Sudan: Watu milioni 25 wako katika hali mbaya ya kibinadamu
Sudan: Watu milioni 25 wako katika hali mbaya ya kibinadamu
Takriban watu milioni 25 wakiwemo watoto milioni 14 wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu nchini Sudan, tangu mapigano yalipozuka kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na wanamgambo wa kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) mwezi Aprili 2023, wamesema wataalam wa Umoja wa Mataifa.
Taarifa iliyotolewa hii leo na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za binadamu jijini Geneva Usiwisi imewanukuu wataalamu hao wakieleza kuwa Sudan inakabiliwa na moja ya majanga yanayotokea kwa kasi duniani ambapo mpaka sasa watu 13,000 wameuawa na 33,000 kujeruhiwa huku watoto milioni 3 wenye umri chini ya miaka mitano wanakabiliwa na utapiamlo mkali na wanahitaji msaada wa kibinadamu.
Wataalamu hao wamesema “tunasikitishwa sana na kuendelea kutoadhibiwa kwa uhalifu unaofanywa na pande zinazopigana na kutozingatia kwao sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu, hasa kuhusu ulinzi wa raia wakati wa vita. Tunaziomba pande zinazohusika kusitisha mara moja uhasama na kulinda raia, hasa wanawake na watoto, vitu vya kiraia na mali ya kitamaduni, wafanyakazi wa matibabu, wafanyakazi wa kibinadamu na mashirika ya kiraia na kutii wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu na haki za binadamu.”
Wametaka Mazungumzo jumuishi ya kisiasa, yakiambatana na usitishaji mapigano wa kibinadamu, yaanze tena kwa haraka ili kuibadilisha Sudani kuelekea Serikali ya kiraia na kutoa njia ya maendeleo jumuishi na endelevu.
Wamekumbusha ahadi zilizowekwa hadharani na pande zote mbili za kutii haki za binadamu na kuchunguza ukiukaji wowote wa sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu lazima zitekelezwe na uwajibikaji uhakikishwe.
Wametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongezwa ufadhili kwa mashirika ya kiraia ili waweze kuwasaidia wahitaji. Hadi kufikia 21 Januari 2024, ufadhhili uliopatikana ulikuwa ni asilimia 3.1 pekee.
Hali ilivyo sasa nchini Sudan
Watoto
Mgogoro wa kibinadamu unaozidi kuzorota nchini Sudan umesababisha watu wengi kuyahama makazi yao, huku takriban watu milioni 9.05 wakiripotiwa kuwa wakimbizia wa ndani ambao ni takriban asilimia 13 ya wakimbizi wote wa ndani duniani.
Idadi hiyo inawakilisha takriban watoto milioni 4 wakimbizi wa ndani na kuifanya nchi ya Sudan kuwa na mzozo mkubwa zaidi wa kuhama kwa watoto duniani.
Zaidi ya shule 170 nchini kote zimegeuka kuwa makazi ya dharura kwa wakimbizi wa ndani.
Watoto milioni 20 wa Sudan wanaripotiwa kutohudhuria shule, na wanakabiliwa na hatari ya kuuzwa, unyanyasaji wa kijinsia, unyonyaji, kutengana na familia zao, kutekwa nyara, ulanguzi na kuandikishwa na kutumiwa na makundi yenye silaha.
Afya
Msongamano wa watu katika maeneo yanayotoa hifadhi nao unaelezwa kusababisha kuenea kwa haraka kwa magonjwa. Takriban wagonjwa 10,000 wa kipindupindu wameripotiwa na vifo 275 vinavyohusishwa na ugonjwa huo vimeripotiwa kote nchini Sudan ikiwa ni pamoja na katika maeneo ambayo wakimbizi wa ndani wanakimbilia.
Takriban watu milioni 17.7 kote nchini Sudan ambao ni sawa na asilimia 37 ya watu wanakabiliwa na njaa kali.
Upatikanaji wa huduma za afya bado ni mdogo, huku asilimia 70-80 ya hospitali nchini kote zimeripotiwa kutofanya kazi ama kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama, au ukosefu wa vituo vya matibabu katika maeneo ya watu waliohamishwa.
Waathiriwa wa unyanyasaji wa kijinsia hawawezi kupata usaidizi na matunzo wanayohitaji, kutokana na mchanganyiko wa ukosefu wa usalama, ukosefu wa usaidizi wa kutosha wa kibinadamu na ukosefu wa ufikiaji kwa wale walioathiriwa na mzozo na watendaji wa kibinadamu.
“Pande zote katika mzozo nchini Sudan lazima ziruhusu na kuwezesha upitaji salama, wa haraka na usiozuiliwa na utoaji wa misaada ya kibinadamu kwa wakati unaofaa kwa watu wote wanaohitaji, ikiwa ni pamoja na wale waliokwama katika maeneo yenye migogoro na maeneo ya mijini yenye watu wengi." wamesema wataalamu hao.
Wameongeza kuwa wahalifu wa ukiukaji wa haki za binadamu wanapaswa kufunguliwa mashtaka na kupokea adhabu zinazolingana na uzito wa vitendo vilivyofanywa, na waathiriwa wanapaswa kupata malipizi kamili.