Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda akiwa na viongozi wa ngazi za juu wa Wizara hiyo wakati wa Mazungumzo ya Mkakati wa hali ya juu kati ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Washirika wa Maendeleo ya Elimu nchini Tanzania.

Harakati za Tanzania na wadau za kurekebisha mfumo wa elimu

UNESCO
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda akiwa na viongozi wa ngazi za juu wa Wizara hiyo wakati wa Mazungumzo ya Mkakati wa hali ya juu kati ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Washirika wa Maendeleo ya Elimu nchini Tanzania.

Harakati za Tanzania na wadau za kurekebisha mfumo wa elimu

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mazungumzo ya kimkakati ya ngazi ya juu kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania na wadau wa maendeleo yalifanyika nchini humo tarehe 24 mwezi Novemba mwaka jana wa 2023 yakiangazia mwelekeo wa marekebisho ya mfumo wa elimu katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Wadau hao wa elimu kwa mujibu wa makala iliyochapishwa na UNESCO ambaylo ni shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni,  ni wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na yale ya kimataifa yakiunda kwa pamoja Kundi la Wadau wa Maendeleo ya Elimu Tanzania Tanzania Bara, EdDPG ambapo walikuwa na kikao na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda akiwa sambamba na watendaji wa ngazi za juu za wizara hiyo. 

Lengo kuu la mkutano huu lilikuwa kushughulikia masuala muhimu yanayohusu mageuzi yanayoendelea ya Sekta ya Elimu Tanzania Bara. Tangu Septemba mwaka wa 2022, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO lilishika uenyekiti wa EdDPG, ambalo huleta pamoja mashirika yanayotoa msaada kwa sekta ya elimu Tanzania Bara na Tanzania Visiwani.

Washiriki wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa mkutano na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Tanzania.
UNESCO
Washiriki wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa mkutano na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Tanzania.

EdDPG ilianzishwa mwaka 2001, lengo kuu likiwa ni kuwezesha afua zilizoratibiwa na mazungumzo ya kisera miongoni mwa washirika wa maendeleo, yenye lengo la kusaidia sekta ya elimu Tanzania katika kufikia matokeo ya kujifunza yanayowiana na Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs.

Profesa Mkenda na dhamiri ya kuona elimu bora Tanzania

Wakati wa hotuba yake, Profesa Mkenda alitoa shukrani zake za dhati kwa wakuu wa mashirika kwa ushiriki wao wa dhati katika mageuzi ya elimu, akisisitiza dhamira yake isiyoyumba katika kuimarisha mazingira ya elimu nchini Tanzania. 

Aliidhinisha toleo la mwaka 2023 la Sera ya Kitaifa ya Elimu na Mafunzo ya mwaka wa 2014, kutoa maarifa kuhusu muundo na mtaala mpya wa elimu. Profesa Mkenda alibainisha changamoto kubwa ya ukosefu wa walimu wa kutosha, akisisitiza umuhimu wa jitihada za ushirikiano ili kuondokana na kikwazo hiki katika utekelezaji wa sera iliyoidhinishwa. 

Alitoa wito wa kuwepo kwa ushirikiano endelevu ili kuhakikisha ongezeko la upatikanaji wa elimu bora, bila kumwacha mtu nyuma katika kutafuta ubora wa elimu. 

Mashirika ya Umoja wa Mataifa kwenye kundi hilo ni pamoja na lile la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, la kuhudumia watoto, UNICEF, la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, shirika la Fedha Duniani, IMF, na Benki ya Dunia.

Wadau wengine ni mashirika ya kimataifa ya maendeleo likiwemo lile la SWeden, SIDA, la Marekani, USAID, la Korea Kusini, KOICA, lile la Uswisi, la Ujerumani, DVD, la Uswisi, SDC, pamoja na taasisi ya Agakhan, na wanachama wengine wa EdDPG. 

Mwakilishi wa WFP nchini Tanzania, Bi.Sarah Gordon-Gibson (anayezungumza), wakati wa Mazungumzo ya Kimkakati ya  ngazi ya juu kati ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Washirika wa Maendeleo ya Elimu nchini Tanzania.
UNESCO
Mwakilishi wa WFP nchini Tanzania, Bi.Sarah Gordon-Gibson (anayezungumza), wakati wa Mazungumzo ya Kimkakati ya ngazi ya juu kati ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Washirika wa Maendeleo ya Elimu nchini Tanzania.

Tunashikamana na serikali ya Tanzania kuboresha elimu- UN

Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP nchini Tanzania, Bi. Sarah Gordon-Gibson, akimwakilisha Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa, alisisitiza kuwa mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania yanashikamana na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Amesema dhamira hiyo ya pamoja inatokana na Mpango wa Ushirikiano kwa Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, UNSDCF, 2022-2027, unaoakisi kujitolea kwa pamoja katika kuleta mabadiliko katika sekta ya elimu.

“Mpango huo ulizinduliwa na Makamu wa Rais wa Tanzania Phillip Mpango mwaka jana, ukielezea mwitikio wetu wa pamoja wa kuchangia kwa ufanisi na umakini zaidi ili kufikia Ajenda ya mwaka wa 2030 ya Maendeleo Endelevu nchini Tanzania,” alisema Bi. Gordon.

Michel Toto, Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa UNESCO nchini Tanzania na Mwenyekiti wa EdDPG, akizungumza kwa niaba ya kundi hilo alitambua hatua nzuri ya serikali katika utengaji wa bajeti ya elimu, sekta katika miaka michache iliyopita. Alisisitiza umuhimu wa kuongeza bajeti ya elimu kutoka asilimia 18 hadi kiwango kilichopendekezwa cha asilimia 20 ili kuharakisha uboreshaji wa matokeo ya sekta ya elimu. 

Bw. Michel Toto, Mkuu wa Ofisi ya UNESCO na Mwakilishi Mkazi wa shirika hilo Tanzania
UNESCO
Bw. Michel Toto, Mkuu wa Ofisi ya UNESCO na Mwakilishi Mkazi wa shirika hilo Tanzania

EdDPG imedhamiria kusidia mageuzi ya elimu

Bw. Toto alisisitiza dhamira ya EdDPG ya kusaidia mageuzi na maendeleo ya sekta ya elimu Tanzania. Zaidi ya hayo, aliangazia usaidizi wa UNESCO kupitia taasisi zake maalum ikiwa ni pamoja na ile ya Kimataifa ya Mipango ya Elimu, IIEP, Taasisi ya UNESCO ya Takwimu UIS, Ofisi ya Kimataifa ya Elimu, IBE, na Taasisi ya Kimataifa ya Kujenga Uwezo Afrika, IICBA.

“Tunapongeza juhudi za serikali za kuboresha na kuongeza upatikanaji wa ubora wa elimu katika ngazi zote. Ulimwenguni, tumetekeleza kwa asilimia 50 lengo la 4 la Malengo ya Maendeleo Endelevu linalomulika elimu, ambalo linalenga kuhakikisha elimu bora, endelevu, jumuishi na sawia, na inayokuza fursa za kujifunza maishani kwa watu wote. Lengo hili ni msingi wa dhamira yetu ya pamoja,” alitamatisha Mkuu huyo wa UNESCO nchini Tanzania.