DRC: UNHCR yahimiza ulinzi wa raia na upatikanaji wa njia salama za kufikisha misaada
Kufuatia ghasia zilizokithiri wiki iliyopita kati ya vikosi vya serikali na vikundi vya wanamgambo huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo -DRC, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi- UNHCR limeeleza kusikitishwa na athari wanazozipata raia, wakiwemo takriban wakimbizi wa ndani 135,000 walioenda kusaka hifadhi katika mji wa Sake ulio karibu na jimbo la Goma.
Taarifa iliyotolewa leo na UNHCR kutoka Geneva Uswisi imeeleza kuwa shirika hilo na wadau wake wamesikitishwa sana na ripoti za mabomu yaliyoanguka kwenye maeneo ya kiraia, ikiwa ni pamoja na katika eneo la Zaina huko Sake na eneo la Lushagala huko Goma, ambapo wakimbizi wa ndani 65,000 wanahifadhiwa, jambo linalozua wasiwasi mkubwa juu ya usalama wao.
Uwepo wa mabomu ambayo bado hayajalipuka husababisha tishio kwa watoto.
“Wananchi mashariki mwa DRC kwa mara nyingine wanabeba mzigo mkubwa wa mzozo unaozidi kushamiri,” amesema Chansa Kapaya, Mkurugenzi wa UNHCR Kanda ya Kusini mwa Afrika na Mratibu wa Kanda wa hali ya wakimbizi wa DRC.
Mkurugenzi huyo amenukuliwa akieleza kuwa “Makabiliano yasiyokoma karibu na Goma yamelenga wanaume, wanawake na watoto wasio na hatia, na kuwalazimu maelfu kukimbia milipuko ya mabomu na ghasia ovyo. Hali ni ya kusikitisha na haikubaliki. Tunatoa wito kwa haraka kwa pande zote kuwalinda raia, kuheshimu sheria za kibinadamu na kuweka njia salama za kuwafikishia raia misaada.”
Tangu wiki ya kwanza ya Februari, takriban raia 15 wameuawa na wengine 29 kujeruhiwa karibu na Goma na Sake.
Ni ngumu kufikisha misaada ya kibinadamu
UNHCR imesema mashambulizi hayo ya kiholela ya mabomu yanazidisha matatizo katika rasilimali ambazo tayari ni chache ili kuwahudumia wakimbizi wa ndani 800,000 katika eneo hilo, na milioni 2.5 waliokimbia makazi yao katika Mkoa wa Kivu Kaskazini.
Vurugu zinaendelea kuzuia kuwafikia watu waliotengwa katika eneo la Masisi na Rutshuru, na kuongeza changamoto zinazokabili mashirika ya kibinadamu katika kutoa msaada muhimu.
Kukiwa na machaguo machache yanayowezekana kwa sasa ya kupita kwa usalama kutoka Goma, jumuiya zinazoongezeka za wakimbizi zinakabiliwa na hali mbaya na wanahitaji kupatiwa msaada wa haraka.
UNHCR inasisitiza umuhimu wa kulinda maisha na ustawi wa raia na wakimbizi.
UNHCR pia inatoa wito wa kusitishwa mara moja kwa uhasama na kuwe na mazungumzo ya amani ili kutatua mzozo huo na kupunguza mateso ya raia wasio na hatia walionaswa katika ghasia hizo.