Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuelekea uchaguzi mkuu nchini Sudan Kusini Jean-Pierre Lacroix atathimini hali

Mnamo mwaka wa 2019, watu wapatao 200,000 walikuwa wakihifadhiwa katika vituo vya Umoja wa Mataifa vya ulinzi wa raia huko Sudan Kusini. (maktaba 2017)
UN Photo/Isaac Billy
Mnamo mwaka wa 2019, watu wapatao 200,000 walikuwa wakihifadhiwa katika vituo vya Umoja wa Mataifa vya ulinzi wa raia huko Sudan Kusini. (maktaba 2017)

Kuelekea uchaguzi mkuu nchini Sudan Kusini Jean-Pierre Lacroix atathimini hali

Amani na Usalama

Jean-Pierre Lacroix, Mkuu wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa amewasili jana (18 Feb) nchini Sudan Kusini kutathmini maendeleo yaliyofikiwa kwenye mchakato wa amani na maandalizi yanayoendelea kwa ajili ya uchaguzi ujao uliopangwa kufanyika Desemba, wa kwanza nchini humo tangu uhuru mwaka 2011.

Mjini Juba, anatarajiwa kufanya mikutano na viongozi wa Serikali ya Mpito ya Umoja wa Kitaifa, wawakilishi wa mashirika ya kiraia, na wadau wengine wakuu wanaohusika katika mchakato wa amani.

Lacroix ameandamana na Hanna Serwaa Tetteh, Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu katika Pembe ya Afrika.

Lacroix amesema, “huu ni wakati muhimu kwa Sudan Kusini. Kuna changamoto na pia kuna matarajio katika nyanja nyingi, na nadhani pia ni kielelezo cha mshikamano kutoka kwa Umoja wa Mataifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda Amani nchini Sudan Kusini, Nicholas Haysom, amesema, “hii ni fursa kwa Msaidizi wa Katibu Mkuu katika Operesheni za Ulinzi wa Amani kuona moja ya operesheni kubwa na yenye ufanisi zaidi; ili tumjulishe changamoto tunazokabiliana nazo na shida na kile tunachofanya ili kuzishinda. Lakini pia ana nia ya Abyei na mzozo wa Warrap kati ya Ngok (Dinka) na Twic (Dinka)."

Lacroix ameongeza, "ni wazi kuwa ukanda huo unakabiliwa na changamoto nyingi. Bila shaka, uhasama nchini Sudan una athari kwa Sudan Kusini yenyewe. Kuna changamoto nyingine—kama ulivyotaja—Abyei; na ninaamini matukio mengine kama athari ya mabadiliko ya tabianchi pia yanaathiri nchi hii. Yana athari kwa raia."

Lacroix na Tetteh pia watatembelea ujumbe wa muda wa Umoja wa Mataifa wa mpito kwenye eneo la Abyei lililoko katikati ya Sudan na Sudan Kusini, (UNISFA), na kuzungumza na Msimamizi Mkuu aliyeteuliwa na Juba, maafisa wa utawala walioteuliwa na Khartoum, viongozi wa kimila pamoja na vikundi vya wanawake na wawakilishi wa mashirika ya kiraia.

Pia watatumia ziara hiyo kutathmini hali iliyopo Kusini mwa Abyei kufuatia ongezeko la ghasia kati ya jumuiya ambazo tumeona, pamoja na juhudi zinazoendelea za ujumbe wa kulinda amani kuwalinda raia na kufanya lolote wawezalo ili kupunguza mivutano hiyo kati ya jamii.

Lacroix pia atakutana na walinda amani wanajeshi na wa kiraia nchini Sudan Kusini na Abyei na kuwashukuru kwa kujitolea na huduma yao katika mazingira yenye changamoto nyingi.

Tags: Jean-Pierre Lacroix, Sudan Kusini, UNISFA