Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Japan na UNHCR zatia saini makubaliano ya $360,000 ili kusaidia wakimbizi wanaowasili Tanzania kutoka DRC

Wakimbizi nchini Tanzania waliokimbia makaazi yao kutoka nchi jiranini. (Maktaba)
UNICEF Tanzania/Fredy Lyimo
Wakimbizi nchini Tanzania waliokimbia makaazi yao kutoka nchi jiranini. (Maktaba)

Japan na UNHCR zatia saini makubaliano ya $360,000 ili kusaidia wakimbizi wanaowasili Tanzania kutoka DRC

Msaada wa Kibinadamu

Serikali ya Japan na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, hii leo zimetia saini makubaliano mapya ya ushirikiano utakaowezesha utoaji endelevu wa huduma muhimu ikiwemo malazi, maji safi na salama, na usafi wa mazingira, kwa wakimbizi wanaoendelea kuwasili mkoani Kigoma nchini Tanzania wakitokea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC. 

Taarifa iliyotolewa leo na UNHCR kwa vyombo vya habari imeeleza kuwa mchango wa dola 360,000 kutoka kwa Serikali ya Japan utasaidia kuimarisha huduma za dharura za kuokoa maisha kwa watu wanaokimbia machafuko nchini DRC.

Mwakilishi wa UNHCR nchini Tanzania Bi. Mahoua Parums ameishukuru Japan na kusema kuwa “Mchango huu (kutoka Japan) umekuja katika wakati muafaka na utaturuhusu kuwasaidia wakimbizi kuishi maisha ya heshima wakiwa ukimbizini,”

Akitia saini makubaliano hayo balozi wa Japan nchini Tanzania Yasushi Misawa ameahidi kushirikiana na wadau kama UNHCR kuisaidia serikali ya Tanzania ili iendelee kutekeleza jukumu lake la kuhudumia wakimbizi kwa mujibu wa sheria za kibinadamu za kimataifa. 

“Kwa kufanya kazi pamoja, tunaweza kuleta mabadiliko yanayo onekana kwa maisha ya wakimbizi na kuwaakikishia mustakabali mzuri na salama zaidi,” amesema Balozi Misawa. 

UNHCR inahitaji dola milioni 8 ili kushughulikia mahitaji ya darura ya wakimbizi kutoka DRC nchini Tanzania na imeomba msaada zaidi wa kibinadamu kutoka kwa jumuiya ya kimataifa kadiri mahitaji yanavyoendelea kuongezeka. 

Shukran kwa serikali ya Tanzania

Kwa mujibu wa UNHCR hadi kufikia tarehe 31 Desemba 2023, Tanzania inahifadhi zaidi ya wakimbizi 240,000, hasa kutoka Burundi na DRC.

UNHCR imetoa shukran zake kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo imekuwa mfano wa kimataifa katika kuwakaribisha wakimbizi pamoja na kuendeleza mshikamano baina ya wakimbizi na jamii zinazowapokea.

Mwakilishi huyo wa UNHCR nchini Tanzania Bi. Parums ameeleza kuwa mwaka jana alitembea kambi za wakimbizi huko Kigoma na Nyarugusu na kuzungumza na wakimbizi, wanawake kwa waume na watoto waliokimbia nchi yao ya DRC “Ni watu kama mimi na wewe licha ya kuwa wanawalilia wapendwa wao walipoteza maisha na kupotea, marafiki zao na majirani zao.” 

Mwaka jana 2023, UNHCR na wadau wake wa kitaifa na kimataifa waliisaidia Serikali ya Tanzania kupokea zaidi ya wakimbizi 14,400 waliofika mkoani Kigoma ambao walipatiwa mahali salama pa kulala, chakula, maji na misaada mingine ya kuokoa maisha.