Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asante UNICEF kuturejeshea matumaiani ya maisha kwa maji safi: Wananchi Rwanda

Josephine Mukandanga mkazi na mmoja wa wanufaika wa mradi wa maji nchini Rwanda akichota maji safi na salama.
UNICEF Rwanda
Josephine Mukandanga mkazi na mmoja wa wanufaika wa mradi wa maji nchini Rwanda akichota maji safi na salama.

Asante UNICEF kuturejeshea matumaiani ya maisha kwa maji safi: Wananchi Rwanda

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mradi wa ushirikiano wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na serikali ya Japan umerejesha mautumaini ya maisha kwa maelfu ya wananchi wa wilaya za Rutsiro, Nyamasheke na Rusizi nchi Rwanda kwa kuwajengea na kukarabati visima vya maji na hivyo kuwaepusha na magonjwa yatokanayo na maji machafu na adha ya kutembea umbali mrefu kwenda kusaka maji. 

Josephine Mukandanga ni mkazi na mmoja wa wanufaika wa mradi huo wa maji toka wilaya ya Nyamasheke akisema kabla ya mradi huo upatikanaji wa maji ulikuwa mtihani mkubwa kwao. Kwa Josephine kama ilivyo kwa maelfu ya wakazi wengine mradi huo umemletea nuru kubwa. 

“Kutokana na maporomoko ya udongo na majanga mengine ya asili mitambo yote ya maji iliharibika na huduma yetu ya maji kukatika. Na hivyo kulazimika kwenda kuchota maji kwenye visima na mabwawa”

Kupitia mradi huu wa UNICEF na Japani watu zaidi ya 50,000 katika wilaya tatu wamefaidika kwa maji safi na salama na sio tu umewaletea furaha na kupunguza adha ya umbali mrefu kusaka maji pia umewaepusha na magonjwa yatokanayo na huduma duni  za maji , usafi na usafi wa mazingira WASH baada ya miaka mingi.

Kwa Josephine huu ni ukurasa mpya kwa maisha yake na jamii yake.

“Kwa sasa tatizo limetatuliwa. Sasa tuna maji safi ya kutosha kuosha vyombo, kuogesha watoto wetu, kufua nguo zetu na kuoga kuhakikisha miili yetu iko safi.”

Ukosefu wa maji uliwafanya watoto wengi katika wilaya hizo tatu kukosa masomo, kuugua mara kwa mara na kukabiliwa na changamoto nyingine wanapokwenda kuteka maji mbali, lakini sasa wananchi wa wilaya zote tatu wanachosema nishukran kwa serikali yao ya Rwanda, UNICEF na serikali ya Japan kwa kuwapa zawadi ya uhai kupitia maji safi na salama ambayo gharama yake haiwezi kupimika katika maisha yao.