Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR na Benki ya Maendeleo ya Afrika waungana kusaidia wakimbizi nchini Sudan Kusini

Familia ya wakimbizi wa Sudan Kusini wanaorejea wakisubiri katika kituo cha UNHCR cha Renk, Sudan Kusini. (Maktaba)
© UNHCR/Andrew McConnell
Familia ya wakimbizi wa Sudan Kusini wanaorejea wakisubiri katika kituo cha UNHCR cha Renk, Sudan Kusini. (Maktaba)

UNHCR na Benki ya Maendeleo ya Afrika waungana kusaidia wakimbizi nchini Sudan Kusini

Msaada wa Kibinadamu

Vita vinapotokea wananchi wanalazimika kusaka kila namna ya kujilinda na kuokoa maisha yao. Mambo yanapokuwa mabaya watu hao hulazimika kuacha kila kitu nyuma na kukimbia kwenda kusaka hifadhi sehemu nyingine. Watu hao wanapoondoka wanaondoka na ujuzi wao mfano kama alikuwa muuguzi, mfanya biashara, fundi muashi au taaluma yoyote ile. 

Mara nyingi sehemu wanazofikia wakimbizi hao iwe ndani au nje ya nchi zao hujikuta wakipata mahitaji muhimu kwa ajili ya kuishi kama vile chakula cha msaada na matibabu, kiufupi watu hawa hugeuka kuwa tegemezi. 

Huko nchini Sudan Kusini, Benki ya Maendeleo ya Afrika na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR wameamua kwenda mbali zaidi na kuwasaidia wakimbizi kutoka Sudan na wakimbizi wa Sudan Kusini wanaorejea makwao pamoja na jamiii zilizowakaribisha kujiinua kiuchumi

Safari ya kuanza maisha kambi ya wakimbizi 

Kupitia video ya UNHCR inayoanza kwa kuonesha malori manne yakifunguliwa, ndani ya malori hayo wanaonekana watoto, wanaume kwa wanawake wakisaidiwa kushuka, miili yao ikiwa imejaa vumbi jekundu wakiwa na vidumu vya maji, maji kidogo yaliyosalia katika chupa zao na vifurushi vidogo vidogo. 

Baadhi ya wanawake wanaoshindwa kushuka katika lori wanasaidiwa kuwekewa ngazi na wanawake wenzao na kisha wanawashika mkono kuwasaidia kushuka. 

Hapo ni makazi yao mapya, kambi ya wakimbizi ya Gendrassa iliyoko kaunti ya Maban, jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini.

Tangu kuanza kwa vita nchini Sudan zaidi ya siku 300 zilizopita, zaidi ya watu nusu milioni wamewasili nchini Sudan Kusini. Kati ya watu hao takriban watu 100,000 ni wakimbizi wa Sudan na wengine 400,000 ni wananchi wa Sudan Kusini waliokuwa wakimbizi huko nchini Sudan kwa miongo kadhaa na sasa wameamua kurejea nchini mwao. 

Wengi wa watu hao wanarejea katika vijiji ambavyo havina huduma zozote na ambako hakuna msaada wa kibinadamu.

Uwezeshaji kiuchumi

UNHCR pamoja na kutoa misaada mbalimbali ikiwemo huduma muhimu zinazohitajika pindi tu wakimbizi wakiwasili kama vile kuwapatia ndoo, taa, na mablanketi, wameona watu hawa ni vyema kupata msaada wa kuwainua kiuchumi. 

Na wazo hilo ndio linaleta ujumbe wa wafanyakazi wa UNHCR na Benki ya Maendelo ya Afrika- ADB katika kambi hii ya Gendrassa. 

Maafisa hao wanaonekana katika video ya UNHCR wakizungumza na wafanyabiashara, mmoja akionesha kikapu alichokifuma, mwingine akizungumza huku macho yake yakionekana kujaa huzuni ni kama anataka kuanza kulia. 

Marie-Laure Akin-Olugbade kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika analeta habari njema, “Tunatazamia kuwasaidia, kuwawezesha vijana na wanawake katika kambi hii ya wakimbizi na kuwapa fursa, fursa za kuwa wachangiaji chanya katika jamii zinazowapokea na kuleta ujuzi, ujuzi ambao walikuwa nao wakati mzozo ulipotokea walikokuwa wanatoka, na ambao wanaleta kwa jumuiya zinazowakaribisha.”

Naye Kamishna Mkuu Msaidizi wa Operesheni wa UNHCR, Raouf Mazou anasema ziara hiyo imewaonesha namna kulivyo na fursa na changamoto nyingi na kukaribisha wadau wa kimataifa kusaidia.

“Tulichokiona ni kwamba kuna fursa nyingi, miradi mingi ambayo inaweza kufadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika. Tumesikia kutoka kwa mamlaka umuhimu wa kujenga daraja ambalo litapanua ardhi ambayo inapatikana kwa wakimbizi na wananchi wa Sudan Kusini wanaorejea. Tulisikia juu ya uwezekano wa kujenga bwawa ambalo lingepunguza athari za mafuriko ambayo yanaathiri jimbo hili mara kwa mara. Kwa hivyo, haya ni aina ya mambo ambayo sisi watendaji wa mashirika ya kibinadamu hatuwezi kufadhili, hatuwezi kuhamasisha ufadhili. Lakini haya ni aina ya mambo ambayo Benki ya Maendeleo ya Afrika na wadau wengine wa maendeleo wanaweza kufanya.”