutubia kikao cha 55 cha Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa.
UN News/Anton Uspensky
Kamishna Mkuu Volker Türk akihutubia kikao cha 55 cha Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa.

Wanasiasa acheni kueneza chuki mnaposaka wafuasi – Türk

Haki za binadamu

Takribani nchi 60 duniani kote mwaka huu zikiwa zinajiandaa na chaguzi, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu Volker Türk amezungumzia kitendo cha baadhi ya wanasiasa kuchochea ukosefu wa maelewano na chuki dhidi ya wageni kama njia ya kusaka wafuasi wa kuwaunga mkono.

Akitoa hotuba yake wakati wa mkutano wa 55 wa Baraza La Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu iliyojikita katika hali ya haki za binadamu hivi sasa ulimwenguni, Bwana Türk amesema wanasiasa mara nyingi hujenga chuki miongoni mwa wanajamii hasa nyakati za uchaguzi ili ‘kuvuna’ wafuasi. 

“Katika harakati hizi za kutelekeza maslahi ya wananchi kwa maslahi binafsi mafupi, wanararua kanuni za msingi za binadamu ambazo zinatuunganisha sote,” amesema Kamishna Mkuu huyo.

Sambamba na kauli za chuki nyakati za chaguzi, ameelezea wasiwasi wake mkubwa juu ya kushamiri kwa kampeni za Habari potofu kupitia Akili Mnemba au AI akisema “kuna umuhimu wa kuwekwa kwa mifumo ya udhibiti haraka iwezekanavyo ili kuhakikisha kuna matumizi ya uwajibikaji ya AI au Akili Mnemba. Ofisi yangu inafanya kile iwezalo kusongesha mifumo hiyo.” 

Rushwa ni ‘mwiba’ wa haki kwa wananchi

Amemulika pia rushwa akisema ni changamoto kubwa ya demokrasia ya haki duniani. “Lengo lake kuu ni kupeleka mrama upitishaji maamuzi na  kuona rasilimali za umma zinaelekezwa kule ambako hakuna maslahi ya umma bali maslahi binafsi na hivyo kuchochea ukosefu wa usawa kiuchumi na kijamii.” 

Bwana Türk amesema kitendo hicho kinakwapua fedha za umma na kuwanyima wananchi ambao ni maskini haki ya kujijengea mustakabali wao. 

Mama na watoto wake wakipita katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao huko Goma, mashariki mwa DR Congo.
© UNICEF/Jospin Benekire
Mama na watoto wake wakipita katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao huko Goma, mashariki mwa DR Congo.

Mizozo duniani- DRC na Ethiopa

 Hotuba yake imegusia pia mizozo duniani kuanzia Afrika, Asia, Amerika, Mashariki ya Kati hadi Ulaya akisemaa hakuna kipindi ambacho ubinadamu umekumbwa na majanga yanayofuatana. 

Amesema duniani kote kuna mizozo 55, mizozo inayoambatana na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na ukimbizi. 

Mathalani huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambako hali ni tete na kwamba tarehe 3 mwezi ujao wa Aprili Baraza la Haki za binadamu litamulika. 

Amemulika pia Ethiopia ambayo amesema kuna matumaini kwani hatua zimechukuliwa kutekeleza makubaliano ya mwezi Novemba 2022 ambayo Pamoja na mambo mengine yatana serikali isitishe operesheni zake za kijeshi dhidi ya jeshi la Tigray, TPLF na kuanzishwa kwa serikali ya muda ya jimbo la Tigray. 

“TPLF imesitisha mashambulizi dhidi ya serikali na kusalimisha silaka nzito. Lakini bado hali ya kibinadamu ni mbaya na hakuna hatua za dhati za uwajibishaji. Mapignao yanaendelea kati ya serikali na vikundi vilivyojihami kwenye majimbo ya Amhara na Oromia.” 

Kwa mantiki hiyo amesema ofisi yake siku chache zijazo itatoa ripoti kuhusu hali ilivyo kwenye eneo hilo. 

Amani humea penye haki

Bwana Türk ametamatisha akisema kuwa amani kama ilivyo maendeleo, hujengwa na kustawi kupitia amani. “Ni kwa kuzingatia na kusongesha haki zote za binadamu, ikiwemo haki ya maendeleo na haki ya mazingira safi, yenye afya na endelevu, ndipo nchi zinaweza kuwa na majawabu ya kudumu kwa sababu zinakuwa zinachukua hatua za kufanikisha ukweli halisi wa usawa na matamanio yasiyozimika ya uhuru na haki..” 

Pata hotuba nzima hapa.