ITU: Dola bilioni 9 kuwekezwa kwenye mawasilino ya simu duniani
ITU: Dola bilioni 9 kuwekezwa kwenye mawasilino ya simu duniani
Shirika la Umoja wa Mataifa la mawasiliano, ITU limetangaza hii leo kuwa sekta ya simu za mkononi au rununu imeahidi kuwekeza zaidi ya dola bilioni 9 kwa ajili ya kupanua mawasiliano na kuwaunganisha wananchi duniani kote.
Akitangaza uwekezaji huo katika Kongamano la dunia la sekta ya simu MWC lililofanyika huko Barcelona nchini Hispania Katibu Mkuu wa ITU Doreen Bogdan-Martin amesema kuwaunganisha watu wote ulimwenguni ni suala lililo ndani ya uwezo wao. “Shukrani kwa ahadi hizi mpya, mamilioni ya watu watafaidika kutokana na muunganisho unaoweza kufikiwa na wa bei nafuu kote ulimwenguni.”
Mkutano huo unaoelezwa kuwa na manufaa kwa maendeleo ya ulimwengu wa mawasiliano umeelezwa kuongeza idadi ya wadau ambao watasaidia moja kwa moja katika mawasiliano na kuunganisha ulimwenguni kidigitali.
ITU imetangaza licha ya kuwa na nchi wanachama 193 sasa shirika lao litakuwa na uanachama mkubwa zaidi na tofauti katika historia ya mashirika kwani imepata wanachama wapya zaidi ya 1000 kutoka katika sekta mbali mbali ikiwemo wasomi na masharika yanayohusika moja kwa moja na masuala ya mawasiliano.
Kwa mujibu wa takwimu za ITU, watu bilioni 2.6 wanasalia nje ya mtandao ulimwenguni kote.
Kwa vile miundombinu ya mawasiliano ya simu inaunda uti wa mgongo wa muunganisho na mabadiliko ya kidijitali, ni muhimu kwa kuhakikisha kunakuwa hakuna mgawanyiko huo wa kimataifa wa kidijitali na kuondokana na vikwazo vya maendeleo katika maeneo kuanzia ya elimu na afya hadi huduma na biashara za serikali.
ITU imetoa wito wa uwekezaji wa jumla ya dola bilioni 100 ifikapo 2026 ili kutoa utaalam na rasilimali zinazohitajika kupanua muunganisho wa watu wote, wenye maana na mabadiliko endelevu ya kidijitali katika kila kona ya dunia.
Katika mkutano uliofanyika huko Barcelona wadau walifanikiwa kutoa ahadi mbalimbali na kufikisha ahadi za zaidi ya dola bilioni 46 kwa ajili ya uwekezaji uliopangwa katika maeneo ya miundombinu, huduma na usaidizi kwa Muungano wa Kidijitali wa Partner2Connect wa ITU tangu mfumo huo ulipofunguliwa Machi 2022.