Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNEA-6 yahitimishwa kwa kupitisha maazimio 15

Inger Andersen Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP na Leila Benali, Rais wa UNEA-6 wakati wa Kufunga Mjadala katika kikao cha sita cha Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA-6) jijini Nairobi, Kenya.
UNEP/Natalia Mroz
Inger Andersen Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP na Leila Benali, Rais wa UNEA-6 wakati wa Kufunga Mjadala katika kikao cha sita cha Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA-6) jijini Nairobi, Kenya.

UNEA-6 yahitimishwa kwa kupitisha maazimio 15

Tabianchi na mazingira

Mkutano wa 6 wa Mataifa wa Baraza la mazingira duniani, UNEA-6, umefunga pazia leo Ijumaa jijini Nairobi kwa kuidhinishwa kwa maazimio 15 na maamuzi mawili, pamoja na tamko la mawaziri.

Chombo kikubwa zaidi cha uamuzi duniani kuhusu mazingira kimeidhinisha maazimio 15 na maamuzi mawili; dhima zikiwa kuanzia uchimbaji madini hadi uhifadhi wa asili katika maeneo yenye migogoro.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mpango wa Mazingira, UNEP Inger Andersen, amesisitiza kwamba nyaraka zilizopitishwa zinaruhusu maendeleo katika kupata vyuma na madini muhimu kwa mpito wa nishati, hatua bora za kulinda mazingira wakati na baada ya migogoro na kuimarisha udhibiti wa kemikali na taka.

Suluhisho kwa watu na sayari

Inger Andersen amesema tamko la mawaziri linathibitisha "nia thabiti ya jumuiya ya kimataifa kupunguza mabadiliko ya tabianchi, kurejesha asili na ardhi, na kuunda ulimwengu usio na uchafuzi wa mazingira."

Kulingana naye, "mazungumzo hayakuwa rahisi kila wakati", lakini hata kwa kutokubaliana, nchi zilitafuta maelewano.

Mkuu wa UNEP ameongeza kuwa "UNEA-6 imefungua mazungumzo muhimu, ambayo sio yote yamekamilika, lakini nina uhakika yataendelea katika ari ya kutafuta suluhu zinazofaa kwa watu na sayari".

Andersen pia ameangazia umuhimu wa ushiriki wa vijana na kuwashukuru vijana, ambao baadhi yao "wameweka wazi roho zao" kwenye mkutano huo, wakiomba mabadiliko wanayohitaji.

Amesema kuwa roho ya ushirikiano wa nchi nyingi ulikuwa dhahiri katika ushirikishwaji wa mashirika ya kiraia, watu wa asili, mashirika ya kimataifa, wanasayansi na sekta binafsi.

Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP akihutubia wakati wa ufunguzi wa mkutano wa ngazi ya juu katika kikao cha sita cha Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA-6) jijini Nairobi, Kenya tarehe 29 Februari 2024.
© UNEP/Kiara Worth

"Tumefanya kazi ya ushirikiano wa kimataifa" – Rais wa UNEA - 6

Katika hotuba yake ya mwisho, Rais wa UNEA-6, Leila Benali, ameshukuru wajumbe kwa kujitolea kwao kwenye mazungumzo. Amesema kuwa mkutano huo umeacha alama kwenye ajenda ya kimataifa ya mazingira, hata kwa ushirikiano wa nchi nyingi "chini ya shinikizo kubwa". Ameongeza kuwa ushirikiano wa mataifa mengi umefanywa kufanya kazi kwa ubora wake.

Mwakilishi huyo ametumia fursa hiyo kuangazia wasiwasi wake kuhusu mivutano ya kimataifa na mizozo mikuu ya sasa, akitoa wito “bila shaka na uharaka mkubwa wa usitishaji mapigano wa mara moja, wa kina na endelevu. Tunataka amani".

Wauaji wa kimya kimya

Akizungumza na waandishi wa habari, kiongozi huyo wa UNEA-6 amesema kuwa anaamini kuwa hii ndiyo UNEA iliyokuwa jumuishi zaidi ya UNEA zingine na kwamba jambo muhimu zaidi sio wingi bali ubora wa maazimio.

Amesisitiza kwamba "inatia moyo na muhimu sana katika UNEA hii ni ukweli kwamba “tunashughulikia katika baadhi ya maazimio kwa wauaji wa kimyakimya  katika mazingira yetu kama vile dhoruba za mchanga na uchafuzi wa hewa".

Seti ya maazimio ni "fungu linaoshughulikia masuala mbalimbali, kuanzia vyuma na madini hadi migogoro inayotumia silaha". Rais wa ‘bunge hilo’ pia amekumbushia kuwa tamko la mawaziri linaorodhesha hatua 10 ambazo mawaziri wa mazingira wamejitolea kutekeleza.

Kutoridhika na taarifa hiyo

Wakati akitangaza kuidhinishwa kwa maadhimio hayo, Leila Benali ameshukuru wajumbe wote kwa "ushirikiano wao wa kujenga, kubadilika na uelewa wa pamoja".

Baada ya kupitishwa, nchi kadhaa zimeomba kwamba kutoridhika kwao na ukweli kwamba tamko la mawaziri halitaji kanuni ya "Majukumu ya Kawaida lakini yaliyotofautishwa" kuwekwe kwenye kumbukumbu za mkutano.

Kanuni hii inaeleza kuwa pande zote lazima zilinde mfumo wa tabianchi kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo kwa misingi ya usawa na kwa mujibu wa uwezo wao.

Kingine kilichokosolewa ni pamoja na ukosefu wa lugha madhubuti kuhusu njia za kutekeleza malengo ya mazingira.