Mashambulizi makubwa yakishika kasi Gaza msaada waendelea kupungua: UN
Mashambulizi makubwa yakishika kasi Gaza msaada waendelea kupungua: UN
Shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limesema msaada mdogo sana wa kibinadamu umeingia katika eneo lililozingirwa la Gaza mwezi huu, na kupunguzwa kwa asilimia 50 ikilinganishwa na Januari. alisema Jumatatu.
Hayo yamesema na Kamishina mkuu wa shirika la UNRWA Philippe Lazzarini Akiandika kwenye mtandao wa kijamii wa X, na kuongeza kwamba "msaada ulipaswa kuongezeka sio kupungua ili kukidhi mahitaji makubwa ya watu milioni mbili wa Gaza, ambao wanaishi katika hali mbaya.”
Ametaja baadhi ya vikwazo vinavyokwamisha utoaji wa misaada kuwa ni pamoja na kukosekana kwa utashi wa kisiasa, kufungwa mara kwa mara kwa vituo viwili vya kuvuka katika eneo hilo, pamoja na ukosefu wa usalama kutokana na operesheni za kijeshi na kuporomoka kwa utulivu wa raia.
Amesema “usitishwaji wa mapigano, kuacha kuzingira eneo hilo ili kuruhusu msaada wa maana wa kuokoa maisha na vifaa vya kibiashara, vimechelewa kwa muda mrefu".
Changamoto ya usalama na kufungwa kwa vivuko
Kwa wastani, karibu malori 98 ya misaada yaliingia Gaza mwezi huu, imesema UNRWA katika ripoti yake ya hivi karibuni kuhusu hali ya eneo hilo iliyotolewa Jumatatu.
Shirika hilo limebainisha kuwa shida kubwa katika kuleta vifaa kupitia vivuko vya Kerem Shalom na Rafah ni kutokana na vikwazo vya usalama na kufungwa kwa muda vivuko hivyo.
"UNRWA wakati fulani imelazimika kusitisha kwa muda kutoa vifaa kutokana na wasiwasi wa kiusalama. Usalama wa kudhibiti kivuko hicho umeathiriwa pakubwa kutokana na mauaji ya polisi kadhaa wa Kipalestina katika mashambulizi ya anga ya Israel karibu na vivuko hivi majuzi” limesema shirika hilo.
Shirika hilo limeonya kwamba mbali ya hofu ya vifo vinavyoongezeka kila uchao hivi sasa kuna hatari kubwa ya utapiamlo unaoongezeka.
Ongezeko la mashambulizi ya anga Rafah
Kwa mujibu wa UNRWA operesheni kubwa ya jeshi la Israel na mapigano yanaendelea katika Ukanda mzima wa Gaza na hususan Kaskazini mwa Gaza, kwenye miji ya Deir al Balah & Khan Younis na kuna idadi kubwa ya watu wanaokimbia mapigano.
Limeongeza kuwa watu hao wanaokimbia mapigano makali ndani na karibu na Khan Younis wanaendelea kuelekea kusini zaidi mwa Rafah ambayo tayari imefurika idadi kubwa ya watu.
Takriban Wapalestina milioni 1.5 wanajihifadhi katika mji huo, jambo ambalo linasalia kuwa kitovu cha wasiwasi wa kimataifa huku kukiwa na tishio la mashambulizi ya pande zote za Israel.
"Ongezeko la mashambulizi ya anga huko Rafah, ikiwa ni pamoja na katika maeneo ya makazi ya watu bila onyo au tahadhari ya mapema limeongeza hofu kwamba yataathiri zaidi operesheni za kibinadamu," UNRWA imesema.
Wakati huo huo, watu wamekuwa wakihama kutoka Rafah kuelekea kambi za wakimbizi za Deir Al Balah na Nuseirat katika eneo la Kati la Gaza, ingawa kuna ripoti za mapigano zaidi na mashambulizi ya anga katika maeneo hayo.
Hali ya kibinadamu
Zaidi ya asilimia 75 ya wakazi wa Gaza, ambayo ni hadi watu milioni 1.7, wamekimbia makazi yao tangu kuanza kwa mapigano kufuatia mashambulizi ya kikatili ya kigaidi yaliyoongozwa na Hamas nchini Israel tarehe 7 Oktoba mwaka jana.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaendelea kuonya juu ya kuongezeka kwa mzozo wa njaa huko Gaza.
Zaidi ya watu milioni mbili wanakabiliwa na mgogoro au viwango vibaya zaidi vya uhaba wa chakula, kulingana na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu, OCHA.
Zaidi ya hayo, ni bomba moja tu kati ya mabomba matatu ya maji kutoka Israel ndio linalofanya kazi, lakini chini ya nusu ya uwezo wake, asilimia 83 ya visima vya maji ya chini ya ardhi havifanyi kazi, mifumo yote ya kusafisha maji machafu haifanyi kazi, na hakuna upatikanaji wa maji safi katika majimbo ya kaskazini mwa nchi.