Wataalamu wa UN walaani mauaji na kuwanyamazisha waandishi wa habari huko Gaza
Wataalamu wa UN walaani mauaji na kuwanyamazisha waandishi wa habari huko Gaza
Wataalamu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wameeleza kusitikishwa na kulaani vitendo vya waandishi wa habari kuuawa, kushambuliwa, kujeruhiwa na kuwekwa vizuizini huko katika eneo la palestina linalokaliwa kwa mabavu na kutoa wito kwa pande zote kwenye mzozo kuhakikisha wanalinda waandishi wa habari.
Katika taarifa yao kutoka Geneva Uswisi hii leo wataalamu hao wameeleza kupokea ripoti zakusikitisha kwamba licha ya waandishi wa habari kuvaa majaketi, kofia na kuwa kwenye magari ya kuwatambulisha kuwa wao ni vyombo vya habari lakini bado walishambuliwa na kuuawa kitendo ambacho wanaeleza kinaonekana kuwa ni mkakati wa makusudi wa vikosi vya Israel kuzuia vyombo vya habari na kunyamazisha kutolewa kwa ripoti muhimu.
“Tunatoa pongezi maalum kwa ujasiri wa waandishi wa habari na wafanyakazi wa vyombo vya habari huko Gaza ambao wanaendelea kuweka maisha yao hatarini kila siku wanapokuwa kazini, huku pia wakivumilia shida kubwa na kuwapoteza wafanyakzi wenzao, marafiki na familia,” wamesema wataalamu hao.
Wataalamu hao ni Irene Khan Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya uhuru wa kujieleza na kutoa maoni, Francesca Albanese, mtaalam maalum wa haki za binadamu katika ardhi ya Palestina, Mary Lawlor, Mtaalamu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali za watetezi wa haki za binadamu, Tidball-Binz ambaye ni Mtaalamu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu mauaji na ukamataji watu kiholela na Ben Saul Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukuzaji na ulinzi wa haki za binadamu na uhuru wa kimsingi huku akikabiliana na ugaidi.
Wamehimiza pande zinazohusika katika mzozo huko Gaza kuruhusu na kuhakikisha uchunguzi wa haraka, huru unafanyika na usio na upendeleo wa kila mauaji ya waandishi wa habari kwa mujibu wa viwango vya kimataifa, hasa Itifaki ya Umoja wa Mataifa ya Minnesota juu ya uchunguzi wa kifo kinachoweza kutokea kinyume cha sheria.
Taarifa hiyo iliyotolewa na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR imekumbusha kuwa waandishi wa habari wana haki ya kulindwa kama raia chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu “Mashambulizi yanayowalenga na mauaji ya waandishi wa habari ni uhalifu wa kivita”
Israel kuzuia waandishi kutoka nje
Wakati wa migogoro, haki ya kupata habari ni 'haki ya kuishi' ambayo maisha yenyewe ya raia hutegemea, na waandishi wa habari wana jukumu muhimu kama chanzo muhimu cha habari, na kama watetezi wa haki za binadamu na mashahidi wa ukatili, wakiripoti ukiukaji na ukiukwaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu.
Wataalamu hao wameeleza wasiwasi wao mkubwa kwa Israel kwani imekataa kuwaruhusu vyombo vya habari kutoka nje ya Gaza kuingia na kuripoti yanayotokea ispokuwa tu ruhusa hiyo inatolewa iwapo waandishi wa habaro wataunganishwa na vikosi vya Israel.
“Tunaziomba mamlaka za Israel kuruhusu waandishi wa habari kuingia Gaza na kulinda usalama wa waandishi wa habari wote katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu.”
Katika hitimisho la taarifa yao wameitaka Mahakama ya Kimataifa ya Haki na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kuzingatia na kukomesha mtindo hatari wa mashambulizi na kutoadhibiwa kwa uhalifu dhidi ya waandishi wa habari, ambao umeongezeka tangu Oktoba 7 ukilenga na kuua waandishi wa habari wa kipalestina.